Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bajeti ya Waziri Magufuli tishio

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KIPAUMBELE cha serikali katika Bajeti inayotarajiwa kusomwa wiki ijayo kitakuwa ni miundombinu baada ya kuelezwa kwamba Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na Dk John Magufuli imetengewa kiasi kinachokaribia Sh1.5 trilioni.Kiasi hicho cha fedha ambacho ni kikubwa kupita bajeti ya wizara zote nchini (ukiondoa Ofisi ya Waziri Mkuu), ni sawa na asilimia 11.53 ya bajeti nzima ya serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 inayokadiriwa kuwa itafikia Sh13 trilioni.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba alisema kutokana na kutengewa kiasi hicho, serikali sasa itakuwa na uwezo wa kujenga madaraja katika maeneo mbalimbali likiwamo lile la Kigamboni, Dar es Salaam; Mto Malagarasi uliopo mkoani Kigoma na Mto Kilombero.


"Takwimu zinaonyesha tangu tupate Uhuru hadi sasa barabara zetu zipo katika kiwango cha lami kwa kilomita 6,000, lakini mipango ya wizara baada ya miaka miwili ijayo ni iwe imefikia kilomita 11,500," alisema Serukamba na kuongeza:


"Magufuli amefanya kazi nzuri na bajeti yake imejitahidi kugusa sehemu zote za Tanzania."Alisema kamati yake imemtaka Dk Magufuli kuendela kusimamia sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuendelea kubomoa nyumba ambazo zinastahili na kulipa fidia kwa wale wanaostahili.


Kwa mujibu wa Vitabu vya Makadirio vya Bajeti ya Serikali ambavyo Mwananchi limeviona, Wizara ya Ujenzi imetengewa kiasi cha Sh 1,250,976,939,000 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kiasi cha Sh245,437,094,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida hivyo kufanya jumla ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya wizara hiyo kufikia Sh1,496,414,043,000.


Fedha hizo ni nyongeza ya asilimia 29 ya kiasi kilichotengwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 31, mwaka huu ambacho kilikuwa Sh1.064 trilioni zikiwemo Sh871.553bilioni za maendeleo na Sh293.429 za matumizi ya kawaida.


Kauli ya Mkulo
Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alipoulizwa kuhusu bajeti hiyo ya Sh1.5 trilioni kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi alisema:"Kama kamati imepitisha kiasi hicho cha fedha basi waseme na vyanzo vya fedha hizo, si kupitisha tu," alisema Mkulo.


Alisema ni lazima bajeti iendane na uwezo wa serikali kwa wakati uliopo hivyo wasiwadanganye wananchi… "Mwulize Serukamba anajua atakapopata fedha hizo. Mimi najiandaa kwenda kuwapunguzia wananchi ugumu wa maisha tukienda Dodoma (bungeni) na huu si wakati wa kutafuta 'popularity' (umaarufu)."


Uchukuzi wako gizani
Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), alisema kamati yake imepitisha bajeti ya wizara mbili na kukwamisha ya Uchukuzi kwa kuwa serikali haijaweka fedha za kuboresha reli na za kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).


"Tunashangaa kwa nini serikali haioni kama suala la Reli ni muhimu. Ni lazima iweke fedha humo. Tumesisitiza kwenye reli lakini fedha hazipo. Inawezekana mpango upo, lakini kama fedha hazipo kwenye vitabu maana yake hakuna kitu," alisema Serukamba.


Alisema reli inahitaji kiasi cha Sh240 bilioni lakini inashangaza Wizara ya Fedha na Uchumi kuwekewa kiasi cha Sh129 bilioni cha matumizi mengineyo."Bajeti nzima ya mwaka huu ni Sh13.5 trilioni hivyo fedha za matumizi mengine zipo nyingi tu ndani yake ambazo tunaweza kuzipunguza na kuziweka kwenye reli na ATCL," alisema Serukamba.


Kwa upande wa Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia alisema kamati hiyo imepitisha Sh64 bilioni kwa kuwa imeridhika na maelezo ya wizara hiyo."Mambo watakayofanya ni pamoja na mkongo wa taifa wa mawasiliano, anuani za makazi na fedha za utafiti zipo humo na pia kuhakikisha mitandao ya simu iwepo ili nchini kote kuwe na mawasiliano," alisema Serukamba.


Waziri Mkuu yatengewa Sh3.2trilioni
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imepitisha mapendekezo ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayofikia Sh3.2 trilioni.


Kamati hiyo imepitisha mapendekezo hayo huku ikiitaka Tamisemi kuweka kipaumbele katika miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zote nchini.Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika alisema kati ya fedha hizo, Sh2.3 trilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na zilizobaki zitatumika kulipa mishahara watumishi wake.


Alisema hiyo itaziwezesha halmashauri nchini kusimamia miradi yake na kuongeza mapato ambayo yatatumika kwenye zake shughuli mbalimbali za kimaendeleo.“Matumaini yangu ni kuhakikisha kuwa, fedha hizi zinatumika kwa ajili ya kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kulipa mishahara watumishi wake, jambo ambalo tunaamini linawezekana,” alisema Mkuchika.


Alisema kuwa wizara hiyo imeiomba kamati hiyo kuwaachia fedha zinazotokana na miradi ya maendeleo ili waweze kuboresha miradi hiyo ambayo itachangia kuimarisha shughuli za kimaendeleo.Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pindi Chana ameitaka Wizara hiyo kuwashughulikia watendaji wasio waadilifu na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.


“Kila mkoa una bajeti yake, lengo ni kuimarisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao, kutokana na hali hiyo watendaji wasio waadilifu wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Chana.


Kamati ya Makamba yakubali bajeti
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepitisha mapendekezo ya bajeti ya Wizara hiyo ambayo ni Sh404.4 bilioni lakini ikiitaka kuweka vipaumbele katika miradi mipya ya umeme pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo wa majini katika maeneo yanayozunguka migodi.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo January Makamba aliliambia gazeti hili jana kuwa, kati ya fedha hizo, Sh327 bilioni zitatumika kwa ajili ya miradi mipya ya maendeleo na zilizobaki kwa ajili ya matumizi ya kawaida.


Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) alisema kamati hiyo imeitaka Wizara ya Nishati na Madini kupeleka umeme vijijini ili wananchi wa aina zote waweze kunufaika na huduma hiyo tofauti na sasa inavyopatikana maeneo mengi ya mjini pekee.“Tumeitaka Wizara kuhakikisha kuwa, bajeti yake inaweka kipaumbele kwenye miradi mipya ya umeme na kusambaza hadi vijijini ili kila mmoja aweze kunufaika na huduma hiyo ambayo imeenea mjini,” alisema Makamba.


Alisema mbali na fedha hizo, Wizara ilitenga kiasi cha Sh1.3 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo katika vijiji vinavyozunguka migodi ili waweze kufanya kazi zao katika hali nzuri na mazingira ya kisasa, jambo ambalo wanaamini linaweza kupunguza migogoro.

0 comments

Post a Comment