Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk. Slaa afanya kufuru Karatu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter • ATAMBA CCM HAITAICHUKUA KARATU


MBUNGE wa Karatu na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, jana alitikisa mji wa Arusha na Karatu, baada ya kupata mapokezi makubwa ambayo yaliwafanya baadhi ya watu kusimamisha shughuli zao.

Dk. Slaa ambaye wiki iliyopita aliteuliwa na CHADEMA kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, amekuwa gumzo kubwa na anatarajia kutoa upinzani mkubwa kwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi.

Tangu kutajwa kwa jina la Dk. Slaa kuwania nafasi hiyo, wadadisi wa masuala ya siasa wameelezea hatua hiyo kuwa ni mabadiliko makubwa, huku wakiongeza kuwa wanatarajia kinyang’anyiro hicho kitakuwa kigumu zaidi, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2005, ambapo Rais Kikwete alishinda kwa asilimia zaidi ya 80.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu ateuliwa kuwania urais na CHADEMA, kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Bwawani, mjini Karatu, Dk. Slaa alisema amekubali kuchukua jukumu hilo zito ili kuwakomboa Watanzania.

Alisema taifa kwa sasa linaelekea kubaya, hivyo linatakiwa kukombolewa na kiongozi makini na yeye amekubali kulibeba jukumu hilo ili Watanzania wafurahie rasilimali zao ambazo kila kukicha zinatafunwa na watu wachache.

“Nawashukuru sana, wana Karatu kwa kunilea, nimekuwa mpaka taifa limeniona, nilikuwa na majonzi kila nilipofikiria kuwaacha, nimekuwa nanyi kwa miaka 15, sasa nimekubali kwa nia moja baada ya ninyi kuridhia uamuzi huu,” alisema Dk. Slaa.

Alisema mahitaji ya Watanzania ni makubwa lakini wamekuwa wakibanwa mno na CCM kutokana na sera zisizozingatia masilahi ya wananchi walio wengi huku masilahi ya wachache yakilindwa.

“Watanzania wamekandamizwa mno kutokana na sera mbovu za CCM kwa kipindi cha miaka karibu 50, wameporwa haki, hakuna utawala wa sheria na utawala bora,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kamwe CCM wasitegemee hata kidogo kuchukua jimbo hilo ambalo linaonekana kuwa ngome kuu ya CHADEMA, kwa kuwa chama hicho kimejizatiti vya kutosha kumsimamisha mgombea makini na anayekubalika kwa jamii.

Awali wakati wa mapokezi ya Dk. Slaa, mamia ya wananchi wa mji wa Arusha na Karatu walisimamisha shughuli zao za uzalishaji mali kwa muda ili kushiriki tukio hilo walilolielezea kuwa ni la kihistoria.

Baadhi ya watu walisema wana imani kubwa kuwa Dk. Slaa ataibuka na ushindi kutokana na uwezo mkubwa wa kujenga na kusimamia hoja.

Katika hatua nyingine, wazee wa wilaya hiyo walimchagia Dk. Slaa sh 200,000 kwa ajili ya kuchukulia fomu za kuwania urais.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema siku za Rais Jakaya Kikwete kukaa Ikulu zinahesabika, kwa sababu chama chake kimemsimamisha mgombea makini zaidi, ambaye wana uhakika anachagulika na kupendwa na wananchi.

“Wana wa Karatu napenda kuwaambia leo kuwa siku za Rais Kikwete kukaa Ikulu zinahesabika, umefika wakati wa kufungasha virago vyake, tunampeleka mtu makini kuingia pale,” alisema Mbowe.

Alisema zama za siasa za kulindana sasa zimekwisha, na kwamba kazi iliyobaki ni wananchi kufanya maamuzi magumu.

Alisema kutokana na hali hiyo, CCM imejawa na wasiwasi mwingi baada ya Dk. Slaa kutangazwa kugombea nafasi hiyo.

“Nawaambia Rais Kikwete na serikali yake hivi sasa wamejawa na wasiwasi mwingi, tunasema kazi ni moja, hakuna kulala mpaka kieleweke,” alisema Mbowe.

Alisema chama hicho kilifikia uamuzi wa kumteua Dk. Slaa baada ya utafiti wa kina uliofanywa na wataalamu wa chama hicho, uliobaini kuwa kiongozi huyo machachari anafaa.

Dk. Slaa aliingia mjini Arusha majira ya saa 7 mchana na kupokewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha.

Baada ya hapo, msafara wake uliondoka kuelekea Karatu ukiwa na magari zaidi ya 80, pikipiki zaidi ya 150 na baiskeli nyingi, huku mamia ya wananchi wakiwa wameshika matawi ya miti, ikiwa ni ishara ya kumshangilia.

Wakati msafara huo ulipowasili eneo la Mto wa Mbu, hali ilibadilika kutokana na mamia ya watu kujitokeza na kuungana na msafara huo, hali iliyosababisha kila kona shughuli mbalimbali kama biashara kusimama kwa muda.

Hali iliyoendelea kubadilika baada ya msafara huo kuingia katika mji wa Karatu, ambako shughuli karibu zote zilisimama, huku mamia ya wananchi wakikimbilia eneo ambalo lilikuwa limeandaliwa kwa ajili ya mkutano.

Leo msafara wa chama hicho unaendelea na mikutano yake wilayani hapa kwa kupita kata hadi kata kwa ajili ya Dk. Slaa kutoa neno la kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo.
Tags:

0 comments

Post a Comment