Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Wabunge Chadema wawaponza wa CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
BAADHI ya wabunge wamelalamikia kutopewa karatasi za mahudhurio bungeni hali inayowafanya kukosa malipo ya posho ya vikao vya Bunge.


Hali hiyo inatokana na hatua ya Bunge kubadili utaratibu wa kusaini karatasi hizo, mabadiliko ambayo yamepata upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM na wale wa vyama vya upinzani.


Habari ambazo Mwananchi lilizipata jana zinadai kwamba utaratibu huo ulilenga kuwanyima posho wabunge wa Chadema ambao waliamua kususia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ulioanza siku nne zilizopita.


Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, posho za vikao (sitting allowance) hulipwa kwa wabunge ambao huwa wamesaini karatasi za mahudhurio ambazo hupitishwa bungeni kila siku asubuhi baada ya kikao cha siku husika kuanza.


Hata hivyo katika siku nne zilizopita, karatasi hizo za mahudhurio zimekuwa zikipitishwa kwa wabunge baada ya kipindi cha maswali na majibu, tofauti na utaratibu wa awali wa karatasi hizo kupitishwa saa tatu asubuhi.


Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge walisema mpango huo ulikuwa unawalenga wabunge wa Chadema na wale wa NCCR-Mageuzi ambao kutokana na kususia mjadala wa muswada wa marekebisho ya Katiba, wamekuwa wakitoka nje baada ya kipindi cha maswali na majibu.


Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda alithibitisha kutotolewa kwa karatasi za mahudhurio wakati wa asubuhi na kwamba wamepata taarifa kwamba mpango huo ni mahususi kwa ajili ya kuwanyima wao (wabunge wa Chadema) posho za vikao.


“Hii nadhani si tabia nzuri, hapa wanatutafuta maneno tu kwamba watu tuseme na kama wanataka hilo basi tunaweza,” alisema mbunge huyo ambaye aliwahi kutofautiana na uongozi wa chama chake kuhusu msimamo dhidi ya posho za vikao bungeni.


Mwingine aliyethibitisha kuhusu ‘utaratibu huo mpya’ ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye alisema: “Ni kweli, ina maana hamfahamu? Sijui wamefanyaje hawa jamaa maana nasikia eti wamebadili utaratibu, lakini si kweli kwani haiwezekani kwamba utaratibu huu uanze siku moja tu tangu tulipotangaza kususia mjadala”.


Kafulila alisema katika utaratibu wa kawaida karatasi za mahudhurio hupitishwa bungeni mara baada ya kuanza kwa kikao, lakini tangu walipoamua kususia mjadala, karatasi hizo zimekuwa zikipitishwa baada ya wao kutoka nje, pale kipindi cha maswali na majibu kinapomalizika.


Kwa upande wake Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe (Chadema) alisema hatua hiyo haiwatishi wala haiwezi kubadili msimamo wao kwani hawategemei posho za vikao katika kuendesha maisha yao na kuwatumikia wananchi.


“Mimi nadhani ni ujinga tu wa watu wasiofikiri, sasa unapotunyima sisi karatasi za kusaini mahudhurio unakuwa na ajenda gani dhidi yetu, maana mahudhurio si kwa ajili ya posho tu, kuna mambo mengine ya muhimu, nimemwambia Katibu (wa Bunge) kwamba wanachokifanya siyo sawa,” alisema Mdee.


Alisema mbali na posho, karatasi za mahudhurio ndiyo hutumika kueleza akidi ya wabunge katika mkutano husika na kwamba hata mtu akifika na kuhudhuria kipindi cha maswali a majibu anapaswa kusaini mahudhurio hayo kwani hakuna kanuni inayozungumzia suala hilo.


Habari ambazo Mwananchi lilizipata jana jioni zinasema Spika wa Bunge, Anne Makinda ndiye aliyetoa maelekezo ya utaratibu huo ambao pia umelalamikiwa na wabunge wa CCM.


Wabunge hao ni wale ambao wamekuwa wakitoka nje baada ya kipindi cha maswali na majibu kutokana na sababu mbalimbali, hivyo kujikuta wakikosa fursa ya kusaini fomu za mahudhurio.


Mmoja wa maofisa wa Bunge aliliambia Mwananchi kuwa wamepokea malalamiko kutoka kwa wabunge zaidi ya 10 wa CCM ambao wamekwenda kudai fomu za mahudhurio ili wasaini baada ya kuzikosa ukumbini.


Ofisi ya Bunge
Hata hivyo Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah jana alikiri kuanzishwa kwa utaratibu mpya wa mahudhurio kutokana na kuwepo kwa wabunge wanaosaini kwa niaba ya wenzao ambao hawashiriki vikao vya Bunge.


“Kama ungekwenda Ofisi ya Huduma za Bunge kule kwa John Joel (Mkurugenzi) angeweza kukupa taarifa kwa undani maana wao ndio wanaosimamia jambo hili, lakini ukweli ni kwamba ni utaratibu mpya ambao nadhani tatizo lake ni kwamba haujazoeleza,” alisema Kashililah.


Katibu huyo wa Bunge alikiri kupokea malalamiko ya wabunge kuhusu kukosa karatasi za mahudhurio na kwamba wengi wamekuwa wakizifuata katika ofisi za huduma za Bunge kwa ajili ya kusaini.


Alisema lengo la utaratibu huo ni zuri tu na kwamba kutokana na malalamiko ambayo yamejitokeza watachukua hatua stahili za kuondoa kasoro zilizopo.


“Kwahiyo bwana mwandishi si kweli kwamba hapa tunawalenga wabunge wa chama fulani, hapana ni utaratibu tu lakini kama nilivyosema malalamiko mengi niliyopata ni kutoka wabunge wa CCM na siyo Chadema ama NCCR-Mageuzi, kwahiyo unaweza kuona hali halisi,” alisema Dk Kashililah.


Mgomo wa wabunge
Wabunge wa Chadema wakiongozwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kuungwa mkono na wabunge wawili wa NCCR Mageuzi ambao ni Felix Mkosamali wa Muhambwe na Kafulila, walitoka nje ya Bunge Jumatatu wiki hii wakipinga kile walichokiita kutotendewa haki na Spika Makinda.


Kadhalika wabunge hao waliendelea na msimamo wa kutojadili muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 kutokana na kile walichosema kwamba si halali kwani kuingizwa kweke bungeni kulikiuka kanuni za Bunge na sheria za nchi.


Hata hivyo muswada huo umeendelea kujadiliwa kwa siku nne na wabunge wa CCM na CUF, na hii leo huenda ukaptishwa hivyo kubaki ukisuburi saini ya Rais Jakaya Kikwete ili kuwa sheria itakayosimamia mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ya nchi.

0 comments

Post a Comment