Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - CHADEMA waweka wazi matumizi yao ya fedha, mshahara wa Dk. Slaa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Kwa nyakati tofauti, Mukama na Nape wamekaririwa wakiwashutumua viongozi wakuu wa CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, kwa maelezo kuwa wameshnikiza mshahara mkubwa wa Sh milioni 7.5 kwa Dk Slaa, na uuzaji wa magari matatu ya Mbowe kwa pesa nyingi mno.

Komu jana alisema kwanza Mukama na Nape wanapotosha umma kuhusu ukweli wanaoujadili, na akasema hata hiyo sehemu ya ukweli wanaougeuza tuhuma imeshapitwa na wakati, kwa kuwa CHADEMA hakifanyi mambo kwa kificho, na kilishafafanua hoja hizo.

Alisema Dk. Slaa hajawahi kushinikizwa alipwe Sh.7.5 milioni. "Kwanza, hatumlipi kiasi hicho, lakini pia Dk. Slaa hajawahi kuomba, kushinikiza wala kuchagiza kulipwa kiasi hicho cha fedha kama ambavyo viongozi wa CCM wanavyotaka kuaminisha umma," alisema Komu.

Badala yake, alisema, chama ndicho kilipanga jinsi ya kumwezesha Dk Slaa kwa kuwa ndicho kilichomwomba agombee urais, huku kikujua kuwa angegombea ubunge na kushinda kirahisi.

Lengo la chama kufanya vile ni kumwezesha Dk Slaa kutenda vema kazi zake za katibu mkuu kama alivyokuwa akitenda kazi za ubunge; hivyo kwa pamoja wakakubaliana awezeshwe kulingana na masharti ya utumishi katika nafasi ya ubunge.

Huku akikosoa takwimu za Nape, Komu alisema Dk. Slaa analipwa Sh 7,174,000 kama kwa mwezi, na si Sh. 7,500,000.

Alisema vilivyochukuliwa vipengele vichache sana katika marupurupu ya mbunge, hivyo si sahihi kusema kuwa Dk. Slaa alipwa sawa na mbunge.

Mkurugenzi huo yalisema vipengele hivyo ni mshahara wake Sh. 1,725,000, wakati mbunge analipwa Sh. 2,305,000 kabla ya kukatwa kodi.

Komu alisema kiongozi huyo analipwa mafuta ya kwenda ofisini na kurudi nyumbani kwake lita 30 kwa siku, sawa na lita 900 kwa mwezi; kwa bei ya kila lita moja Sh. 2000.

Wakati mbunge analipwa lita 1,000 kwa mwezi kwa bei ya kila lita moja Sh. 2,500, bei ambayo haipo, lakini Bunge limeridhia kulipa.

Alisema sekretarieti ya Kamati Kuu ilipeleka pendekezo hilo katika vikao vya Kamati Kuu na Baraza Kuu kupitishwa kwa njia ya uwazi na likaingizwa katika mpango kazi wa chama.

"Wakati wote wa kujadili pendekezo hilo, Dk. Slaa aliachia nafasi yake na kikao kiliendeshwa na katibu wa Wanawake, Dk. Naomi Kaihula, ambaye ni mbunge wa Viti Maalum kutoka Mbeya," ilisema.

Alisema mbunge akikaa katika kikao cha Kamati ya Bunge au akihudhuria mkutano wa Bunge analipwa Sh. 70,000 kama posho ya kikao, Sh. 30,000 posho ya mafuta na Sh. 80,000 posho ya kujikumu akiwa Dodoma.

Na akiwa Dar es Salaam, mbunge analipwa Sh. 50,000 kama posho ya mafuta, Sh. 70,000 posho ya kikao na Sh. 80,000 kama posho ya kujikimu huku fedha hizo zikilipwa bila kujali kama mbunge huyu amekuja na gari lake Dar es Salaam na amekwenda nalo Dodoma.

Akahoji: "Mbona hakuna mtu alishawahi kuuliza wakati hizo zote ni fedha za umma?"

Alihitimisha kwamba Dk. Slaa anastahili kulipwa kiasi hicho kwa kuwa aliombwa na chama kugombea urais, naye kukubali, zaidi kukubaliwa na umma pamoja na wanachama kutokana na ukweli wake katika kazi ya siasa.

"Baada ya kukubaliwa na umma, alionyesha umakini, umahiri na uwezo wa hali ya juu katika kujenga hoja zenye tija kwa taifa, na kwamba Dk. Slaa alithibitisha na bado anaendelea kuthibitisha kuwa yeye ni kiongozi bora na shupavu anayestahili kulipwa mshahara mzuri," alisema Komu.

