Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Pinda:Hatuwang'oi Mawaziri wa Afya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAKATI madaktari wakisisitiza kufanya mgomo waliouita wa kihistoria kuanzia leo kushinikiza kuondolewa madarakani kwa Waziri wa Afya, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewasihi wataalamu hao wa afya kutochukua hatua hiyo kama kweli wana nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi.
Jana, madaktari hao walibandika mabango katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakisisitiza kuanza mgomo huo leo hali ambayo imezua kutaharuki kubwa miongoni mwa wagonjwa na jamaa zao. Muhimbili ndiko kulikokuwa chimbuko la mgomo wa madaktari uliofanyika mwezi uliopita.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Waziri mkuu Pinda alisema Serikali haioni sababu ya kuwawajibisha mawaziri hao kwa sasa na kueleza kushangazwa kwake na hatua ya madaktari hao kugeuza suala hilo kuwa dai namba moja hivi sasa.


“Hivi kweli mnataka nifike mahali nimwaambie Rais (Jakaya Kikwete) tunakupa saa 72 uwafukuze kazi viongozi hao? Hapana... hapana... hapana kwa lipi hasa? Siwezi kumwambia atekeleze hayo. Ingekuwa hatujafanya chochote sawa, hata angekuwa mtu yeyote hawezi kukubalina na hayo unless (vinginevyo) wenzetu madaktari watuambie wana hoja nyingine.”


Pinda alisema Dk Mponda mwenyewe anayelalamikiwa ndiyo kwanza ana mwaka mmoja na nusu kazini na hata madai mengine hayajui kwa kuwa hakuwepo wakati huo akisema shinikizo la kutaka awajibishwe ni kumuonea.


Alipoulizwa endapo mawaziri hao wataamua kuwajibika wenyewe ili kunusuru maisha ya Watanzania Serikali itakuwa tayari kwa hilo, Pinda alihoji: “Kwa lipi hasa? Naona ni vyema tusubiri majadiliano, hayo yote yatajulikana baada ya kufikia mwisho.”


Waziri Mkuu aliwataka madaktari kutumia busara, hekima na uzalendo na kuendelea na kazi kama kawaida wakati Serikali inaendelea na majadiliano na viongozi wao.


“Nawapa rai ndugu zetu madaktari wasigome kama wanavyodhamiria kufanya kwa sababu watawaumiza watu wasio na hatia, turudi tuweze kukamilisha majadiliano tuliyoyaanza,” alisema Pinda.


Alipoulizwa kuhusu hatua ambazo Serikali itachukua endapo madaktari hao watagoma leo alijibu: “Tuache tuone, tukiamka asubuhi (leo) kama ni ngangari itabidi sisi kama Serikali tutaangalie cha kufanya.”


Alisema sheria imeweka bayana kuwa watu wanaotoa huduma katika maeno nyeti hawapaswi kugoma kwa kuwa kufanya hivyo wanahatarisha usalama, afya na maisha ya watu.


Alizitaja huduma hizo muhimu kuwa ni pamoja na maji na usafi, umeme, afya na maabara, zimamoto, udhibiti wa safari za anga na mawasiliano ya ndege za kiraia na huduma yoyote ya usafiri inayohitajika kwa ajili ya kutoa huduma hizo.
“Migomo iwe ni ya wafanyakazi au waajiri, iwe ni batili au halali ina athari kubwa sana kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla endapo itatekelezwa,” alisema.


Pinda alisema kutokana na ukweli huo, ndiyo maana sheria za kazi zimeweka mifumo na taratibu za kutatua migogoro ya kikazi kabla haijazaa migomo. Alisema Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Na. 6/2004 na ile ya Utumishi wa Umma Na. 8/2006 zinatambua haki ya wafanyakazi na waajiri kugoma lakini baada ya utaratibu ulioinishwa kuzingatiwa vinginevyo migomo hiyo itakuwa batili.


Alitoa mfano wa Kifugu cha 80 (1) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Na. 6/2004 kuwa mgomo halali ni ule ambao mgogoro wake ni maslahi, umejazwa kwenye fomu maalumu na kuwasilishwa katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, haujasuluhishwa katika kipindi cha siku 30 tangu ulipopokewa na Tume au katika kipindi alichoongeza msuluhishi.


Alisema mgomo unaoitishwa na madaktari hao pamoja na kuwa ni wa kimaslahi, haujawahi kuwasilishwa kwenye tume aliyoitaja kwa usuluhishi na pia haujaitishwa kwa mujibu wa sheria hiyo ya ajira.


Utekelezaji wa madai
Akizungumzia utekelezaji wa madai ya madaktari hao, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali imekuwa ikiyatekeleza akitolea mfano hatua yake ya kuahirisha safari ya kwenda Dodoma kwa saa kadhaa ili aweze kuonana nao na kusikiliza madai yao.
Alisema madai ya kurudishwa kwa madaktari walio katika mafunzo Muhimbili yametekelezwa kama ilivyokuwa katika madai ya kuongezwa posho.
Kuhusu kubadili uongozi wa juu wa wizara, Pinda alisema aliwaeleza kwamba suala hilo liko mikononi kwa Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi wao.


