Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Walichokosea wabunge wa Chadema, CCM hadi JK kukubali kujadiliana katiba mpya ni hiki

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakitoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Kilichotokea ndani ya Bunge la Muungano lililokutana hivi karibuni mjini Dodoma kujadili mchakato wa muswada wa Sheria ya Katiba Mpya ya mwaka 2011 kimewatia hofu kubwa wananchi kiasi cha wengi kuhoji nini hasa utakuwa mustakabali wa taifa letu siku zijazo.


Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba, wabunge badala ya kuujadili mchakato wa muswada huo katika muktadha wa kupata mwafaka na maridhiano ya kitaifa, wametofautiana vikali kiasi cha wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadhi wa NCCR kususia mjadala huo na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.


Kuna makosa ambayo wabunge wa pande mbili, wapinzani na chama tawala, wameyafanya ambayo ni lazima niyaeleze ili nao waweze kujijua na ikiwezekana kujifunza.


Kwanza, kitendo cha wabunge wa Chadema na baadhi wa NCCR kutoka nje ya ukumbi na kuacha kujadili au kutoa maoni ya kile walichokuwa wanakipinga lilikuwa ni kosa kubwa.


Tuliona jinsi walivyoshiriki mjadala wa mswada wa manunuzi, japokuwa John Mnyika (Chadema) na David Kafulila (NCCR) ndiyo walioonekana wachangiaji wakuu,lakini naamini mawazo yao yaliisaidia serikali.


Pili, kitendo cha baadhi ya wabunge wa upinzani kususia kikao kilisababisha kutokea kwa vitendo visivyotegemewa kutoka kwa wabunge wa CCM, CUF na TLP kwani nao badala ya kujikita katika mjadala wa ajenda ya muswada iliyokuwa mezani, waliligeuza bunge kuwa jukwaa la kisiasa na vijembe dhidi ya Chadema na wabunge wake, kiukweli haikuwa mahali pake.


Kila mbunge wa CCM na CUF aliyesimama kujadili muswada huo alitumia muda mwingi kutoa kauli za kuudhi na zisizokuwa za kibunge dhidi ya chama hicho, wabunge wake na spika au wenyeviti wa vikao wakikaa kimya bila kukemea vitendo hivyo au kuwataka wabunge hao wafute kauli zao.


Kwa mfano katika kikao kimoja cha asubuhi, mbunge mmoja alidiriki kuwaita wabunge wa Chadema ‘waovu’, lakini mwenyekiti wa kikao hicho alikaa kimya bila kukemea.


Ndugu zangu, lazima niseme ukweli kwamba, vitendo vya aina hiyo vinalidhalilisha Bunge mbele ya wananchi kwa sababu wanaona wanapoteza muda wao kwa kujadili majina ya watu au chama badala ya hoja za muswada wa katiba ambao ni kitu kizito sana katika nchi.


Mimi na wananchi wenzangu tulishuhudia katika kikao hicho cha bunge wabunge wakizomeana na kutoleana maneno ya kashfa badala ya kutoa hoja zenye mantiki kwa lengo la kuuboresha mchakato wa muswada huo ili hatimaye taifa letu lipate katiba nzuri itakayolinda matakwa ya raia wote bila kujali itikadi.


Kwa taarifa viongozi wa serikali wanapaswa kutambua kwamba, katika kuandika katiba mpya (constitution making) mahali popote duniani, wanaobeba dhima ya kusimamia mchakato huo hulazimika kuhakikisha mwafaka wa kitaifa unapatikana katika kila jambo linalojadiliwa kwa kuzingatia dhana kwamba kila wazo ni muhimu katika mchakato huo.


Bila kufanya hivyo niiambie serikali yetu kuwa katiba inayopatikana hukataliwa kwa sababu huwa siyo ya wananchi, hivyo hukosa uhalali (legitimacy) na kuonekana kazi yote iliyofanyika ni bure.


