Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Jiji la Mwanza, Moshi laibuka tena kinara wa usafi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

  • Ni mara ya sita kwa upande wa majiji
  • Moshi mjini yang’ara kundi la manispaa
Jiji la Mwanza

MILIMA ya Matogoro katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, ndipo unapoanzia moja ya mito mikubwa nchini, Mto Ruvuma, lakini vyanzo hivyo vya maji vinakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira.
Manispaa ya Moshi
Wakazi wa Manispaa hiyo ya Songea ni watumiaji wakubwa wa mto huo wanaoutegemea kwa shughuli zao mbalimbali, kubwa kuliko yote ikiwa ni matumizi ya majumbani. Hao ni mbali ya wategemezi wengine wa mto huo maeneo unamopita kabla ya kuingia kwenye Bahari ya Hindi.


Innocent Nyoni kutoka Mtandao wa Mazingira Ruvuma anazitaja shughuli za binadamu kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira ya milima hiyo ambapo ni pamoja na upasuaji mbao, uchomaji mkaa, kilimo na uchomaji moto ambao huendelea kuwaka hata kwa zaidi ya mwezi.


Kuni na mkaa ndio chanzo kikuu cha nishati kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma huku shughuli za uchomaji matofali zikiongoza katika matumizi ya kuni; hivyo kuwa kichocheo kikuu cha ukataji miti mkoani humo.


Shughuli zingine zinazotajwa kuchangia katika uharibifu wa mazingira mkoani Ruvuma ni pamoja na ufugaji; hususani jamii za wafugaji waliohamia mkoani humo na kilimo hususani cha bustani kinachoendeshwa kwenye kingo za mito.


Hata hivyo, mkoa huo hauonekani kutoa kipaumbele katika suala zima la mazingira kama anavyobainisha Nyoni ambaye anaitaja Mamlaka ya Maji Mji wa Songea (SAUWASA) kuwa taasisi pekee yenye kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.


Sababu kubwa inayochangia katika kupuuzwa kwa suala la mazingira mkoani humo ni kukosekana kwa hamasa kuhusu suala zima la mazingira kuanzia kwa wananchi hadi viongozi wenyewe.


“Hawa SAUWASA wanaonekana wako peke yao katika kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira ya ile milima ya Matogoro, uhamasishaji na hamasa viko chini, serikali mkoani hapa haijatoa kipaumbele kwa suala la mazingira,” anasema Nyoni katika mahoniano yake na Raia Mwema.


Wakati hali ikiwa hivyo, jirani na milima hiyo ya Matogoro yalifanyika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani wiki iliyopita. Hapo ni katika Uwanja wa Mpira wa Majimaji ulipo kwenye Manispaa hiyo ya Songea mkoani Ruvuma ambako kuna tangazo la kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani isemayo “Misitu: Huduma yako ya Asili,” ambayo ni tafsiri ya Nature at Your Service.


Katika kuadhimisha miaka 50 ya uhuru, vile vile ipo kaulimbiu ya mazingigira ya kitaifa isemayo “Panda Miti na Kuitunza: Hifadhi Mazingira, huku Ujumbe wa Umoja wa Mataifa mwaka huu ukiwa ni “Mwaka wa Kimataifa wa Misitu”.


Hatua ya kupeleka maadhimisho hayo mkoani Ruvuma inaelezwa na wadau wa mazingira kuwa muafaka katika udhibiti na utunzaji wa mazingira mkoani humo.


Wadau hao wanaiona hatua hiyo kama moja ya njia sahihi ya kuamsha harakati za uhamasishaji na hamasa katika suala zima la udhibiti na utunzaji mazingira katika mkoa huo ambao ni muhimu katika ustawi wa taifa kutokana na kuwa miongoni mwa maeneo nchini yenye vyanzo vya maji ya mito mikuu na misitu ya asili.


Waziri wa Ardhi na Makazi, Prof. Anna Tibaijuka anaiona njia pekee ya kuokoa misitu nchini ni kwa wananchi kujenga utamaduni mpya wa kupenda na kuthamini miti; hivyo kuacha tabia ya kufyeka miti hovyo. Hii ikiwa ni pamoja na kudhibiti uchomaji moto misitu unaochangia kupotea kwa uoto wa asili, uchimbaji madini holela, ufugaji uliozidi kipimo na kilimo kisicho endelevu.


Prof. Tibaijuka, aliyemwakilisha Makamu wa Rais katika maadhimisho hayo alibanisha kuwa mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu, na ndio uhai wa Taifa lolote hapa duniani.


“Binadamu hawezi kuishi bila kutumia mazingira yanayomzunguka kwa mfano, ardhi, misitu na mimea mbalimbali, maji mimea na hewa. Pamoja na umuhimu wote huo bado tunashuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira; hususani uharibifu wa misitu.”


Alikumbusha baadhi ya mikakati ya taifa kuhusu mazingira ukiwemo ule wa kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji uliopitiswa na Serikali Aprili, 2006 ambao unagiza upandaji miti, kila wilaya ikitakiwa kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.


