Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Hofu kubwa vikao vya CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HOFU kubwa imetawala miongoni mwa makada wa CCM kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba huenda wanachama sita maarufu ndani ya chama hicho kikomgwe nchini wakatimuliwa katika vikao vya juu ambavyo vitafanyika kaunzia mwishoni mwa wiki hii na kumalizika mapema wiki ijayo.


Vikao hivyo ni vile vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kitakachotanguliwa na Kamati Kuu ya CCM (CC) ambavyo vitaongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.


Juzi kulikuwa na kikao cha maandalizi wa maofisa wa makao makuu wa CCM na jana Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama ilikutana kuandaa vikao hivyo ambavyo uamuzi wake unasubiriwa kwa shauku kubwa.


Wakati maandalizi hayo yakiendelea habari kutoka ndani ya chama hicho zinadai kwamba hofu kubwa iliyotawala ni kuwepo kwa taarifa kwamba huenda makada sita ambao ni wanachama wakongwe wa CCM (majina tunayahifadhi kwa sasa) wakasimamishwa uongozi na wengine kutimuliwa uanachama kutokana na tuhuma kwamba wanakivuruga chama hicho.


Habari za uhakika ambazo Mwananchi limezipata zinadai kwamba tayari watuhumiwa hao wa vurugu ndani ya CCM wameitwa mbele ya Kamati ya Maadili ambayo itafanya kikao chake leo au kesho chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.
Miongoni mwa tuhuma zinazowakabili makada hao ni kutoa kauli zinazokinzana hadharani, kupinga uamuzi halali wa vikao vya juu vya chama na kuendesha siasa za makundi ambazo zimekigawa chama hicho tawala.


Mmoja wa wanaotajwa kuitwa mbele ya kamati ya maadili, alilithibitishia Mwananchi kupokea wito huo na kwamba atakwenda mjini Dodoma kusikia kile alichoitiwa.


“Unachokisema ni kweli, nimeitwa kwenda mbele ya kamati ya maadili ijapokuwa sifahamu sababu ya wito huo, nitakwenda kusikiliza halafu nifahamu kile nilichoitiwa huko huko,”alisema kada huyo ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa moja ya mabaraza ya jumuiya za CCM.


Jumuiya za CCM ni tatu ambazo ni Umoja wa Wanawake (UWT), Jumuiya ya Wazazi na Jumuiyaya Umoja wa Vijana (UVCCM).


Maazimio ya NEC
Kikao cha NEC kinakutana miezi minne tangu kilipokutana mara ya mwisho na kutoa maazimio ambayo yalisababisha mmoja wa makada wake, Rostam Aziz kujiuzulu ubunge katika jimbo la Igunga pamoja na ujumbe wa NEC.


Rostam katika kujiuzulu huko aliitupia lawama sekretarieti ya chama hicho kwa kile alichokiita kuwa ni kuendesha siasa chafu dhidi yake na kuwataja kwa majina Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara, John Chiligati na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kuwa wahusika.


Kujiuzulu kwa Rostam ambako kulifanya Bunge kutangaza nafasi wazi katika jimbo la Igunga mkoani Tabora, ni miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mjadala wa CC na NEC.


Katika mazingira hayo, kuna kika uwezekano wa kutathini jinsi falsafa ya kujivua gamba ilivyotekelezwa na kama ni Rostam peke yake ambaye alipaswa kuchukua uamuzi wa kujindoa kwenye nafasi za uongozi wa juu wa CCM.


Habari zaidi zinadokeza kuwa Sekretarieti ya Mukama nayo imegawanyika katika suala la utekelezaji wa uamuzi wa NEC, hali inayoongeza sintofahamu ndani ya chama hicho.


Kutokana na mambo yalivyo, busara ya Mwenyekiti, Rais KIkwete inatarajiwa sana kuchukua nafasi ili kuepusha uwezekano wa mgawanyiko kuwa mkubwa zaidi baada ya vikao hivyo.


Hali ilivyo Dodoma
Mmoja wa makda wa CCM aliliambia Mwananchi juzi mjini Dodoma kuwa kuna uwezekano wa hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya makada ambao wanatoka katika makundi ambayo yamekuwa yakipigana vita ndani ya chama.


Alisema: “Kutokana na hali hiyo, kila kundi linafanya jitihada za kutafuta wafuasi wa kuliunga mkono ili watu wake wasifikwe na adhabu inayokusudiwa kutolewa”.