Alisema matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, ambapo Dk. Slaa alikuwa mgombea wao wa urais yanathibitisha kuwa hata bila kuzingatia uchakachuaji wa kura, ameanzisha ukurasa mpya wa mwisho wa mwanzo wa zama za mwisho wa CCM.

Akifafanua kuhusu tuhuma za Mbowe kuhusu kuuzia chama magari chakavu, alisema CHADEMA ndiyo iliomba kuuziwa hicho wanachoita "magari chakavu."
Alisema hayo si magari ya kawaida na hayawezi kufananishwa kwa kiwango chochote na magari ya FUSO yanayotembea mitaani, na kwamba hiyo ni mitambo maalumu ya uenezi wa siasa.

Alisema katika magari hayo kuna vipaza sauti vyenye thamani ya dola za Marekani 148,000 sawa na Sh. milioni 222, jenereta tatu zilizonunuliwa kwa Sh. milioni 47 kwa kila gari kwamba yana bodi maalumu yenye uwezo wa kubeba watu wasiopungua 12.

Pia alisema magari hayo kila moja lina uwezo wa kubeba mapipa ya mafuta ya helikopta, jukwaa la kuhutubia na vifaa vya matangazo ambavyo vyote vimejengwa kwa Sh. milioni 48.4.

Alisema Mbowe aliombwa, na kamati kuu iliunda kamati ya watu wanne chini ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Mohammed Issa kumwomba akiachie chama mitambo hiyo baada ya majadiliano marefu.

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo, waliobariki kuwa ni Mabere Marando, Mkurugenzi wa Rasilimali, Suzan Lyimo (MB) na Anthony Komu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.

Aidha Komu alisema dai la CHADEMA kwamba inanunua magari chakavu si jipya kwao, kwani inao uwezo mdogo wa kifedha na kwamba imezoea kununua magari chakavu siku zote Japani na Uarabuni.

"Kwanza magari yanayozungumziwa chakavu yamenunuliwa nje na kuanzia kazi CHADEMA mpaka leo, na hayajawahi kutumiwa na Mbowe," alisema
Alisema kama CHADEMA imeweza kuweka wazi hoja walizozielekeza kwao, ni vema na wao wakawaeleza Watanzania fedha walizozitumia katika uchaguzi mkuu na mshahara wa Katibu Mkuu wao Mukama, badala ya kukwepa hoja za msingi.

"Tunasisitiza kuwa CHADEMA imeweka wazi malipo ya viongozi wake, gharama za uchaguzi na vyanzo vyake vya mapato na jinsi inavyotumia mapato yake...tunaitaka CCM nayo iweke wazi malipo ya viongozi wake wakuu, gharama za uchaguzi na vyanzo vya mapato yake," alisema.

Alisisitiza kwamba CCM ni chama cha kifisadi kwa kuwa viongozi wake ni mafisadi, wanafiki na wasio wa kweli kwa kuwa walikiri wenyewe katika hicho wanachoita kujivua gamba kuwa katika siku 90 wanachana na mafisadi.

Alisema CHADEMA wanataka kuona hilo likifanyika bila visingizio na kuelekeza mashambulizi kwa Nape hana hadhi ya kuinyoshe akidole chama kwa kuwa si mtu makini mwenye agenda kwa watanzania.

Na kwamba Nape anatakiwa kuonwa na watanzania ama kuitwa vuvuzela anayecheza ngoma asiyoijua na kwamba ni mnafiki, mzushi na mtu asiye na msimamo.

Komu alisema CHADEMA inao ushahidi wa kutosha kuwa ni mmoja wa watu walionufaika na fedha za wizi wa EPA kupitia kwa kwa Jeetu Patel ambaye ameeleza vizuri jambo hili katika maelezo yake mbele ya kamati ya rais kwamba alitumia fedha hizo katika kampeni zake.

Komu alisema hivi sasa Nape analipwa mshahara wa ukuu wa wilaya na huku akilipwa na CCM na kutumia fedha za serikali kufanya kazi za CCM.

Alienda mbali zaidi na kusema kwamba baada ya kushindwa kupata nafasi ya kugombea Ubunge kupitia CCM aliomba agombee kupitia CHADEMA akakataliwa kwa kuwa hakuwa na sifa za kumzidi John Mnyika.

Mbali na hilo alisema pia ni mmoja wa waasisi wa chama cha CCJ na kuhoji iweje leo awe na ubavu wa kuionyeshea kidole CHADEMA?

