IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MAHAKAMA ya hakimu mkazi Arusha, jana ilikataa kutoa hati ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu lililowasilishwa na upande wa mashtaka baada ya washtakiwa hao kutofika mahakamani.
Hakimu Mkazi, Devotha Msofe alikataa ombi la wakili wa serikali, Haruna Matagane kwa sababu yeye alipaswa kutekeleza jukumu la kuahirisha shauri hilo la jinai namba 454 ya mwaka huu inayowakabili viongozi wa juu, wanachama na mashabiki wa Chadema wanaodaiwa kufanya mikusanyiko isiyo halali kati Saa 12 jioni ya Novemba 7 hadi 8, mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza, ilisikilizwa na hakimu Devotha Kamuzora ambaye jana alikuwa na dharura, hivyo mwenzake Msofe kusaidia kutaja na kuiahirisha hadi Desemba 20 mwaka huu itakapotajwa tena ili kupangiwa tarehe ya kusikilizwa baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi umekamilika.
“Mimi leo nina jukumu moja tu la kuahirisha shauri hili, nadhani ni vema maamuzi ya kutoa hati hiyo kama upande wa mashtaka unavyoomba yakatolewa na hakimu anayesikiliza kesi hii,” alisema Hakimu Msofe.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Method Kimomogoro alieleza mahakama kuwa wateja wake walishindwa kufika mahakamani jana kutoka na tatizo lililokuwa nje uwezo wao baada ya ndege waliyopanga kusafiria jana asubuhi kubadilisha ratiba ya safari yake.
Wakili huyo aliomba kuwa iwapo ni lazima wawepo mahakamani, basi shauri hilo liahirishwe kwa muda hadi mchana ambapo ndege hiyo ingekuwa imefika kabla ya muda wa mahakama kumalizika saa 9:30 alasiri.
Kimomogoro alidai washtakiwa hao walishindwa kufika Arusha mapema kabla ya jana kwa sababu walikuwa wakihudhuria vikao vya kamati kuu (CC) ya Chadema ambavyo Mbowe ndiye mwenyekiti wake huku Lissu akiwa mjumbe, vikao alivyodai vilimalizika usiku wa kuamkia jana.
Licha ya wakili serikali kupinga hoja hizo za utetezi akidai washtakiwa walipaswa kupanga na kufanya vikao vya mapema kabla ya siku zinazokaribiana na tarehe ya kesi, hakimu Msofe alisema zina msingi na kuhairisha shauri hilo.
Washtakiwa wengine 26 akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa walikuwepo mahakamani ambapo wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu tofauti ikiwemo kufanya kusanyiko kinyume cha sheria , kukataa kutii amri halali ya polisi iliyotolewa na kamanda wa oparesheni maalumu mkoa wa Arusha, Peter Mvulla akiwaamuru kutawanyika.
Shtaka la tatu linamkabili Dk Slaa peke yake, anayedaiwa kutoa maneno ya uchochezi Novemba 7 mwaka huu, saa 11.30 jioni kwenye viwanja vya NMC akimtaka IGP Said Mwema kumuhamisha Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) wa Arusha, Zuberi Mwomboje na kuwa watamng’oa Rais madarakani kwa maandamano.
Katika hali iliyozua hofu na wasiwasi kwa wananchi waliohudhuriwa kesi hiyo, idadi kubwa ya askari polisi ilizingira maeneo yanayozunguka mahakama hiyo, huku magari zaidi ya manane ya jeshi hilo, mengi yakiwa na namba za usajili za kiraia yakiwa yameegeshwa kila kona ya viwanja vya mahakama.
Pamoja na idadi kubwa ya polisi, watunisha misulu maarufu kama mabaunsa ambao hawakujulikana mara moja wameletwa na nani walikuwa wakirandaranda kila kona na mara baada ya shauri hilo kuahirishwa walienda kubana pembeni mwa geti la kuingia na kutoka mahakamani bila kujulikana wanavizia kitu gani.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Hakimu akataa ombi la kuwakamata Mbowe, Lissu
0 comments