IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inakusudia kutumia Sh 613 bilioni kwa mwaka wa fedha 2011-2012 huku kipaumbele kikiwekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya jamii na kupunguza umaskini.
Akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2011/12, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema Serikali haitapandisha kodi yoyote katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.
“Kwa mwaka wa fedha 2011/12 serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote. Inakusudia kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vyanzo vilivyopo na kuziba mianya,” alisema.
Aliahidi kuimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vyanzo vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.
Mzee alisema Serikali inakusudia kuimarisha huduma za utumishi wa umma ikiwemo maslahi bora na katika mipango hiyo, inakusudia kuongeza mishahara kwa watumishi wake katika mwaka huu wa fedha baada ya kufanyika kwa mapitio na mapendekezo mapya kwa watumishi wa Serikali.
Alisema viwango vipya na taratibu zake zitatolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kwamba viwango vipya vimezingatia vigezo vya elimu alivyonavyo mtumishi pamoja na uzoefu wa kazi.
Mzee aliwaambia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba SMZ imekusudia kuimarisha zao la karafuu ili kulifanya kuwa tegemeo kwa taifa pamoja na wakulima kwa ujumla.
Alisema kiwango cha usafirishaji wa zao hilo kimeshuka kutoka tani 2,900 mwaka jana hadi kufikia tani 2,000, wakati bei iliongezeka katika soko la dunia kutoka Dola za Marekani 3,559.8 kwa tani na kufikia Dola 3,591.4.
Mikakati inayokusudiwa kuimarisha zao hilo ambalo katika miaka ya 1970 Zanzibar iliongoza katika soko la dunia ni pamoja na kupanda mikarafuu mipya ni kuwatafutia soko la uhakika wakulima kazi ambayo itafanywa na Wizara za Kilimo, Biashara na ile ya Fedha.
Alisema SMZ inakusudia kuimarisha kilimo cha mwani ili kiwe mkombozi kwa wananchi tofauti na ilivyo sasa ambapo uzalishaji umeshuka kutoka Dola za Marekani 264.4 kwa tani mwaka 2010 hadi kufikia Dola 255.7 mwaka huu.
SMZ pia inatarajia kutumia Sh613.08 bilioni kati ya hizo mapato ya ndani yanakadiriwa kufikia Sh221.24 bilioni wakati ruzuku pamoja na mikopo kutokana na misaada ya washirika ya maendeleo ni Sh340.96 bilioni.
Waziri huyo alisema bajeti ya mwaka huu imelenga katika mwelekeo wa uchumi wa Dira ya Maendeleo 2020, Mpango wa Kukuza Uchumi Zanzibar (Mkuza-II) pamoja na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika juhudi za kuongeza na kuimarisha mapato, alisema mwaka ujao, Serikali itaanza kupokea marejesho ya kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa wafanyakazi wa taasisi za Muungano wanaofanya kazi Zanzibar, hatua ambayo imetokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali zote mbili.
Waziri huyo alisema serikali imeweka kipaumbele katika mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na kutoa mikopo nafuu kwa wananchi kwa lengo la kupunguza umaskini.
Alisema serikali inakusudia kukusanya Sh221.24 bilioni katika vyanzo vyake mbalimbali vya mapato vya ndani na Sh10.22 bilioni kutoka katika vyanzo vya kodi na Sh11.02 bilioni vyanzo visivyokuwa vya kodi.
Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inakusudia kukusanya Sh100.58 bilioni wakati Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inakusudia kukusanya Sh120.66 bilioni.
Mzee alisema SMZ imepata Msaada wa Wahisani katika Bajeti (GBS) wa Sh30.28 bilioni ikiwa ni asilimia 4.5 ya misaada ya kibajeti kupitia Serikali ya Muungano.
Mzee alisema SMZ inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Muungano ili kuondoa suala la mafuta katika mambo yaliyo katika orodha ya Muungano akisema hivi sasa ipo katika mipango yake ya kuchimba mafuta na gesi kama ilivyopanga awali.
“SMZ inaendelea na mipango yake ya kuchimba mafuta na gesi pamoja na kuwasiliana na Serikali ya Muungano kuliondosha suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano na serikali inaendelea na mipangop yake kama ilivyopangwa awali,” alisema Mzee na kushangiliwa na wajumbe wote.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Waziri huyo alisema mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na utulivu uliopo ambao alisema unahitaji kuendelezwa kwa nguvu zote ili Zanzibar ipige hatua za kimaendeleo.
Alisema kutokana na hatua hiyo, washiriki wa maendeleo wameonyesha nia ya kusaidia huku wawekezaji wakipiga hodi kutaka kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kiuchumi.
“Hapa natoa ombi maalumu kwa wananchi wa Zanzibar kwamba hii amani tuliyonayo kwa sasa tunalazimika kuienzi kwa nguvu zote kwani imejenga misingi ya mapenzi na amani na nchi wafadhili wamepata moyo sana kutusaidia, wameonyesha nia ya kutusaidia kutokana na hali ilivyo sasa, hatuna budi kuendeleza nchi yetu ili tufikie maendeleo tunayoyataka,” alisema Mzee.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bajeti: Zanzibar hakuna ongezeko la kodi
0 comments