Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Membe: Tanzania haitakurupuka kutambua waasi Libya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Raymond Kaminyoge  
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Tanzania haitakurupuka kuitambua serikali ya mpito ya  waasi wa Libya wakati bado vita inaendelea.  

Membe alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wa mgogoro wa Libya.  Msimamo huo wa Tanzania kuhusu mgogoro wa Libya, unakuja wakati mapigano kati ya waasi na wanajeshi wanaomtii Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, yakiwa yamepamba moto hasa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.  

Akitoa msimamo hu, Membe alisema serikali itatambua Libya,baada ya waasi kuapishwa na kuweka serikali ya mpito itakayoungwa mkono na Walibya wenyewe.  “Tanzania haiwezi kukurupuka kuitambua Libya wakati bado vita inaendelea, kwani  tunakimbilia wapi, viongozi hao wa waasi wakishaapishwa ndipo tunaweza kuwatambua,” alisema.  

Kwa mujibu wa Membe, nchi za Afrika ziizoitambua serikali ya waasi wa Libya ni pamoja na Kenya, Botswana, Ethiopia, Djibut, Rwanda na Tunisia.  Nyingine ni Senegal, Gabon, Gambia, Bokina Faso, Benin na Nigeria.  Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 41 za Afrika ambazo bado hazijaitambua serikali ya mpito ya waasi wa  Libya.

Membe alisema Tanzania inajua kwamba hatima ya Kanali Muammar Gaddafi kuongoza Libya imekwishafikia, lakini haiwezi kuwatambua waasi wakati bado hawajaunda serikali.   “Serikali ni pamoja na kuwa na viongozi walioapishwa,  tutawatambua kama watakuwa na  mihimili mitatu ya serikali, bunge na mahakama,” alisema Membe.  

Alizitaka pande zinazoendelea kupigana nchini Libya kusitisha mapigano, ili kuepusha umwagaji wa damu.   Wakimbizi wa Kisomali   Waziri Membe alisema serikali haiko tayari kuwapokea wakimbizi  kutoka Somalia, kwa sababu nchi bado ina wakimbizi wengi kutoka katika nchi za maziwa makuu   Membe alisema hayo wakati akijibu swali kama Tanzania iko tayari kupokea wakimbizi kutoka Somalia. 

“ Hatuko tayari kuwapokea wakimbizi wa Kisomali kwa sababu bado tuna wakimbizi wengi, tuko tayari kusaidiana nao kwa hali na mali lakini si kwa kuwapokea kama wakimbizi,” alisema Membe.

  Membe alisema serikali imepeleka msaada wa tani 300 za mahindi nchini Somalia ili kukabiliana na baa la njaa linalopoteza maisha ya watu.  Alisema serikali imetenga tani 11,000 za mahindi ambazo zitauzwa kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Somalia  Taarifa zinasema kati ya watu 10,000 nchini Somalia, watu sita hufa kutokana na njaa kila siku. 

Membe alisema wasomali 800,000 wameihama nchi yao kama wakimbizi na kwenda katika nchi jirani.        

0 comments

Post a Comment