“Kuna taarifa kwamba Mwenyekiti (Rais Kikwete) amechoshwa na siasa hizi za kuviziana, sasa tunasikia kwamba ameamua kuchukua hatua na kuna uwezekano wa baadhi ya makada wenzetu wakafukuzwa kabisa uanachama”.


Katika kuthibitisha hali ilivyo tete, wabunge wanne wa CCM, wakiwamo mawaziri wawili kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili kwamba hawatakubali mtu wao ang’olewe.


“Mimi (anamtaja jina) akifukuzwa uanachama, basi hata mimi najiuzulu ubunge, huyu bwana ni mtu muhimu sana na ni brain ya chama, lakini hawa jamaa eti wanataka kumfukuza nadhani hilo halikubaliki,”alisema mmoja wa wabunge kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Mbunge mwingine alisema vita ndani ya CCM ni harakati za Urais wa mwaka 2015. “Ujue (anamtaja jina) anaogopwa sana kwamba anaweza kuwa Rais 2015, kila mmoja anamwona tishio hivyo anaandamwa kutoka kila kona, lakini ukiona hivyo ujue kwamba anafaa, kama mnaweza na ninyi tusaidieni basi”.


Tangu kuanza kwa kikao cha Bunge wiki iliyopita, baadhi ya makada wamekuwa wakiwashawishi baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa NEC kuwa na msimamo wa kuwaokoa wale wanaolengwa kufukuzwa ndani ya CCM.


Miongoni mwa mbinu ambazo zimepangwa ni kupendekezwa kwa Mwenyekiti kwamba mtu asichukuliwe hatua bila kupewa nafasi ya kujieleza mbele ya kikao hicho na kwamba hatua hiyo inalenga kutoa mwanya wa mapendekezo ya kuwanusuru baadhi yao.


“Hakuna mtu atakayechukuliwa hatua bila kusikilizwa, hilo tutalisimamia maana hiyo ndiyo natural justice kwa kila mtuhumiwa, na tukifanya hivyo tutafanikiwa tu,”alisema Mbunge mwingine kutoka Kanda ya Kaskazini.


Hali ndani ya CCM
Kikao hicho pia kinafanyika wakati ambao kumekuwa na misigano miongoni mwa makada wa chama hicho tawala nchini hasa kuhusu jinsi Sekretarieti ya Katibu Mkuu Mukama inavyotekeleza maazimio ya kikao cha mwisho cha NEC kilichoridhia mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho.


Hatua ya Nape na Chiligati kutajwa na Rostam katika hotuba yake ya kujiuzulu aliyoitoa jimboni Igunga kwamba ni miongoni mwa viongozi waliopotosha nia njema ya kukivusha CCM katika matatizo yanayokikabili ni ishara kwamba kazi itakuwa kubwa wakati wa kikao cha NEC.


Kujiuzulu kwa Rostam kulitafsiriwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya NEC hasa baada ya yeye (Rostam), Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kutajwa kwa majina kuwa ni miongoni mwa wanaotakiwa kujivua gamba kufuatia kutajwa katika tuhuma mbalimbali za ufisadi.


Tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, hiki ni kikao cha kwanza cha juu cha CCM kukutana na taarifa hiyo ya Msekwa ambayo inachagizwa na kujiuzulu kwa Rostam huenda ikawasilishwa na kujadiliwa na NEC.


Pia Msekwa siku chache zilizopita alikutana na wenyeviti wa CCM wa mikoa, huku Mukama akikutana na makatibu wa mikoa katika vikao visivyo vya kikatiba vilivyofanyika jijini Dar es Salaam kutafakari hali ilivyo ndani ya chama.


Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zilidai kwamba utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba ulipingwa vikali kwamba unakigawa chama hicho.


Katika kile kinachothibitisha kuwepo kwa misigano miongoni mwa makada wa CCM, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu wiki hii aliliambia Mwananchi mjini Dodoma kuwa "Wanachama wengi wa CCM hawafurahishwi na ziara za Nape na washirika wake mikoani," kwamba zinaweza kukigawa chama badala ya kukiimarisha.


"Kwa mfano unapowataja watu watatu tu kwamba ndio wanaopaswa kujivua gamba una maanisha nini, Mimi nadhani si haki kabisa, hawa jamaa wanataka kutupeleka mahali ambako siko,"alisema mjumbe huyo wa CC.


Siku chache zilizopita, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kupitia kwa Kaimu Mwenyekiti wake, Benno Malisa uliingia katika mvutano na Nape, baada ya kutoleana kashfa hadharani.

0 comments

Post a Comment