Hakika kikao kile cha bunge kilichafua mchakato mzima wa kuelekea kwenye kupata katiba hiyo, tulitegemea wabunge wajadiliane na kukubaliana juu ya tume za uchaguzi za bara na visiwani ambazo zinalalamikiwa kila chaguzi na wagombea wa chama tawala au wapinzani kusimamia kura za kupitishwa kwa katiba mpya. Je, kuwapa hao haki ya kusimamia zoezi hilo ni sawa? Kuna msuguano hapo.


Kwa nchi za wenzetu, hali ya msuguano inapotokea, serikali haisemi ‘potelea mbali,’ bali juhudi za makusudi hufanywa kuhakikisha makundi yote yanasikilizwa bila ubaguzi wowote na kumaliza tofauti zao kabla ya katiba kuandikwa upya. Ndiyo maana nampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukubali kuonana na viongozi wa Chadema.


Bila shaka Rais Kikwete atasikiliza hoja zilizotolewa na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwamo wanaharakati naamini atazipa uzito stahiki badala ya kubezwa na kudharauliwa.


Ndugu zangu, hoja kwamba muswada huo haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kama ilivyofanyika ilikuwa ni hoja yenye uzito mkubwa kwa kuzingatia ukweli kwamba, marekebisho yaliyofanyika kwenye muswada huo baada ya kuondolewa bungeni mara ya kwanza yalikuwa makubwa mno, hivyo muswada huo ilibidi usomwe mara ya kwanza kisha upelekwe kwa wananchi waweze kuujadili, kulikuwa na tatizo gani kufanya hivyo?


Wabunge wote pamoja na spika, wanaelewa kuwa Bunge lilipourudisha muswada huo serikalini ili, pamoja na mambo mengine uandikwe katika lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza kama ulivyoandaliwa awali, wananchi waliona hatua hiyo kama fursa pekee ya kuwawezesha kuujadili kikamilifu kifungu kwa kifungu na kwa uelewa mkubwa baada ya kuelimishwa kwa wale wasiouelewa.


Ni vyema nikasema kuwa serikali na uongozi wa Bunge wamefanya kosa la kudhani kwamba kitu muhimu zaidi kwa wananchi ni kutoa mawazo kuhusu katiba wanayoihitaji badala ya kujadili muswada wa namna ya kukusanya maoni yao (wananchi).


Makundi ya kijamii yamehoji madaraka makubwa aliyopewa rais katika mchakato wa kupata maoni ya wananchi kwani wamesema yeye ndiye ataunda vyombo na kuteua watendaji wa kusimamia mchakato huo.


Kwamba licha ya kuteua wajumbe 116 watakaoungana na wabunge wa Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge la Katiba, rais pia anapewa mamlaka ya kutoa hadidu za rejea.


Asasi za kijamii wanasema wabunge au wajumbe wa baraza la wawakilishi wasihusishwe na bunge la katiba na badala yake watunge sheria za kuwezesha bunge na tume ya katiba kuundwa.


Kibinadamu huwezi kujitungia sheria kwa kitu kizito kama katiba ya nchi, unaweza kujipendelea. Kifupi suala hili la mchakato wa kuandikwa katiba mpya linahitaji mjadala mzito na siyo kama walivyofanya baadhi ya wabunge wiki iliyopita ambao muda mwingi waliutumia kujadili chama na watu.


Fursa ya kupata mwafaka na maridhiano bado ipo na si vyema kungoja misuguano inayotoa cheche itokee ndipo watu wakae kujadiliana. Naamini katiba ya nchi ndiyo mlinzi wa amani na gharama ya amani ikitoweka huwa ni kubwa sana, hivyo kukaa meza moja na wadau ni kitu muhimu ili katiba isikataliwe na wananchi. Ndiyo maana nampongeza Rais Kikwete kwa kukubali kukaa mezani na Chadema ili kusikiliza hoja zao.


Kuamini kwamba mwishoni wananchi watapiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’ na kwamba wengi wakisema hapana itatumika katiba ya sasa, bila kusema kwa muda gani, ni kosa pia.


Kama taifa ikija kukataliwa hiyo katiba mpya tutakuwa tumefeli na kupoteza fedha nyingi za walipa kodi kwa sababu lengo litakuwa halijafikiwa muafaka na waliosababisha watabeba lawama.

0 comments

Post a Comment