Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA - Zitto kuthibitisha madai yake leo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MBUNGE Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe leo anatarajiwa kuthibitisha madai yake bungeni kwamba Baraza la Mawaziri limeshawishiwa kufikia uamuzi wa kutaka kuliua Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma nchini, (CHC).


Zitto alitoa kauli hiyo Juni 23, mwaka huu wakati akichangia Azimio la Serikali kutaka kuongeza muda wa uhai wa shirika hilo kwa miaka mitatu na baadaye shughuli zake zipelekwe kwa Msajili wa Hazina (TR).


Alisema anaamini hatua hiyo ya Serikali imetokana na watu wachache waliofanikiwa kulishawishi Baraza la Mawaziri ili wanufaike kwa namna moja au nyingine kwa kuwa mpango huo haukupendekezwa na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na Kamati ya Mashirika ya Umma.


“Jamani tulikubaliana vingine kabisa katika Kamati, leo kilicholetwa hapa ni kitu kingine. Kamati ya Fedha na Uchumi ilijadili na kutaka shirika hili lipewe muda zaidi kutokana na majukumu yaliyopo mbele yake, lakini hiki kilicholetwa hapa ni kitu kingine.


“Wabunge kataeni haya maamuzi ya Baraza la Mawaziri, yametokana na ushawishi wa watu wenye lengo la kuua CHC kwa ajili ya maslahi yao."Ikumbukwe kuwa chombo hiki kinaangalia mali za umma na mashirika, lakini pia kuna kesi mbalimbali za watu ambao wanadaiwa na mashirika, hivyo kwa kuja na hoja hii ni sawa na maandalizi ya wizi,” alisema Zitto.


Kauli hiyo ilimwingiza katika mgogoro mwingine bungeni baada ya Waziri wa Nchi (Sera na Uratibu), William Lukuvi kumtaka alithibitishie bunge kwa ushahidi kuhusu madai hayo.


Kutokana na kauli hiyo Spika wa Bunge Anne Makinda, alilazimika kumpa mbunge huyo siku saba hadi leo kuthibitisha kauli yake.Baada ya maneno hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) George Mkuchika, aliomba mwongozo wa Spika kutaka Zitto athibitishe kauli yake.


Zitto aliliambia gazeti hili kuwa hadi jana mchana alikuwa hajawasilisha ushahidi ofisi ya Bunge, lakini anapanga kuwasilisha leo kwa barua kwenda kwa Spika.


“Sijawasilisha,”alisema Zitto saa 10:00 jioni jana kwa ujumbe mfupi alioutuma kwa mwandishi wa habari.Alipoulizwa atatumia njia gani kuwasilisha ushahidi huo, alijibu:“Kwa barua kwenda kwa spika.”

0 comments

Post a Comment