Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bunge laanza uchunguzi tuhuma za ufisadi maliasili

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
BUNGE kupitia Kamati ya Maliasili na Mazingira limeanza uchunguzi wa kuwapo kwa vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kufanywa katika Wizara ya Maliasili na Utalii, vikihusisha utoroshaji wa wanayamapori kwenda nje ya nchi.


Habari zilizopatikana mjini Dodoma na kuthibitishwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah zinasema Kamati ya Maliasili na Mazingira imeteua kamati ndogo yenye wajumbe watano ambayo imepewa muda wa wiki tatu kukamilisha kazi yake.


“Kweli kamati hii imeundwa na kimsingi imeshaanza kazi yake, lakini nilitarajia kwamba leo (jana), baada ya kuwa nimekutana nayo ningetoa taarifa rasmi ili umma uweze kufahamu jambo hili,” alisema Dk Kashililah.


Kuundwa kwa kamati ndogo kumetokana na ombi lililowasilishwa kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli akitaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina kutokana na kuwepo kwa taarifa za kuendelea kwa vitendo vya utoroshaji wa wanyama kwenda nje ya nchi.


Habari zinasema, baada ya kuthibitika kutoroshwa kwa wanyama kadhaa Novemba mwaka jana kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), vitendo hivyo vimeripotiwa kuendelea na zaidi ya twiga hai watano wameshatoroshwa.


Kamati hiyo ndogo pia itachunguza malalamiko ya kutozingatiwa kwa ushauri wa kitaalamu katika kazi ya ugawaji wa vitalu vya uwindaji.


Lembeli alipoulizwa kuhusu kuundwa kwa kamati hiyo hakuthibitisha wala kukanusha.


Kamati ya Lembeli iliwahi kuwasilisha maombi ya kuunda kamati ndogo wakati wa kuahirisha Bunge la Bajeti Agosti, mwaka huu lakini spika alikataa maombi hayo.


Lakini sasa imethibitika kwamba Spika amekubali maombi ya awamu ya pili yaliyowasilishwa mezani kwake na Kamati hiyo hivyo kuruhusu kamati yake ndogo inayoongozwa na Mbunge wa Mafia (CCM), Abdulkarim Shah kuanza kazi yake tangu Jumatatu wiki hii.


Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Bernadeta Mushashu, Mbunge wa Pangani (CCM), Salehe Pamba na Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Khamis Seif.


Hadidu za rejea za kamati hiyo ni kuchunguza uhalali wa twiga wawili kukamatwa wakiwa hai kisha kusafirishwa kwenda nje ya nchi, kuchunguza ushiriki wa watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika biashara haramu ya nyara za Serikali na kuchunguza uadilifu wa watumishi wa wizara hiyo wanaofanya kazi katika sekta ndogo ya wanyamapori.


Nyingine ni kuchunguza utaratibu uliotumika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji na kwamba uchunguzi katika eneo hilo unatokana na malalamiko yaliyotolewa na wawindaji wazalendo kwamba kulikuwa na ushawishi uliosababisha upendeleo.


Shah alikiri kuundwa kwa kamati yake lakini hakuwa tayari kuzungumza lolote akisema taratibu za awali zilikuwa hazijakamilika.


Msingi wa kanuni
Kamati Ndogo ya Bunge huundwa kwa mujibu wa Kanuni ya 114 (18) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007 na kwa mujibu wa taratibu za kuundwa kwake, wajumbe huteuliwa na mwenyekiti wa kamati ya kudumu husika, kisha kuridhiwa na Spika.


“Kamati yoyote inaweza kuunda kamati ndogo kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli zake kadri itakavyoona inafaa na kila kamati ndogo itapangiwa kazi zake na kamati ya kudumu inayohusika,” inaeleza kanuni hiyo ya 114 (18).


Matumizi ya kanuni hiyo yameonyesha ufanisi mkubwa pale Kamati ndogo ya Kamati ya Nishati na Madini, ilipotoa taarifa yake Bungeni na kuweka wazi ufisadi katika sekta ya gesi ulioikosesha Serikali kiasi cha Dola za Marekani 110 milioni.


Pia kanuni ya 116 ya Kanuni hizo inasema mbali na majukumu yake yaliyoainishwa katika kanuni hizo, kamati yoyote inaweza kupendekeza kwa Spika ipewe majukumu ya nyongeza ambayo yatatajwa katika mapendekezo husika.


Matumizi ya Kamati ndogo yanaonekana kurahisisha uchunguzi katika sekta za Serikali zenye utendaji tata, badala ya Bunge kusubiri kamati teule ambazo kuundwa kwake kuna urasimu mkubwa kutokana na kuhitaji ridhaa ya Bunge zima.
Madudu Maliasili


Kama ilivyo Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikilalamikiwa kutokana na watendaji wake kuhusishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo vimekuwa vikilikosesha taifa kiasi kikubwa cha fedha.


Wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu, wabunge walichachama kutokana na kuwepo kwa tuhuma za utoroshaji wa wanyama hai na ndege kwenda nje ya nchi, kiasi cha kumfanya Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Wanyamapori, Obeid Mbangwa.


Wakati akihitimisha hotuba ya Bajeti ya Wizara yake, Maige alitangaza kuunda tume tatu za kuchunguza masuala tata yaliyozungumzwa na wabunge wakati wa kuchangia hotuba yake lakini hadi sasa matokeo hayajawahi kutolewa hadharani.


Waziri Maige mbali na kumsimamisha Mbangwa pia aliwasimamisha kazi maofisa wengine wawili wa wizara hiyo huku akiahidi kuunda tume za kuchunguza suala unyanyasaji wa wananchi katika Wilaya ya Urambo pia utoroshaji wa wanyama hao kupitia KIA, Novemba 24, 2010.


Kauli hiyo ya Maige ilitanguliwa na uamuzi wa Serikali ambao ulitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wa kusitisha leseni zote za ukamataji wa wanyama hai na kuwasafirisha kwenda nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka mmoja pamoja na kuahidi kwamba wanyama waliotoroshwa watafuatiliwa na kurejeshwa nchini.

0 comments

Post a Comment