Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Meya: Magufuli acha ubabe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SIKU moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kuamuru mabango yaondolewe barabarani, Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa amemtaka waziri huyo kuacha ubabe katika utekelezaji wa majukumu yake badala yake atumie vikao rasmi kutoa matamko yake.


Juzi wakati akizindua kituo cha daladala Mbezi, Dk Magufuli alitoa siku tano kwa wakala wa barabara (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam kuondoa wafanyabiashara na mabango yote yaliyojengwa pembezoni mwa barabara ili kukabiliana na msongamano.


Akizungumza ofisini kwake jana, Silaa alisema viko vikao vya bodi ya barabara na vya kamati ya ushauri ya mkoa ambavyo vyote vinaongozwa na mkuu wa mkoa na kwamba waziri huyo anaweza kuvitumia kupeleka hoja zake na kujadiliwa.


“Nchi hii siyo ya kwake na lazima atambue kuwa halmashauri zote ziko kisheria hivyo atumie vikao rasmi kutoa maagizo yake,”alisema Silaa. Alisema waziri huyo anatumia sheria ya barabara ya mwaka 2007 na kwamba kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo kulikuwapo na sheria nyingine ambazo hadi leo bado zinatumika hivyo anatakiwa aziheshimu.


Alisema miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini ni wenye mabango hivyo kutaka kuyaondoa ni sawa na kuhujumu maendeleo.Kwa mujibu wa meya huyo fedha za mabango zimekuwa zikitumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama shule, barabara na hospitali.


Alisema watu wenye mabango wana mikataba halali na halmashauri na wanaotangaza kwenye mabango hayo wana mikataba halali na wenye mabango hayo na kwamba kuyaondoa ni kusababisha usumbufu usiokuwa wa lazima katika mikataba hiyo.


Kuhusu suala la kutochaji ushuru katika kituo cha Mbezi, Meya huyo alisema suala hilo siyo sahihi kwani kuna gharama mbalimbali za uendeshaji ambazo zitatakiwa kulipwa.


Kwa mujibu wa meya huyo gharama hizo ni walinzi na uendeshaji wa choo ambao alisema zinaweza kulipwa na ushuru utakaokuwa unatozwa.


Katika hatua nyingine, halmashauri hiyo imesema itawashtaki wamiliki wa mabango ya biashara walioshindwa kulipa ushuru ambao unafikia Sh984 milioni. Silaa alisema karibu kampuni 20 zinadaiwa ushuru wa mabango na halmashauri hiyo zikiwamo kampuni ya simu za mkononi, kampuni ya vinywaji na kampuni zinazohusika kuweka mabango.


Alisema wameamua kuwashtaki baada ya kuzungushwa kwa muda mrefu na wamiliki hao ambao kila wanapofuatwa wamekuwa wakidai kuwa hawana fedha.

0 comments

Post a Comment