Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Sitta ajitosa mgogoro wa Umeya Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HARAMBEE ya ujenzi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu, Tereza katika Jimbo Kuu la Arusha, jana iligeuka uwanja wa kupigana vijembe vya kisiasa na njia ya kuelekea mapatano ya mgogoro wa umeya wa jiji hilo ambao umekuwa chanzo cha machafuko kwa muda mrefu.


Mgeni rasmi katika harambee hiyo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, ndiye aliyekuwa chachu ya upatanisho huo, pale alipowakutanisha Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema na Meya wa jiji hilo, Gaudence Lyimo na kuwataka waache tofauti zao.


Sitta aliwataka Lema na chama chake cha Chadema kuacha kudai wanachokitaka kwa maandamano na vurugu kama chama kinachotaka kushika dola, badala yake aliwashauri wajenge siasa za kuvumiliana.


Dalili za siasa kutawala harambee hiyo zilijionesha mapema baada ya Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Lazaro Nyalandu kufika kanisani hapo na Sitta kusimama na kusema "taifa linahitaji viongozi vijana kama Nyalandu."


“Vijana kama hawa tunawahitaji sana, wakiungana na mbunge wenu mheshimiwa Lema, wanaweza kuleta mabadiliko ambayo ni muhimu sana katika kizazi hiki kwani Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana na Mungu,” alisema Sitta huku akishangiliwa.


Baada ya Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kukaribishwa na Sitta na kisha kuwasalimia waumini na wananchi waliofika kwenye harambee hiyo, alisema anamheshimu sana Sitta kutokana na uwezo aliounyesha wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa.


Lema alidai hana ugomvi binafsi na Lyimo bali utaratibu uliotumika hakubaliani nao na atahakikisha anasimamia hilo hadi ufumbuzi upatikane.


Awali, Waziri Sitta alisema hakuja Arusha kuongoza harambee hiyo kwa lengo la kujisafisha kama wanavyofanya wengine kwa kuwa anaamini kuwa yeye ni mwadilifu.


“Ndugu zangu sikuja kujisafisha kama wanavyofanya wengine, kwa kuwa sina sababu ya kufanya hivyo. Nyie mnajua watu waadilifu sihitaji hata kuwaambia,” alisema Waziri Sitta.


Januari 5 mwaka huu, Chadema kiliongoza maandamano ya kitaifa yaliyopoteza maisha ya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa, wakipinga Gaudence Lyimo kuwa meya huku viongozi wa Chadema wakifunguliwa kesi ya kufanya mkusanyiko bila kibali.


Vingozi wengine waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo,Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aisha Nyerere, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi na wafanyabishara mbalimbali.

0 comments

Post a Comment