Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Jukwaa la Katiba, Asasi zisizo za Kiserikali na wanaharakati waandaa maandamano nchi nzima

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, akizungumza na waandishi
*Yatahusisha asasi 180,TUCTA, wenye VVU
*Ni kumshinikiza asisaini muswada wa katiba
*Kikwete afurahia kukutana na CHADEMA
WANAHARAKATI wa asasi za kiraia zaidi ya 180, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Jukwaa la
Katiba Tanzania, wameandaa maandamano makubwa yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi, wiki hii ili kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asitie saini muswada wa mchakato wa katiba mpya.


Tamko la kuitishwa kwa maandamano hayo lilitolewa Dar es Salaam jana na wanaharakati hao kwa hoja kuwa muswada wa katiba mpya uliopitishwa bungeni wiki iliyopita hauna nia njema kwa wananchi wa Tanzania.


Miongoni mwa waliothibitisha kushiriki maandamano hayo ni vyama vyote vya watu walemavu, wanaoishi na UKIMWI na taasisi za kiimani.


Akitoa tamko hilo Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Bw. Deus Kibamba alisema asasi za kiraia zaidi ya 180 zimethibitisha kushiriki maandamano hayo na zinaendelea na ushawishi wa kuwataka wananchi washiriki.


Bw. Kibamba alisema iwapo mchakato muswada uliopitishwa utasainiwa na Rais Kikwete kama ilivyokusudiwa, basi kuna hatari kubwa ya rasimu ya katiba itakayopatikana kukataliwa na wananchi wakati wa kura ya maoni, kwa kuwa wanaharakati watakuwa wameeneza sumu kwa wananchi.


"Matokeo yake ni kupoteza fedha nyingi za umma na kuendelea kulitia hasara taifa, huku wananchi wakitaabika kwa umaskini," alisema.


Alisema kuwa kutokana na hali hiyo jukwaa limeona ni vema kulinusuru taifa na kuwawezesha wananchi kuamua wenyewe kuhusu hatma ya maisha yao, kwa kuandaa maandamano nchi nzima yatakayoshirikisha wananchi ili kutoa kilio chao.


Alisema maandamano hayo yatafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na yanaratibiwa na jukwaa hilo.


Kwa Mkoa wa Dar es Salaam yataanzia viwanja vya Mnazi Mmoja saa mbili na kuelekea katika viwanja vya Jangwani.


Bw. Kibamba alisema hakuna sababu yoyote ya maandamano hayo kuhitaji kibali cha polisi na hawatarajii kwenda kukiomba kwa sababu muswada wa mabadiliko ya katiba uliopitishwa umebeba adhabu ya jinai na vitisho kwa wananchi.


"Suala la kibali ni dhana potofu wala, hatuna nia ya kukiomba... hatuna muda wa kwenda kuonana na makamanda wa kila mkoa, jukumu hilo ni la IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) na sisi tumempa taarifa na yeye," alisema Bw. Kibanda.


Alisema polisi wanatakiwa watumie intelejensia yao kubaini kama kutakuwa na upungufu wa amani katika maandamano hayo.


Alisema kilichofanyika bungeni ni kinyume ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayotoa uhuru wa wananchi kutoa maoni yao.


"Tunatoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya amani ya kumtaka Rais Kikwete asitie saini muswada huo, kwani wananchi wengi watakuwa wamekosa fursa ya kushiriki mchakato wa katiba kuanzia hatua ya msingi, vinginevyo wengi tutajikuta tuko jela na hivyo kujenga chuki baina ya serikali na wananchi na matokeo yake ni uvujifu wa amani," alisema na kuongeza;


"Tuhamasishane wanawake na wanaume, vijana na wazee, wakulima na wafugaji, wafanyakazi na viongozi wa taasisi zote za kiimani, polisi hasa brass band tunaomba watuongoze kwenda viwanjani, lengo letu kuu ni kujenga msingi mzuri kwa ajili mwafaka wa kitaifa kupitia ushiriki wa Watanzania wote."


