Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - CCM Arusha hali sasa ni mbaya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter HALI ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Arusha, imezidi kuchafuka na sasa Umoja wa Vijana wa chama hicho, unawataka baadhi ya viongozi wa mkoa wajiuluzu.

Wanaotakiwa kujiuzulu ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Onesmo Ole Nangole na Mwenyekiti wa Mkoa wa UVCCM, James Ole Millya.Tamko rasmi la kundi la UVCCM mkoani Arusha, lililosomwa mbele ya waandishi wa habari jana, pia iliwataka viongozi wote wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wakufuzwe kwa maslahi ya CCM na taifa kwa julma.

"Tunapongeza na kuiinga mkono Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa kutambua kwamba mafisadi wamechangia kukidhoofisha na kukipotezea mvuto chama chetu mbele ya umma. Kwa mantiki hiyo tunatamka kwa kauli moja kwamba...wafukuzwe mara moja," lilisema tamko hilo lililosomwa na Ally Said Babu.

Babu ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM  katika Wilaya ya Arusha, alisema UVCCM pia inamuonya Mbunge wa Viti Maalumu  katika Mkoa wa Arusha kupitia tiketi ya  vijana, asitumike kuwagawa vijana wa mkoa huo vinginevyo, kanuni za jumuiya hiyo zitatumika kumsimamisha.

Tamko hilo la kurasa tatu, pia limemtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Arusha, Ally Bananga, kuacha kutumia jukwaa la vijana kuwatetea mafisadi. "Tunapenda kuujulisha umma kuwa Ally Bananga hana nafasi yoyote ndani ya umoja wa vijana wa CCM kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa. Kwa mantiki hiyo aache mara moja kuganga njaa kwa kutumia jina la UVCCM,"ilisema taarifa hiyo.

Hata hivyo tamko hilo limewataja Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda na mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Mrisho Gambo, kuwa ni viongozi shupavu, wachapa kazi na wanaojali maslahi ya chama.

Viongozi hao wametakiwa wasibabaishwe kwa kauli au shinikizo zinazowataka kujiondoa katika nyadhifa zao."CCM taifa wamwache Chatanda aendelee kuwa Katibu wa Mkoa wa Arusha, ni mpiganaji na lulu ya CCM. Tunatamka rasmi kumtambua ndugu Mrisho Gambo kuwa ni mjumbe halali wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa akiwakilisha Mkoa wa Arusha. Tunaunga mkono ujasiri, umahiri na uzalendo wake katika kupambana na ufisadi ndani na nje chama," lilisema tamko hilo.


Katika mkutano wa waandishi wa habari jana, vijana watano waliodai kushiriki katika maandano ya kumtaka Chatanda ajiuzulu, walirejesha fedha tasmili Sh50,000 walizodai kupewa ili kushiriki katika maandamano hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu kuhusu tuhuma dhidi yao, Nangole, Millya na Magige walikanusha madai yote dhidi yao na kudai kuwa waliozitoa, ni kundi la wahuni waliokusanywa na watu kwa malengo na maslahi binafsi.

"Najua na nina taarifa kuhusu watu hao ambao si wawakilishi halali wa UVCCM wilaya wala Mkoa wa Arusha... wamekusanywa na wale tunaowatuhumu kuhujumu chama kwenye uchaguzi mkuu uliopita. UVCCM ina uongozi na vikao vyake halali vya kujadili na kutoa maamuzi, walete hoja kwenye vikao. Wasizungumze vichochoroni," alisema Millya .

Mwenyekiti huyo wa vijana alisema hajui sababu za shinikizo la kumtaka ajiuzulu lije katika kipindi hiki anachoongoza kampeni ya kutaka katibu wa mkoa, aondolewe kwa tuhuma za kuhujumu kampeni za CCM, katika  Jimbo la Arusha Mjini.

Hata hivyo alisisitiza kuwa Chatanda lazima ang'oke na uamuzi wa kumsimamisha Gambo unabaki pale pale."Kama wanamtambua Gambo mimi siwazuii kufanya hivyo, wakae naye huko vichochoroni. Laini sisi kama UVCCM Mkoa wa Arusha hatumtambui na huu ni uamuzi wa vikao halali visivyoweza  kubatilishwa na mtu au kundi la watu wenye maslahi binafsi," alisema Millya.

Kwa upande wake, Ole Nangole alisema tuhuma na shikizo ni za vichochoroni na kwamba hazimnyimi usingizi.Mbunge Magige yeye alielezea kushangazwa kwake kuhusu tuhuma dhidi yake na kusisitiza kuwa  amekuwa akitekeleza majukumu yake  bila kubagua wala kutenga kundi lolote.

0 comments

Post a Comment