KUNDI la waumini wa Dhehebu la Waadventista Wasabato Masalia, kwa mara ya tatu limesambaratishwa na askari wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, baada ya kurudi tena uwanjani hapo huku wakiwa wameongezeka idadi yao kutoka 17 hadi kufikia 51.
Wasabato hao masalia, walifika katika uwanja huo mnamo saa 2:00 asubuhi huku wakiwa na mabegi yao tayari kwa safari wakisema: "Bwana alikuwa amewaambia tena kuwa jana ilikuwa ndio siku ya kuondoka na kuelekea nchi za Ulaya kuhubiri injili."
Mara baada ya kufika uwanjani hapo, askari wa uwanja huo wa ndege waliwauliza kwa lengo la kutaka kujua endapo awamu hii wamejikamilisha tayari kwa safari, lakini cha kushangaza waumini hao waliendelea kutoa majibu yale yale kwamba wao tiketi yao na hati za kusafiria ni Biblia.
Baada ya kujibiwa hivyo, askari hao waliamua kuorodhesha majina ya waumini hao na kuchukua jukumu la kuwapiga picha mmoja mmoja na kuwaamuru watoweke katika viwanja hivyo.
Kama ilivyokawaida ya waumini hao, pindi wanapotaka kufanya jambo lao lazima wainamishe vichwa vyao chini na kupiga magoti huku wakimuomba Mungu kimya kimya, ndivyo walivyofanya jana nje ya geti la kuingilia uwanjani hapo.
Baada ya kusali kwa dakika chache, waumini hao walianza safari ya kurudi katika eneo lao waliloweka kambi ambalo ni Tabata Magumi, ambapo waliondoka kwa maandamano huku wakiimba wimbo wao ambao ulikuwa una ujumbe usemao: “Tunasubiri Mavuno”.
Waumini hao wakati wakiondoka kwa maandamano, walisindikizwa na kundi la askari wa uwanja wa ndege, ambao walipofika barabara ya Nyerere, askari hao walizuia magari kwa muda wa sekunde kadhaa ili kundi hilo la waumini liweze kuvuka.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Mkuu wa Kituo cha Polisi cha uwanja huo wa ndege Saimoni Haule, alisema aliwapiga picha ili sura zao ziwe kumbukumbu na endapo wataonekana tena katika maeneo ya uwanja huo hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao.
“Sasa tumewaambia kuwa hii ni mara ya mwisho kwao kuja hapa, endapo tutaona tena sura zao hapa ndipo watakapo tutambua sisi nani,” alionya Kamanda Haule.
Haule alisema anasikitishwa kuona katika kundi hilo kuna watoto, ambao wangestahili kuwepo shuleni kwa kipindi hiki ukilinganisha na umri wao.
Hata hivyo, waumini hao walipoulizwa kuhusiana na msimao wao sasa, walisema msimamo wao kwenda Ulaya kuhubiri injili upo palepale hawajakata tamaa na kwamba wanaendelea kumsikiliza mungu atakachowaambia.
“Safari bado ipo, hata hivi unavyotuona tupo safarini hatujakata tamaa tunamsikiliza bwana, ”alisema mmoja wa waumini hao ambaye hakutaka kutaja jina lake, ila alisema yeye ni Mwinjilisti
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Abbas Kandoro, alisema kundi hilo la waumini analichukulia kama ni kundi la wazururaji pia wanakiuka sheria za nchi hivyo ni lazima atawachukulia hatua za kisheria.
“Kama unavyoelewa, serikali inapiga marufuku kitendo cha watu kuwatorosha wanafunzi shule sasa waumini hao wana watoto ambao wanahitajika kuwepo shule kwa sasa, lazima niwafuate huko waliko,”alisema Kandoro.
Kandoro aliongeza kwamba, anataka kujua kama dhehebu hilo limesajiliwa kisheria kutokana na imani yao ambayo watu wengi wameonekana kutokuielewa vizuri na kugeuka mshangao kwa kila mtu wa kizazi hiki.
Awali, Kandoro aliwapiga marufuku waumini hao kufika katika viwanja vya ndege kwani eneo hilo si la mchezo kama wanavyodhani.
Waumini wa Dhehebu la Waadiventista Wasabato Masalia, hivi sasa wameingia mwezi wa tatu tangu waweke kambi katika jiji hili la Dar es salaam, walifika kwa lengo la kusafiri kwenda nchi za Ulaya pasipokuwa na nyaraka zozote za kusafiria.
Awali, waumini hao idadi yao ilikuwa 17 lakini wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku na sasa kufikia idadi ya watu 51, wameshafika katika uwanja huo wa ndege mara tatu kwa lengo la kusafiri pasipokuwa na nyaraka za kusafiria, mara zote hizo uongozi wa uwanja wa Ndege uliwafukuza katika eneo hilo.
0 comments