Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - SAKATA LA KATIBA Dk Salim: CCM kaeni na Chadema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
ANONYA BILA MARIDHIANO NCHI ITAELEKEA KUBAYA, KITINE ADAI SERIKALI 'INATUPELEKAPEKA'
Boniface Meena
MJADALA wa Muswada wa Katiba Mpya umechukua sura mpya baada ya viongozi waandamizi wa Serikali wakiwamo wastaafu, kutaka upatikane mwafaka wa kitaifa kuhusu suala hilo vinginevyo taifa litaelekea kubaya.Onyo la viongozi hao akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa , Dk Hassy Kitine, linakuja ikiwa ni siku chache baada ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe kutaka mwafaka huo wa kitaifa.


Jana, viongozi wakichangia maoni yao katika mdahalo uliondaliwa na Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), kuhusu nafasi na umuhimu wa katiba katika maisha ya Watanzania, kwa sehemu kubwa walipaza sauti kutaka mwafaka huo ili kunusuru taifa.


Kauli ya Dk Salim
Dk Salim ambaye ni mwenyekiti wa MNH, alisema ni muhimu kuwe na makubaliano na maafikiano katika suala la Katiba Mpya kwa CCM na Chadema.


Alisema, “Chama tawala na chama kikuu cha upinzani vijue tunaangalia mustakhabali wa taifa letu, lazima uelewano uwepo”.
Dk Salim alisema kwamba malumbano si mazuri japokuwa ni sehemu ya siasa, lakini akaonya kwamba yasiruhusiwe yakasababisha nchi ikafika pabaya.


“Ninachoomba chama tawala na Chadema wafikirie mwafaka na kuangalia mustakhabali wa taifa, kama hakuna maafikiano si jambo zuri kwa taifa,”alisema Dk Salim ambaye ana uzoefu na utatuzi wa migogoro ya kimataifa.
Alisema zoezi la Katiba ni zito na linatakiwa kufanyika kwa busara na kuwahusisha Watanzania wote.


“Kwa hali ya kisiasa hivi sasa ni lazima mjadala uwe wa nia njema lengo ni kuendeleza makubaliano na si kuhitilafiana. Tujenge na kuimarisha undugu na mishikamano wetu na kuonyesha uzalendo na uongozi madhubuti wa taifa letu,”alisema Dk Salim.


Kitine aionya Serikali
Kwa upande wake, Dk Kitine, alisema ni vizuri Serikali ikasoma alama za nyakati kutokana na hoja iliyoko bungeni kwa kuangalia suala hilo la katiba.


Dk Kitine alisema Serikali haitakiwi kuruhusu Muswada huo wa Marekebisho ya Katiba ukasomwa kwa mara ya pili, kwani tayari upinzani bungeni umekwishapinga.


“Serikali iutoe na kusoma upya, nchi haiko tayari kuona Serikali inavyotupeleka. Sasa ndiyo maana kuna matatizo kila sehemu,”alisema Dk Kitine.


Jaji Samatta
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta alisema kuna baadhi ya wanasiasa hawaelewi maana ya katiba na kupotosha kuwa ni mapatano kati ya wananchi na viongozi.“Katiba ikifutwa viongozi hakuna, hivyo Katiba ni moyo wa taifa,”alisema.


Jaji Samatta alisema kutunga Katiba ni kazi nzito na haiwezekani kila kitu anachokihitaji au kitu kinachohitajiwa na kundi fulani, kiwepo katika Katiba.“Katiba ni makubaliano, lakini muda uliowekewa suala hili ni mchache,”alisema.


Alisema Katiba ya mwaka 1977 imefanya kazi nzuri, lakini ina matatizo mengi ndani yake, moja ikiwa ni dhana ya mfumo wa chama kimoja.


“Mfano Spika wa Bunge kuwa sehemu ya Halmashauri Kuu ya chama tawala, hapa atasababisha mgongano wa maslahi kwa kutetea chama chake,”alitoa kasoro hiyo.


Alisema kutokana na hali hiyo, Katiba Mpya ni lazima iwe na chachu ya upanuzi wa demokrasia na uboreshaji wa utawala wa sheria.“Iwe ya mfumo wa vyama vingi na kuondokana na mfumo wa chama kimoja na iwe, inayoongozwa na wananchi,”alisema Jaji Samatta.


Dk Slaa atabiri Katiba mbovu
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema mchakato wa Katiba uikiwa mbovu Katiba yenyewe itakuwa mbovu.


“Wenzetu kule Dodoma wanapotosha kwamba kilichopo ni mchakato wanafikiri mchakato ni kitu kidogo, katiba ndiyo mzazi wa kila kitu hivyo kwa hali ilivyo katiba hii haiwezi kuwa ni ya wananchi badala yake Rais anajitengenezea Katiba yake,”alisema Dk Slaa.


Dk Bilal
Awali, akifungua mdahalo huo baada ya wachangiaji hao kutoa maoni yao, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal alisema nchi haiwezi kuwa na katiba nzuri ambayo itapatikana kwa kuliacha taifa likiwa vipande.


Alisema, ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo majadiliano kuhusu kupata Katiba kukiwa na dhamira ya pekee ya kuhakikisha umoja, mshikamano na muunganmo vinabakia na kuimarika zaidi.


Dk Bilal alisema Serikali imejipanga vizuri na itahakikisha zoezi hilo linafanyika vema bila bughudha yoyote na kila mwananchi anapata haki ya kutoa maoni yake, kwa uwazi bila vizingiti vyovyote.


“Tunataka kubakia taifa ambalo linasimamia uhuru, haki na misingi ya kutafuta usawa kwa kila mwananchi. Tunataka kubakia taifa linaloheshimu utu, kuenzi ubinadamu na kuthamini ujenzi wa taifa lisilofungamana na matabaka,”alisema Dk Bilal.


Makamu wa Rais alisema kazi ya kuandika Katiba mpya ni lazima ifanyike kwa umakini, kwa uangalifu na kwa weledi mkubwa kwa kuwa taifa linapaswa kubaki linalokuwa kisiasa, kijamii na kiuchumi.


Tangu kuanza kwa mjadala kuhusu muswada huo, wabunge wote wa Chadema akiungwa mkono na baadhi ya wabunge wa NCCR- Mageuizi hawakuwahi kushiriki kutokana na kile wanachodai kwamba kuingizwa kwake bungeni kulikiuka kanuni za Bunge na Sheria za nchi.

0 comments

Post a Comment