Akizungumzia madai mapya, Pinda alisema wakati Serikali ikishughulikia madai yao, madaktari wamekuja na sharti jipya la kutaka uongozi wa juu wa wizara uondolewe ndipo majadiliano yaendelee.


“Serikali inajiuliza kama kweli madaktari wana nia ya dhati ya kumaliza matatizo yao au wana ajenda nyingine ambayo sisi kama Serikali hatuifahamu?,” alihoji.


Alisema ameshangaa kuona kwamba baada ya kamati iliyoundwa kumaliza kazi yake na kuwasilisha mapendekezo yake kwake, alipotaka kukutana na makundi yote yaliyohusisha kamati hiyo, madaktari walijitenga na kutaka makundi mengine yasihusishwe.


“Tarehe Mosi, Februari nilipata barua kutoka kwa Chama cha Madaktari (MAT), imesainiwa na Dk Namala Mkopi wakidai kuwa wanaomba Serikali isiwahusishe makundi mengine, nilipoipata nikamwambia Katibu Mkuu hii si nzuri, nikamwambia ajaribu kuzungumza naye,” alisema.
Alisema hata siku ya pili, kamati hiyo ilipofika ofisini kwake kwa ajili ya majadiliano, madaktari hao waliamua kuondoka na kususia mkutano huo na siku inayofuata walikuja wenyewe wakiwa na sharti hilo jipya la kuwafukuza mawaziri kwanza.


Alisema hata Rais Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa ya Februari, 29 mwaka huu alisisitiza kufanyia kazi madai ya madaktari hao na kusema kwamba uamuzi wa kugoma ni kutomtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Hofu yatanda
Matangazo ya mgomo huo yaliyokuwa yamebandikwa katika kuta mbalimbali katika Hospitali ya Muhimbili yaliibua hofu kubwa miongoni mwa wagonjwa na jamaa zao.


Moja ya tangazo lilisomeka: “Kama tulivyotaarifiana kwenye kikao chetu cha Machi 3, mwaka huu ni kwamba makubaliano yaliyofikiwa na hatimaye kutiliana saini kati ya madaktari na Serikali Machi 2, mwaka huu ni kuwa ili mazungumzo ya kujadili madai yetu yaweze kuendelea na hatua ya pili ni lazima, Waziri Dk Mponda na Naibu wake, Dk Nkya ama wawe wamejiuzulu au wamewajibishwa.”
Baadhi ya ndugu wa wagonjwa waliokuwa katika maeneo ya hospitali hiyo ambao walisoma matangazo hayo walilalamikia kutomalizwa kwa mgogoro huo hali inayohatarisha maisha yao.


Akizungumza baada ya kusoma moja ya matangazo hayo, Zainabu Masoud ambaye alifika hospitalini hapo kumjulia hali mwanaye Abdallah Ali (17), alisema, “Nailaumu Serikali kwa kushindwa kuchukua hatua hadi madaktari wanagoma.”


Alihoji sababu za kuwabeba mawaziri hao wawili hata kufikia kuahatarisha maisha ya Watanzania wakati viongozi wanapougua wanasafiri kwenda nje ya nchi kutibiwa.


Msimamo wa madaktari
Akitetea ya kutangaza mgomo kwa kubandika matangazo na kuwatisha wagonjwa, Dk Mkopi alisema ni hatua nzuri ya kuwajenga kisaikolojia.
“Tumefanya hivyo kwa nia njema ya kuwajenga kisaikolojia. Ni jambo jema hata wao wakajua kinachoendela na wakachukua hatua pale inapobidi. Si kama tunafanya hivyo kwa kupenda, bali Serikali yetu inatulazimisha kudai haki za Watanzania na zetu kwa njia ngumu,” alisema.
Dk Mkopi alisisitiza kwamba hatua hiyo ni utekelezaji wa mambo matatu yaliyo kwenye mkataba baina yao na Serikali waliyokubaliana kwenye kikao cha pamoja.


“Katika kikao cha pamoja tulitiliana saini mambo yaliyogawanyika katika sehemu tatu, ambazo ni kujenga mazingira bora ya majadiliano, kuanza kwa majadiliano kutolewa kwa taarifa za Serikali kuhusu utekelezaji wa hoja zetu na kutiliana saini,”alisema Dk Mkopi.


Alisema suala la kujenga mazingira bora ya majadiliano ni kwa kuondolewa kwa Waziri wa Afya na Naibu wake kwani wanahusika na tukio la mgomo uliopita na kwamba haiwezekani utekelezaji wa makubaliano ya sasa ukawa mikononi mwao.


“Ni nani asiyejua majibu ya kejeli na dharau yaliyotolewa na wahusika hawa wakati wa mchakato wa madaktari kudai haki zao? Kama majibu ya majadiliano watasimamia wao madaktari hawatakuwa na moyo wa kufanya kazi,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Taus Mbowe, Geofrey Nyang’oro na Boniface Meena

0 comments

Post a Comment