Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Safari ya Pinda, ratiba vyazua hofu bungeni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SAFARI ya ghafla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mabadiliko ya ghafla ya ratiba ya vikao vya Bunge, jana vilizua hofu miongoni mwa wabunge, huku kukiwa na taarifa kwamba huenda muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ukaondolewa bungeni leo.


Jana alfajiri Pinda aliondoka kwa ndege kwenda jijini Dar es Salaam, ikielezwa kwamba safari yake ilikuwa ni kuitikia wito wa Rais Jakaya Kikwete. Baadhi ya wasadizi wa Pinda walioko mjini Dodoma walithibitisha Pinda kuitwa na Rais, lakini hakuna aliyekuwa akifahamu kuhusu kiini cha wito huo.


“Amekwenda Dar es Salaam na atarudi jioni leo (jana), kaitwa na bosi wake, lakini ndio hatujui ila ni safari ya kawaida,”alisema mmoja wa wasaidizi wa Pinda ambaye hakuwa tayari kutajwa gazetini.


Safari ya Pinda ilisababisha kutokuweapo kwa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu bungeni jana na badala yake kuwapo kwa kipindi cha maswali ya kawaida ambacho kilifuatiwa na mjadala wa muswada huo.


Baadhi ya wabunge wa CCM walisikika wakihoji sababu ya Pinda kuitwa ghafla na katika mazungumzo ambayo Mwananchi liliyasikia, walikuwa wakihofu kwamba huenda Rais akataka muswada huo urejeshwe kwa umma kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.


Mmoja wa wabunge hao alimhoji mwandishi wa gazeti hili akisema: “Eti nyie waandishi huwa mnafahamu mambo mengi, hivi ni kweli kwamba Pinda kaitwa na Rais ili kuondoa muswada…..! Kama ni hivyo basi itakuwa imekula kwetu”.


Hofu hiyo ilisikika kwa zaidi ya wabunge sita wa CCM ambao walizungumza na Mwananchi huku wengine wakihusisha suala hilo na hatua ya kubadilishwa kwa ratiba ya Bunge.


Mbunge mwingine alisema: “Hili jambo linawezekana ni la kweli, kwanza ratiba imebadilishwa ghafla bila kuitishwa kwa Kamati ya Uongozi, halafu PM (Waziri Mkuu) hayupo, lakini hebu tusubiri tuone kitakachotokea kwani kesho siyo mbali”.


Kikwete aendesha kikao Ikulu


Hata hivyo, taarifa ambazo Mwananchi imezipata kutoka Ikulu jijini Dar es Salaam zinasema kwamba Rais Kikwete jana alikuwa na kikao nyeti na Pinda, Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).


“Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wana kikao cha ghafla Ikulu, nahisi wanazungumzia muswada ulioko bungeni,” kilisema chanzo cha habari .


Chanzo hicho kilisema kwamba huenda Rais Kikwete akaliongelea suala hilo leo.






Mabadiliko ya ratiba
Juzi jioni mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba alipokuwa akiahirisha kikao cha Bunge, alitangaza mabadiliko ya ratiba ya vikao vya Bunge yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, mabadiliko yaliyoongeza siku moja zaidi katika mkutano huu wa tano.


Badala ya kumalizika leo, tangazo hilo lilisema kuwa mkutano huo utamalizika kesho Jumamosi, huku mjadala wa Muswada wa Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 ukiongezewa muda zaidi.


Katika ratiba ya awali, muswada wa marekebisho ya katiba ulipaswa kuhimitishwa juzi jioni, lakini katika ratiba iliyotangazwa na Mabumba unatarajiwa kuhitimishwa leo katika kikao cha asubuhi, baada ya wabunge kumaliza kuchangia jana mchana.


Ripoti ya Jairo kusomwa leo


Mabadiliko hayo yanaonyesha kuwa, ripoti ya Jairo ya Kamati Teule ya Bunge itasomwa leo baada ya kuhitimishwa kwa muswada huo, na kesho Bunge litapokea ripoti ya kamati ya Nishati na Madini kuhusu sekta ya gesi kisha Bunge kuahirishwa.


Jana hakukuwa na kikao cha jioni baada ya Bunge kukutana asubuhi, hali ambayo iliwafanya wengine kuhoji sababu za muswada huo kuwekwa kiporo hali kulikuwa na muda wa kuhitimisha jana.


“Kama wachangiaji hawapo kwanini wanaendelea kutuweka hapa sasa, maana leo (jana) jioni hakuna Bunge, wachangiaji wameisha tunasubiri nini?,” alisikika mmoja wa wabunge wa Viti Maalum (CCM), akiwauliza wenzake katika viwanja vya Bunge jana.


Lukuvi na Kashililah
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema: “Lazima mfahamu jambo moja, sisi Serikali hatuna mamlaka na ratiba ya vikao hivi, kazi hiyo ni ya ofisi ya Bunge. Lakini tumefurahi kwamba leo (jana) jioni hakuna Bunge kwasababu tunapata fursa ya kujibu hoja na kuzingatia majedwali ya mabadiliko yaliyoletwa na wabunge”.


Lukuvi alisema hadi jana jioni hakukuwa na mabadiliko yoyote kwenye ratiba iliyotolewa na Bunge juzi na kwamba Serikali ilikuwa ikijadiliana na wabunge waliowasilishwa majedwali ya mabadiliko katika muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuona jinsi ya kuyazingatia katika sheria hiyo.


“Sisi tunadhani kwamba ofisi ya Spika imefanya vizuri, maana kama tusingepata muda wa leo ingekuwa ni vigumu sana kujibu hoja zote za watu zaidi ya 70 katika muda wa saa 2 au tatu za mapumziko ya mchana, lakini sasa tuna imani kwamba kila kitu kitakwenda sawa maana tutapata muda wa kujadiliana na wabunge na mambo yote kesho (leo) yatakwenda sawa,”alisema Lukuvi.


Kwa upande wake, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mabadiliko ya ratiba ya Bunge yalizingatia wingi wa majedwali ya marekebisho ya muswada huo yaliyowasilishwa na wabunge.


Awali kulikuwa na taarifa kwamba majedwali hayo (schedules of amendments) yalikuwa yamefikia 29, lakini Dk Kashilila aliliambia Mwananchi kwamba majedwali hayo yalikuwa yakikaribia 40.


“Lazima tufanye kazi hii nje ya Bunge, tunataka Serikali ikutane na hawa wabunge ili kufanya majadiliano ya awali kupunguza kazi hii maana ni vigumu sana kushughulikia majedwali haya bungeni, inaweza kutuchukua siku nzima,”alisema Katibu huyo wa Bunge.




Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ilitarajiwa kukutana jana saa saba mchana, lakini kikao hicho kiliahirishwa hadi saa 10 jioni kutokana na Serikali kuwa na mzigo mkubwa wa hoja za wajumbe.


Kuwepo kwa idadi kubwa ya majedwali yanayopendekeza marekebisho ya muswada huo, ni dalili kwamba hata wabunge wengi wa CCM wamebaini kasoro nyingi licha ya kwamba wote waliochangia waliuunga mkono.

0 comments

Post a Comment