IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitakubali kupokea barabara ambazo zimejengwa chini ya kiwango na makandarasi na kuitaka Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inawachukulia hatua watendaji ambao wamekuwa wakizisimamia.
Rais Kikwete alisema hayo wakati akifungua ujenzi wa Barabara ya Usagara-Geita yenye urefu wa kilomita 90 iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh78 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Alisema kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ni nyingi mno na kutaka ujenzi huo uendane na thamani ya fedha ambazo zinatolewa.Alisema barabara zote zilizo chini ya kiwango zisipokelewe na kwamba atashangazwa sana na maofisa wa Wizara ya Ujenzi ambao watakataa kupokea barabara hizo kwa kuwa kazi yao ni kuzikagua wakati ujenzi ukiendelea.
Alisema kuwa katika kipindi chake cha Awamu ya Pili, Serikali itaanzisha Mfuko wa Barabara ili kuendeleza shughuli za ujenzi kwa ufanisi zaidi.Rais Kikwete alisema kuwa mfuko huo utakuwa na jukumu la kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara barabara zote za mikoa na barabara kuu ili ziweze kudumu kwa muda mrefu .
Akizungumzia madeni ya makandarasi wanaodai Serikali, Rais Kikwete alisema kuwa wakandarasi wote wanatarajiwa kuanza kulipwa fedha zao katika bajeti ya mwaka huu.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema kuwa ili kukabiliana na ubabaishaji wa wakandarasi, wizara yake imeamua kukaa eneo la ujenzi ndani ya miaka mitatu badala ya mwaka mmoja kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Alisema kuwa maamuzi hayo yalifikiwa baada ya kugundulika kuwa baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakijenga barabara kwa kiwango cha chini na kuzikabidhi Serikali baada ya mwaka mmoja zinaanza kuharibika.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - JK: Serikali haitokubali kupokea barabara mbovu
0 comments