You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - SIMBA kuweka kambi Ujerumani Kukabiliana na YANGA. TFF yaipuuza Simba SC
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema halitabadilisha ratiba ya michezo ya Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na timu hiyo kudai kutaka kuweka kambi nchini Ujerumani.
Hatua hiyo ya TFF imekuja siku moja baada ya Simba kudai itaweka kambi ya wiki mbili Ujerumani kabla ya kukutana na watani zao wa jadi Yanga katika mchezo wao wa kwanza wa ligi hiyo Oktoba 26 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema hawatabadili ratiba kwa kuwa timu fulani inataka kuweka kambi nje ya nchi, kwani walitoa muda mwingi wa timu kujiandaa.
Alisema kama Simba inaona ratiba itawaruhusu kufanya hivyo, basi waendelee na maandalizi hayo wanayoyataka, lakini si kubadilisha ratiba yao, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa hawakuzitendea haki timu nyingine.
''Hatuwezi kubadilisha ratiba kwa sababu timu inataka kuweka kambi nje ya nchi, sisi hilo halituhusu, ila kama wao wanaona muda utawaruhusu kufanya hivyo, basi wafanye kwani tulishatoa muda mwingi kwa klabu mbali mbali kujiandaa,'' alisema Mwakalebela.
Jana Katibu Mwenezi wa Simba, Said Rubeya alikaririwa na gazeti hili akisema wanajipanga kuiomba TFF iwape muda wa wiki mbili kwenda Ujerumani kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga.
0 comments