Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Wingu lagubika mabilioni ya rada

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo
WINGU zito limetanda kuhusu malipo ya Paundi 29.5 milioni (Sh80 bilioni), ambazo zinatokana na malipo ya ziada ya ununuzi wa rada kati ya Serikali na Kampuni ya BAE Systems baada ya Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo kutoa taarifa zinazokinzana.


Wakati Desemba 6, mwaka jana alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema tayari fedha hizo zilikwishaingizwa kwenye akaunti ya Benki Kuu Tanzania (BoT), Akaunti ya London, Uingereza, juzi aligeuka na kusema fedha hizo bado hazijalipwa.


Aidha, Februari mwaka jana, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema tayari Serikali imezielekeza fedha hizo kutatua kero kwenye mipango ya elimu nchini na mojawapo ni kutengeneza madawati.


Lakini, juzi akizungumzia mchakato huo wa urejeshaji wa fedha hizo, Waziri Mkulo alisema bado fedha hizo hazijaingia mikononi mwa Serikali ya Tanzania na mawasiliano bado yanaendelea.


Alipoulizwa ilikuwaje mwaka jana alisema fedha hizo zimeshaingizwa BoT, alijibu: “Vyombo hivyo vili ni-misquote (nukuu vibaya). Lakini ukweli ndiyo huu ninaokuambia leo… fedha hizo bado hazijaingia,” alisema Mkulo.
Mkulo alisema sababu za fedha hizo kutoingia kwenye akaunti hadi sasa alisema ni kutokamilishwa kwa taratibu za kifedha kati ya Serikali za Tanzania na Uingereza.


“Unajua kila Serikali ina taratibu zake za kifedha. Lakini naweza kusema tumefikia mahali pazuri tu. Ni kwamba kwa sasa process (mchakato) zimefikia katika kiwango cha hali ya juu,” alisema.


Hata hivyo, alisita kusema ni lini taratibu hizo zinaweza kukamilika na fedha hizo kuingia serikalini tayari kutumika kwa ajili ya kutatua matatizo katika sekta ya elimu kama ilivyokwishaamua.Mkulo alisema kimsingi, hakuna tatizo lolote lililojitokeza katika utekelezaji wa taratibu hizo za kukabidhi fedha hizo ingawa alisema hajui lini zitakamilika.


“Hakuna tatizo… Itakapokuwa tayari tutaitisha ‘press conference’ (mkutano na waandishi wa habari), tutaita vyombo vyote na kuwaeleza,” alisema.


Akizungumzia suala hilo, Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu hata kama anajua kinachoendelea, hawezi kusemea jambo hilo kwa kuwa hana mamlaka kwa mujibu wa taratibu za kibenki.


“Taratibu zinakataza benki kutoa taarifa za akaunti ya mteja. Serikali ni mteja wetu. Siwezi kuzungumzia lolote kuhusu akaunti yake. Serikali ndiyo yenye mamlaka kuhusu hilo.”


Biashara ya rada
Mchakato wa biashara hiyo ya rada kati ya Serikali na BAE Systems, ulifanyika kuanzia mwaka 1999 hadi 2002 na uliibua mvutano katika Serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.


Wakati nchini Uingereza suala hilo likiibua utata mkubwa uliowahi kumfanya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short kujiuzulu wadhifa huo, Tanzania moto huo wa rada umekuwa ukiwaka na kuzimika.


Kashfa hiyo ilimfanya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge kujiuzulu wadhifa Aprili 21, 2008 baada ya kukutwa na kiasi cha fedha Sh1.2bilioni alizokuwa amezihifadhi katika kisiwa cha Jersey.


Fedha hizo zilikutwa kwenye akaunti hiyo baada ya upekuzi uliofanywa na Taasisi ya Kushughulikia Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza na Chenge alipoulizwa, alijibu: “Hivyo ni vijisenti,” kauli ambayo iliibua hasira za Watanzania na kushinikizwa ajiuzulu.


Hata hivyo, kujiuzulu kwa Chenge ambaye wakati wa biashara hiyo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kulitoa nafasi ya SFO na Takukuru kufanya uchunguzi zaidi lakini hadi sasa hakuna aliyeshtakiwa.


Mwaka jana, suala hilo liliibuka bungeni baada ya Mahakama ya Uingereza kutoa hukumu kwa BAE Systems kurejesha mabilioni hayo kwa Serikali ya Tanzania. Baada ya hukumu hiyo, BAE Systems ilitaka ilipe kupitia misaada yake kwa mashirika ya hisani ya Uingereza yanayofanya kazi nchini.
BAE iliweka shinikizo hilo ikidai inafanya kazi na Serikali ya Uingereza kupitia wizara yake ya Maendeleo ya Kimataifa kutoa malipo hayo kulingana na utaratibu wao na isingeweza kulipa fedha hizo moja kwa moja kwa Serikali.


Lakini, Bunge la Tanzania liingilia kati na kutuma ujumbe wa wabunge watano ukiongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai kuishawishi Serikali ya Uingereza iishinikize BAE Systems kurejesha fedha hizo kupitia mkondo uleule zilikotoka ambao ni serikalini.


Uamuzi huo wa Uingereza kurejesha fedha hizo unakwenda sambamba na ombi lake la kutaka watuhumiwa wote hapa nchini waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba washtakiwe Tanzania au Uingereza baada ya kubainika dosari kwenye ununuzi huo ambao kama ungefanyika kihalali ungegharimu Pauni 10.5 milioni, kununua rada mpya.


Hata hivyo, Mkurugenzi Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema taasisi yake imeshindwa kuwapeleka mahakamani watuhumiwa kwa sababu hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kuna Mtanzania aliyekula rushwa kwenye ununuzi huo wa rada.


Kampuni ya BAE ilishutumiwa na wabunge wa Uingereza kwa kujivuta kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

0 comments

Post a Comment