IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WIKI iliyopita tuliandika habari za Watanzania 23 kati ya 25 waliouawa nchini Somalia ambao walijiunga na wapiganaji wa Kikundi cha Kigaidi cha Al-Shabaab na serikali ya nchi hiyo, askari wa Kenya na wale wa Umoja wa Mataifa (UN).
Tuliona mbinu zinazotumiwa na Watanzania kujiunga na kikundi hicho bila serikali kujua. Mwandishi wa makala haya anaendelea kukuletea mfululizo wa matukio ya Al –Shabaab kama alivyozungumza na mmoja wa askari Mtanzania, Aizak Ibnu Ilah katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Ilah anaeleza: “Tumekuwa tukichukuliwa hapa Tanzania na baadhi ya viongozi wa dini kutoka Pakistan ambao wapo hapa nchini kwa ujanja wa kuwarubuni wazazi wetu kwamba tunaenda kusomeshwa mambo ya dini.
“Wazazi wetu hawajui kinachoendelea kuhusiana na vita, wanachokijua ni kwamba tunaenda kusomea dini, tunachukuliwa tukiwa wadogo sana kati ya umri wa miaka mitatu hadi minne.
“Viongozi hao wa dini wapo hapa nchini kwa muda mrefu na wapo katika taasisi za dini. Wamekuwa viongozi katika majengo hayo ya kuabudia na wana mtandao mkubwa duniani. Ni vigumu serikali kutambua kinachoendelea kwa watoto kwani wanaamini ni masuala ya dini tu.
“Wamekuwa wakitumia majengo ya ibada yaliyopo Gongo la Mboto na Kinondoni jijini Dar es Salaam, Morogoro, Iringa na Tanga. Zanzibar majengo hayo yapo Sabasaba, tunapofika Pakistan tunakutana na watoto wengine kutoka nchi mbalimbali duniani.
“Watoto wengine waliopo huko, wengi wao wanatoka hapa nchini, Kenya, Ethiopia, Yugoslavia, Afrika Kusini na Sudan. Tukiwa chuoni tunafundishwa kwamba ukijilipua kwenye mkusanyiko wa watu na kuwaua wote, unakwenda peponi.
“Tunatakiwa kuanza kufundishwa imani, mafunzo ya kikomandoo na hatua ya tatu kutiwa majini au nguvu za ziada za kutoa woga kwa ajili ya kupambana na maadui bila kurudi nyuma.
“Kuanzia miaka 10 tunakuwa tumeiva kimafunzo kiasi kwamba unapofikisha umri wa mika 15 unakuwa tayari kukabiliana na kitu chochote. Wakati huo inakuwa tayari kipindi cha kujiunga na vita kimewadia.
“Tuliingia vitani nchini Somalia tukiwa wafuasi wa Al –Shabaab, tulipigana kwa muda wa miezi sita. Nilinusurika kuuawa mara nyingi. Huwezi kuamini, kati ya Watanzania 25 tuliokuwa huko, tuliobaki ni wawili tu, 23 walikufa. Nikaamua kurejea nchini na mwenzangu ambaye alikwenda kwao Iringa.
“Mpaka leo hii tumeendelea kuishi kwa hofu kubwa, kwani tumekuwa tukitafutwa na Al-Shabaab. Hakuna mtu anayetupenda, sina makazi maalum. Ndugu mwandishi, sitaki kabisa sura yangu ionekane gazetini kwani itawafanya watu waniogope.
“Kwa sasa naishi hapa Dar es Salaam, kama raia mwema kabisa na sina matatizo na watu,” alimaliza kuelezea Ilah.
Wiki ijayo tutawaletea sababu iliyomfanya Aizak kubadili dini, jambo lililosababisha afukuzwe nyumbani kwao. Aidha, tutaona ushauri wake kwa jamii juu ya watoto kujiunga na Al-Shabaab.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Hivi ndivyo watanzania walivyojiunga na Al-Shabab
0 comments