Aidha alisema yeye (Nape) ndiye aliyetumwa CCM kuiwakilisha katika Mkutano Mkuu wa CHADEMA 2010 na kukisifia chama hicho: "CHADEMA inaenda vizuri kama taasisi na kwa hoja."

Katika hatua nyingine madiwani wa CHADEMA katika manispaa ya Kinondoni wanatarajia kuuelezea umma sababu ya kuibuka kwa vurugu katika baraza la bajeti la 2011/ 2012 lililoketi hivi karibuni.

Licha ya kuuelezea umma pia wanajipanga kutoa tamko juu ya kukiukwa kwa sheria na kanuni na baraza hilo kuamua kupitisha bajeti isiyokuwa na tija kwa wananchi.

Wakizungumza jana na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti madiwani hao walisema kuwa umma unapaswa kufahamu yale yaliyojitokeza ndani ya baraza hilo ambapo bila kuweka jitihada za pamoja kuna uwezekano kata zinazoshikiliwa na wapinzani kushindwa kupata maendeleo.

Diwani wa Saranga Ephraim Kinyafu alisema kuwa bajeti hiyo imejaa uozo huku wakiacha kuweka kipaumbele katika masuala ya maendeleo.

Alisema ili kuondoa dhana ya madiwani wa chadema ni wakorofi suala hilo linatarajiwa kufikisha kwa wananchi na kuwafafanulia suala la milioni 95 kutumika kwa ajili ya ulinzi wa mkurugenzi wa manispaa hiyo.

"Hata kama wameipitisha bajeti hiyo…tunaamini wananchi watakuwa waamuzi wetu tutawafahamisha sababu za sisi kuipinga bajeti maana haiwezekani mavazi ya madiwani yatengewe sh milioni 100 hizo fedha ni nyingi zipoelekwe katika miradi ya maendeleo," alisema.

Alieleza kuwa iwapo manispaa hiyo ingeweza kuongozwa na chama hicho basi wanahakiki wangepiga hatua kubwa katika maendeleo kuliko ilivyo hivi sasa masuala ya anasa yanapewa kipaumbele.

Alifafanua kuwa imeshangaza kuona kuwa kata kubwa kama ya ubungo kushindwa kupewa miradi jambo ambalo linaashiria kuwa viongozi wa eneo hilo waonekane kwa wananchi kuwa hawawezi kuwajibika.

Diwani wa Viti Maalum Kata ya Kawe, Esther Samanya alisema kuwa si kwamba madiwani walipanga kufanya vurugu bali walikuwa wakipigania maendeleo kwani haifurahishi kuona thamani za ofisi zikitengewa fedha huku miradi ya maendeleo ikipewa kisogo.

Alisema pamoja na kujitokeza kwa masuala hayo bado madiwani wa chama hicho wamepanga kutoa tamko na kupinga bajeti hiyo ambayo haina tija kwa wananchi.

"Hivi kweli viongozi makini wanaweza kuacha kuwapigania wananchi na wakasimama kwa ajili ya kutetea watumishi wa idara ambapo wanalipiwa maji na umeme wakati jukumu hilo si la manispaa,"alihoji.

Bajeti ya mwaka wa fedha 2011/ 2012 ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilielezwa kuwa ya kifisadi, hali iliyosababisha kutokea kwa vurugu baada ya madiwani wa CHADEMA kuamua kuipinga.

Kikao hicho kilitanguliwa na vikao vya siku tano vya kamati za kudumu za madiwani wa Manispaa ya Kinondoni lakini katika hatua ya upitishaji wa bajeti hiyo, mabishano makali yaliibuka baada ya madiwani wa CHADEMA kuipinga bajeti hiyo wakieleza kuwa vipaumbele havijazingatiwa kwenye baadhi ya kata, huku wale wa CCM ambao ni wengi wakiiunga mkono.

Madiwani hao wa CHADEMA pia walihoji kiasi cha zaidi ya sh milioni 44 kuwekwa katika bajeti ya manispaa kwa ajili ya kuandaa ilani ya uchaguzi wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani, hali ambayo ilisababisha mvutano mkali kwa madiwani wa CHADEMA na CCM.

Mvutano huo wa madiwani baina ya pande mbili ulisababisha baadhi ya madiwani kuchana hansard za bajeti wakidai kuwa bajeti ni ya kihuni na isiyokuwa na masilahi kwa ajili ya wananchi kuweza kupata maendeleo.

0 comments

Post a Comment