Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Spika Sitta: Sikilizeni maoni ya viongozi wetu wa dini

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SPIKA wa Bunge, Samwel Sitta amewataka viongozi nchini kusikiliza maoni ya viongozi wa dini na kwamba wanasiasa wanapaswa kuwa wasafi.

Spika Sitta aliyasema hayo jana wakati akichangisha harambee ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kisasa inayotarajiwa kujengwa Kitunda jijini Dar es salaam na masista wa shirika la wabenekitini la mtakatifu Agnes lililopo Chipole mkoani Ruvuma.

Alisema viongozi wa dini wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika ujenzi wa shule, zahanati, hospitali, kutunza yatima na kufanya shughuli mbali mbali katika jamii na kwamba mchango huo, unafurahiwa na viongozi wa siasa.

Alisema kanisa katoliki nchini limefanya mambo mengi mazuri na watu wengi wamepata elimu kupitia shule za kanisa hilo, pia baadhi ya shule bora hapa nchini zimekwa zikimilikiwa na kanisa hilo.

Alisema pia zahanati na hospitali nyingi nchini ni ubia kati ya serikali na kanisa katoliki na kwamba kupitia vituo hivyo, wananchi wamekuwa wakipata matibabu ya uhakika.

"Sisi viongozi tuwe na moyo wa kuwasikiliza viongozi wa dini tupokee maoni kutoka kwa watu mbalimbali, mengine yanaweza kuwa ya mekosewa kwa sababu sitegemei askofu anaelewa utendaji kazi katika ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, lakini anapotoa maoni ya kujenga ni lazima tuyafuate,"alisema Sitta.

Aliwataka viongozi wa madhehebu yote ya dini wasisite kukosoa viongozi wa siasa kwani ni haki yao na kuwashauri viongozi hao kujenga tabia ya kuwasikiliza viongozi wa dini wanapozungumzia maadili ya dini.

Awali Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea Norbert Mtega alisema wameamua kujenga kanisa hilo, Dar es salaam badala ya Songea kwa kuwa kanisa katoliki lipo kwa ajili ya Taifa zima na litaendelea kutoa huduma sehemu yoyote duniani hivyo ni wajibu kusaidia jamii na kuwataka watu wote wenye uwezo wa kuchangia wasaidie kutoa michango ili wafanikishe ujenzi wa hospitali hiyo.

Aliwataka masista hao, kuwaombea daima wahisani wao ambao wamewasaidia kuchangia ujenzi huo ili waweze kufika mbinguni pia amewataka waendelee kutoa huduma bora kwa jamii, ikiwemo elimu, afya pamoja na kutunza yatima na maskini kwani wao ni wamisionari na kazi yao ni kutoa huduma na kuombea watu.
Tags:

0 comments

Post a Comment