Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Spika aunda kamati ya kumchunguza Jairo. Bunge lahitimishwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter INAUNDWA NA WABUNGE WATANO KUTOKA CCM, CHADEMA, CUF
Neville Meena, Dodoma
MKUTANO wa nne wa Bunge la Bajeti ulihitimishwa jana kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kutangaza majina ya wabunge watano, wanaounda Kamati Teule kuchunguza utaratibu uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini, kukusanya fedha kutoka katika taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kupitisha wa bajeti.

Makinda akihitimisha Bunge baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa hoja ya kuahirisha bunge, alisema kamati hiyo itakayofanya kazi kwa wiki zisizozidi nane pia itachunguza  iwapo hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutangaza matokeo ya uchunguzi dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo uliingilia haki na madaraka ya Bunge.

Hii ni kamati teule ya pili kuundwa wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, lakini kwa wizara hiyohiyo ya Nishati na Madini ambayo hivi sasa inaongozwa na Waziri William Ngeleja.

Februari 7, 2008 aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mkataba tata wa Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Richmond.

Kamati hiyo iliongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dk Harrison Mwakyembe. Mwakyembe sasa ni Naibu waziri wa Ujenzi.

Wanaounda kamati ya kumchunguza Jairo ni mbunge wa Tunduru Kaskazini, Injinia Ramo Makani (CCM), Mbunge wa Karagwe, Goesbert Blandes (CCM), Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Jachi Umbulla (CCM).

“Mtakumbuka kwamba tarehe 24, Agosti, 2011, Bunge lilipitisha azimio la kuunda Kamati Teule kwa ajili ya kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti na kubaini kama kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizokuwa zikichangishwa na Wizara ya Nishati na Madini kimeingilia na kuathiri madaraka ya Bunge," alisema Makinda na kuongeza:

"Sasa napenda kuwataarifu kwamba utaratibu huo umekamilika na kamati hiyo nimeiunda kwa mujibu wa Kanuni ya 2(2) na 117(4) ya Kanuni za Bunge toleo la 2007".

Makinda alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa kuongozwa na hadidu tano za rejea ambazo ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa Hotuba za bajeti za wizara bungeni na kwamba, hadidu hiyo ya kwanza itakuwa na vipengele vitatu.

Vipengele hivyo ni pamoja na kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni, iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.

"Hadidu rejea ya pili ni kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara hiyo Bungeni," alisema Makinda na kuongeza:

"Hadidu rejea ya tatu ni kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kuarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo".

Makinda alisema hadidu rejea hiyo ya tatu ina vipengele viwili ambavyo ni kuchunguzwa kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.

Aliitaja hadidu ya rejea ya nne kuwa ni kuangalia nafasi ya Mamlaka ya Uteuzi kwa ngazi za Makatibu Wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na ya mwisho inawaelekeza wajumbe wa Kamati hiyo kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na uchunguzi huo.

“Ni imani yangu ya wabuge wote na Watanzania wote kwa ujumla kwamba ninyi niliowateua mtafanya kazi hii kwa umakini, busara na uaminifu mkubwa mkiongozwa na Katiba ya nchi, sheria na kanuni zetu na vilevile mtatoa haki kwa watu wote watakaohusika na suala hili," alisema Spika Makinda.

Rais Kikwete alimsimamisha kazi Jairo kwa mara ya pili ili kupisha uchunguzi zaidi juu ya tuhuma zinazomkabili kuhusiana na matumizi mabaya ya madaraka yake.


Hatua hiyo ilithibitishwa juzi na Waziri Mkuu, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni. Pinda alisema kuwa, suala la Jairo limefika kwa Rais na tayari kiongozi huyo wa nchi amekwishalitolea uamuzi.

Jumanne wiki hii wabunge walitishia kusimamisha shughuli zote za Serikali katika Bunge hilo hadi hapo uchunguzi wa Jairo ambaye alituhumiwa na Mbunge wa Kilindi kuwa anahusika na uchangishaji wa fedha zitakapopelekwa bungeni.

Kitendo cha wabunge kutoa kauli hiyo kilitokana na kauli ya Luhanjo kutangaza kuwa Jairo hakupatikana na hatia katika uchunguzi uliofanyika na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba, alitakiwa kurudi kazini kuanzia Jumatano.Uamuzi wa kuundwa kwa kamati teule ulifikiwa Jumanne baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kusema kuwa Luhanjo alikuwa amelidharau Bunge na Waziri Mkuu.

0 comments

Post a Comment