Bw. Kibamba alisema kama kweli Rais ni msikivu na mpenda wananchi wake na amani ya nchi kwa ujumla, basi hatasaini muswada huo.


Alisema Rais akifanya hivyo atakuwa ametumia uamuzi wa busara kuliko wakati mwingine wowote wa uongozi wake.


Bw. Kibamba alisema kitendo cha muswada huo kusomwa mara ya pili kabla ya kufikishwa kwa wananchi wa maeneo yote ya nchi ni kujenga msingi mbovu wa katiba ya nchi.


Alisema wabunge walioshiriki muswada huo wajiulize kama nyumba inayojengwa ina msingi imara na kama itadumu.


Msimamo wa TAMWA


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya, alisema anasikitika kuona wabunge wanawake bungeni, wanageuka vipashio, wakizungumza kwa jazba, kubezana wao na vyama vyao na ndio maana wamepitisha muswada uliobeba adhabu ya jinai na vitisho.


Bi. Nkya alisema wanalaani mapema matamshi yaliyokuwa yakitolewa na wabunge na viongozi wengine wa serikali, ambayo asilimia kubwa yalikuwa yanapotosha ukweli.


"Tunalaani matamshi na matamko yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa serikali na wabunge dhidi yetu na kauli hizo zimetolewa kiitikadi zaidi kwa kuwa hazielezi ukweli wa jambo," alisema na kuongeza;


"Niwajulishe wabunge kwamba walichokifanya ni kama kujenga nyumba ya msingi wa uyoga au keki, pia wafahamu hawajatendea haki wananchi wao na ndio maana wengine wanaona aibu kwenda kuwaeleza hilo."


Bi. Nkya alisema wabunge walishindwa kujadili muswada badala yake walijadili majukwaa, majina ya watu na vyama vya siasa, huku wengine wakionekana kama vipashio vya mijadala na kujisahau.


Msimamo wa TUCTA


Naye Naibu Katibu Mkuu TUCTA, Bw. Herzon Kaonya, alisema ikiwa Rais atasaini mkataba huo itakuwa ni kielelezo sahihi cha kuwapuuza wananchi wake.


Aliongeza kuwa kwamba watachukua hatua mbadala ya kukusanya maoni kwa wananchi ikiwa muswada huo utasainiwa.


Bw. Kaonya alisema kuna uwezekano mkubwa wa mfumo uliotumika kupitishwa muswada huo ndio utakaotumika kutafuta maoni kwa wananchi.


Alisema kawaida ya watawala barani Afrika hupenda kujiwekea vitu ambavyo hulinda maslahi yao na kuwaandaa watoto wao kuendelea kushika nyadhifa huku wakiwapuuza wananchi.


"Nasema serikali itambue kwamba iliwekwa madarakani na wananchi na itaondolewa na wananchi hao hao," alisema.


Msimamo wa TGNP


Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Issu Malya, alisema serikali imevurunda, hivyo haikuwatendea haki wananchi.


"Watu wanafanya maamuzi kwa itikadi za vyama, bila kujua kuwa vyama vitakufa na wananchi watabaki, nyumba zitabomoka, lakini watu wataendelea kuwepo, kwa kweli naweza kusema kuna upepo mchafu umeingia nchini na ndiyo unawasumbua viongozi na kushindwa kujua wanachokifanya," alisema.


Wanaharakati hao wametoa msimamo huo huku Rais Kikwete, akiwa ameishatangaza kusaini muswada huo mapema akishirikiana na Rais wa Zanzibar.


Tamko hilo la wanaharakati limetolewa ikiwa ni siku siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza majina ya watu sita watakaokwenda Ikulu kuzungumza na Rais Kikwete, kuhusu sakata hilo la katiba.

0 comments

Post a Comment