Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Wanafunzi Tabora Girls waua mlinzi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, wamemuua mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Rukwa Security ya mjini Tabora baada ya kumkuta akiiba katika lindo lake la kazi.

Habari za kuaminika kutoka katika lindo lake la kazi Shule ya Tabora Wasichana, mlinzi huyo alishambuliwa na wanafunzi wa shule za sekondari za Tabora Wasichana na Tabora Wavulana usiku wa manane.

Habari hizo zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, zimesema kuwa, mlinzi huyo aliyekuwa na mwenzie walishirikiana kuvunja stoo ya kuhifadhia vitu mbalimbali vya shule hiyo hivyo kuanza kuiba.

Taarifa zimeeleza kuwa baada ya kuanza kuiba vifaa hivyo, walinzi hao walikutana na vijana waliokuwa wakifanya doria kwa ajili ya kudhibiti wizi shuleni, ambao walipiga kelele zilizowafanya wanafunzi waliokuwa wamelala bwenini kuamka na kuwashambulia.

Taarifa zimemtaja mlinzi aliyepoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Luwali Idd (45), ambaye alishambuliwa na kufariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete, alikopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Taarifa hizo zimemtaja mlinzi aliyejeruhiwa kuwa Mohamed Rashid (48), ambaye amelazwa katika hospitali hiyo kwa matibabu na hali yake bado ni mbaya.

Mlinzi huyo alisema, yeye hakuwa katika lindo hilo, lakini aliitwa na mwenzake na kujikuta akiingia katika mtego wa wizi.

Mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari, Hellen Makala, alisema, wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakilalamikia matukio ya wizi wa vitu vyao hali ambayo iliwafanya wapange zamu ya kufanya ulinzi shirikishi nyakati za usiku.

Hata hivyo alisema, juhudi hizo za wanafunzi zimezaa matunda sasa baada ya kukamatwa kwa wezi hao na kuongeza kuwa zaidi ya vitanda 500 vilivyokuwa vikitumiwa na wanafunzi shuleni hapo vimetoweka katika mazingira yasiyofahamika.

Kamanda Barlow, amesema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini njama na mbinu zilizokuwa zikitumiwa na walinzi hao kuiba mali za shule.

Alisema, mtuhumiwa Mohammed atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi huo kukamilika ili ajibu tuhuma zinazomkabili.

0 comments

Post a Comment