*Ni kufuatia kamatakamata ya wabunge wa Chadema akiwemo Mbowe
*Asema uvumilivu basi, watu waingie mtaani
*Asema uvumilivu basi, watu waingie mtaani
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amewataka wafuasi wa chama hicho nchi nzima kuingia mitaani kupinga vitendo vya Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wao wakiwemo wabunge bila kufuata utaratibu.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku mbili baada ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto kukamatwa na polisi wakihusishwa na matukio tofauti.
Wakati Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, akikamatwa na kushikiliwa jijini Dar es Salaam kufuatia amri ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, akidaiwa kuidharau Mahakama, Zitto alikamatwa na kuhojiwa kisha kuachiwa mkoani Singida akidaiwa kuzidisha muda wa mkutano wa hadhara.
Akitoa msimamo wa chama leo mbele ya waandishi wa habari, Dk. Slaa alisema wamechoshwa na unyanyaswaji wa polisi na Serikali, na hivyo akawaagiza wananchi kuingia mitaani nchi nzima, huku akidai wasilaumiwe kwa lolote litakalotokea.
“Tumekuwa wavumilivu na watulivu kama kondoo lakini ukondoo wetu sasa basi, tunawasiliana na jumuiya za kimataifa zilizoko hapa nchini na nje na kuishtaki Tanzania tukitaka ifukuzwe hata kwenye jumuiya mhimu kama IPU na CPA. Naomba wala tusinekane hatuna uzalendo,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa wanataka kuueleza ulimwengu kuwa vyombo vya dola na mahakama vimeacha kusimamia sheria na sasa vinafanya kazi ya kisiasa ya kuwanyanyasa wapinzani kwa maelekezo ya watawala.
Dk. Slaa alikiri kupigiwa simu na wakuu wa jeshi la polisi jijini Dar es Salaam jana asubuhi wakimuomba awatulize vijana waliokuwa wamekusanyika makao makuu ya polisi wakitaka Mbowe aachiwe, ombi alilosema alilikataa na badala yale anawataka wajitokeze mitaani.
“ Nimewaeleza polisi kuwa wao na Serikali ndiyo wanachochea vurugu kwa kuwanyanyasa viongozi wa CHADEMA na nikawaambia sitawazuia vijana wangu bali nitawataka wajitokeze kupinga uonevu huu,” alisema Dk. Slaa.
Kuhusu kuendelea kushikiliwa kwa Mwenyekiti wao, Dk. Slaa alisema wametoa maagizo kuwa ikiwa hatafikishwa mahakamani leo na kuachiwa bila masharti yeyote, chama kitawazuia wabunge wake kuhudhuria vikao vya Bunge vya mkutano wa nne vinavyoanza Kesho.
“Kesho, kuna kikao mhimu cha kamati ya uongozi ambacho wajumbe wake mbali na Spika na Waziri Mkuu pia Mbowe na Zitto ni wajumbe. Sasa Serikali ione maagizo yake ya kukurupuka yatakavyoathiri shughuli za Bunge, maana watu wetu hawapo,” alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, wamemzuia Zitto asihudhurie kikao hicho cha kamati ya uongozi na wala hawatatuma mwakilishi yeyote kwa vile wamegundua wameundiwa njama za kuifanya kesi ya Mbowe na wenzake iwe ya kisiasa badala ya sheria ili asipate muda wa kuandaa hotuba yake ya bajeti ya upinzani.
Akithibitisha hilo, Dk. Slaa akikuwa ameambatana na wabunge wengi wa chama hicho, alisema licha ya Mbowe kufika polisi mwenyewe na kufanya mahojiano, walishangaa ghafla kuona kiongozi huyo anageuziwa kibao na kuambiwa atakuwa kizuizini.
“Nimetoka Arusha kwenye kesi yetu hiyo, lakini tunashangazwa na Hakimu kuitaja akijua hatutakuwepo na kutoa amri kwa polisi kutukamata wakati alikwisha kutukubalia hadi shughuli za Bunge zikimalizika,” alisema Katibu huyo.
Aliobainisha kuwa ameshangazwa na amri hiyo wakati katika rekodi za mahakama hakuna kumbukumbu zinazoonesha Mbowe na wadhamini wake wanatakiwa kukamatwa. Pia wadhamini wa Mbowe hajapelekewa kibali cha kuoneshwa sababu ya mdhaminiwa wao kukamatwa.
“Tukiunganisha matukio yote ya kamatakamata ya wabunge wetu kule Arusha, Tundu Lissu na Esther Matiko kule Tarime, Magdalena Sakaya wa CUF kule Tabora alikokamatwa na kuweka ndani hadi sasa na jana (juzi) Zitto na Mbowe ni dhahiri kuna siasa ndani yake na si sheria tena. Nasi hatuko tayari kwa hilo,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kama wabunge wa CCM hawakamatwi hovyo na polisi hadi kuwepo na kibali cha Spika kutoka ofisi ya Bunge, inakuwaje kwa wabunge wa upinzani polisi wanakamata tu?
“Zitto amekataa kuandika maelezo polisi naye ametaka polisi wamwoneshe kibali cha Spika ndipo atakuwa tayari kufanya hivyo. Polisi hawa wameomba kibali kwa Spika ili kumhoji mbunge wa Busega (CCM), Dk. Titus Kamani, anayedaiwa kutaka kuua,” alisema Dk. Slaa.
Mpaka mtandao huu unaondoka makao makuu ya chama hicho, viongozi walikuwa wakiendelea na kikao cha dharura na nje vijana wengi walikuwa tayari wamejikusanya kuanza maandamano ya kuelekea polisi anakoshikiliwa Mbowe.
0 comments