Inaelezwa kuwa baadhi ya wilaya zilivuka lengo katika msimu wa 2007/08 na 2008/09, na hizi ni pamoja na Arumeru, Mbozi, Makete, Mufindi, Ludewa, Njombe, Iringa, Kilombero, Ulanga, Mbinga, Nachingwea, Lindi, Kilosa, Kilwa, Maswa, Shinyanga Vijijini, Kahama, Bariadi, Meatu na Kishapu.


Mkakati mwingine alioutaja Prof. Tibaijuka ni ile Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Kupanda na Kutunza Miti aliyosema ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha wananchi kwenye kaya, taasisi, makampuni, mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali kujenga utamaduni wa kuhifadhi vyanzo vya maji, kupanda ya kutunza miti.


Hata hivyo, ni dhahiri kwamba suala la ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni halikupewa umuhimu sana katika maadhimisho hayo kutokana na ukweli kwamba ndio tegemeo la nishati kwa Watanzania, japo ni shughuli inayofahamika kuwa kikwazo katika utekelezaji wa MKUHUMI.


Msimamo wa serikali uko wazi, kwamba haiwezi kuzuia wananchi wake kutumia kuni na mkaa kwa sababu ya kukosekana nishati mbadala, ikitilia maanani kwamba kuwazuia ni sawa na kuwambia wasile.


Pamoja na ujumbe wa mwaka huu kuweka mkazo zaidi katika utunzaji misitu, bado suala la usafi wa mazingira ya miji na maeneo mengine nchini limendelea kupewa kipaumbele wakati wa maadhimisho ya mwaka huu, ambapo miji iliyofanya vizuri ilizawadiwa siku hiyo.


Katika maadhimisho ya mwaka huu, Jiji la Mwanza limeendelea kutesa kwa kuibuka kinara wa usafi katika kundi la majiji nchini liliposhika nafasi ya kwanza, Moshi Mjini ikibuka mshindi kundi la Manispaa, Mji wa Mpanda ukiongoza kundi la Halmashauri za Miji na Njombe ikiongoza kundi la Halmashauri za Wilaya.


Hii ilikuwa ni mara ya sita sasa kwa Jiji la Mwanza kuongoza kwa usafi miongoni mwa jiji yaliyopo nchini, na kutokana na ushindi huo wenyewe wanasema wanajiandaa kuingia kwenye Premium League ya usafi duniani.


Akionyesha furaha yake kutokana na ushindi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe alisema:“Nataka kuingia Premium League katika usafi.”


Hata hivyo, anaitaja sababu kuu inayolifanya jiji hilo liibuke mshindi kila mwaka kuwa ni hatua ya wananchi kubadili tabia kutoka kutochukulia uchafu kama sehemu ya maisha yao hadi kuuchukia na kupenda usafi, na kwamba sasa wamejenga utamaduni wa usafi.


“Usafi ndio kipaumbele chetu cha kwanza. Attitude (hulka) ya usafi hivi sasa imejingeka miongoni mwa wakazi wa Mwanza. Wananchi hivi sasa wanapenda usafi. Kumekuwepo na ushirikishwaji wa wananchi na uanzishaji wa vikundi vya usafi,” alisema Kabwe.


Halmashauri ya Mji wa Mpanda kwa upande wake imefanikiwa kuongoza kwa usafi katika kundi la Halmashauri za Miji baada ya kufanya mapinduzi makubwa katika usimamizi wa usafi ndani ya mji huo.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji huo, Enock Gwambasa anaitaja mikakati iliyofanikisha katika usafi wa mji huo kuwa ni pamoja na kufunga madampo manne yasiyo rasmi yaliyokuwemo ndani ya mji huo na badala yake kutengeneza bustani kwenye maeneo hayo kwa kuwa tangu awali yalikuwa ni maeneo ya wazi.


Mwenyekiti huyo anaitaja mikakati mingine kuwa ni kuunda vikundi kazi kwa ajili ya kusimamia zoezi zima la utupaji taka hovyo na kuhamasisha wananchi kulipa ushuru wa taka wa Shilingi 1,000 kwa mwezi kwa kila kaya. Kazi ya fedha hizo ni pamoja na kutengeneza mikokoteni ya kusomba taka kutoka kwenye kaya, kununulia vifaa vya kazi kama vile gloves na gum boots, posho kwa ajili ya vikundi kazi na askari wa mazingira.


Katika kuhakikisha mji wao unakuwa msafi muda wote, mamlaka ya mji huo ilihakikisha barabara zinajengwa kwa kuzingatia viwango, ujenzi wa mifereji ya maji, utunzaji wa miti iliyopo na kuzuia mifugo kuzurura mjini.


Umoja wa Mataifa umeutangaza mwaka huu kuwa ni wa misitu, kaulimbiu na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani nayo inaimba kuihusu misitu ikisema Misitu: Huduma yako ya Asili, lakini wakati huo huo Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi ya nishati ambayo ni wazi inadhofisha utekelezaji wa mpango mzima wa MKUHUMI.


Hapa hakuna njia ya mkato zaidi ya kuelekeza nguvu katika nishati mbadala na rafiki kwa mazingira, Tanzania ikidhamiria inaweza, na ikifanikiwa hapo ndipo hata maadhimisho ya mwaka huu mkoani Ruvuma yatakapokuwa na maana zaidi.

0 comments

Post a Comment