Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO , HABARI ZA MICHEZO - Leo Barca vs Madrid, Simba vs Yanga. Nanimbabe?

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Na Mwandishi Wetu
BAADA ya tambo za kila aina, leo ndiyo siku ya hukumu. Mbabe kwenye Ngao ya Hisani kati ya Yanga na Simba, atajulikana.

Lolote linawezekana kwa kuwa ni mchezo wa soka lakini kila upande utalazimika kujituma ili kushinda mechi hiyo muhimu.

Achana na Yanga na Simba jijini Dar es Salaam lakini jijini Barcelona, Hispania Real Madrid watakuwa wageni wa Barca kwenye mechi ya pili ya Kombe la Super Cup baada ya ile sare ya mabao 2-2 kwenye dimba la Santiago Bernabeu.

Kwa upande wa watani wa nyumbani, Yanga wanaonekana kuwa na uhakika zaidi labda kutokana na matokeo ya mwisho ya mechi iliyowakutanisha watani baada ya kushinda bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Kagame.

Beki:
Kwa upande wa makipa, timu zote haziwezi kuwa na hofu na Juma Kaseja au Yaw Berko lakini safu za ulinzi zinapaswa kupunguza makosa madogo madogo.

Kwa Yanga: Nadir Cannavaro, Chacha Marwa inabidi wawe makini zaidi hasa kwa mipira inayopitishwa katikati na viungo wa Simba na iwapo Victor Costa atacheza kwa Msimbazi, basi lazima apunguze kujiamini wakati Kelvin Yondani au Juma Nyosso, pia watatakiwa kuongeza umakini hasa kwa ile mipira ya juu.

Kiungo:
Kurudi kwa Nurdin Bakari ni taarifa njema kwa Yanga, ana uwezo wa kukaa na kugawa mipira kwa uhakika hasa akishirikiana na Rashid Gumbo, itakuwa hatari zaidi. Jerry Santo na Patrick Mafisango pia ni wa kuchunga na Yanga wanapaswa kuwa makini na pasi ndefu za viungo hao.

Ushambuliaji:
Ni wakati mwingine mpya, hakika safu ya Yanga bado ni nzuri zaidi kwa kuwa ilishaonyesha ina Davies Mwape, Jerry Tegete na Kenneth Asamoah. Lakini Simba ina wageni watatu, Felix Sunzu, Gervais Kago na Emmanuel Okwi ambaye alikosekana mechi iliyopita, lazima kutakuwa na kitu kipya, Yanga wakae makini pia.

Inawezekana kabisa, Kocha wa Simba, Moses Basena akaamua kuwatumia wachezaji watatu mbele, atakayeongezwa atakuwa ni Haruna Moshi ‘Boban’, hivyo kuifanya timu yake iwe na washambuliaji wengi zaidi.

Kauli za makocha:
Basena: “Tuko katika hali nzuri na tuna uwezo wa kushinda, tumejiandaa vizuri na mechi hiyo itakuwa kipimo kwetu.”

Sam Timbe (Yanga): “Uhakika wa kushinda ni sisi kucheza vizuri na kuepusha makosa. Simba si timu ya kubeza, lakini tunataka kushinda.”
Ukiachana na kipute cha Dar es Salaam, kule jijini Barcelona, Makocha, Jose Mourinho na Pep Guardiola kila mmoja anajiamini kuwa watashinda.

Mourinho-Madrid: “Tunataka kushinda, ni kitu kinachowezekana. Lakini lazima tucheze kwa tahadhari kubwa.”

Guardiola-Barca: “Kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi, kuhusu (Cesc) Fabregas, vuteni subira amefanya mazoezi siku mbili. Huenda akacheza lakini tunataka kushinda.”

0 comments

Post a Comment