Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mipango Miji yambana Spika afungue barabara

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MWENYEKITI wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira Manispaa ya Kinondoni, Abbas Tarimba ametaka barabara iliyofungwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda ifunguliwe akisema hakuna mwenye mamlaka ya kujenga juu ya barabara.
Akizungumza baada ya kikao cha kamati hiyo kilichofanyika juzi, Tarimba alisema siyo sahihi kwa barabara hiyo inayounganisha eneo la Kijitonyama na Sinza kufungwa.

“Unaweza kuifunga barabara kwa muda tu, ama kwa kuwa unajenga au kuna tatizo la kijamii kama vile msiba au kitu kingine cha namna hiyo,” alisema Tarimba akisisitiza kuwa hata mambo ya namna hiyo yana taratibu zake.
Tarimba alisema hakuna mtu ambaye ana mamlaka ya kuifunga barabara moja kwa moja kisha akafanya ujenzi katika eneo hilo la njia.

Alisema ingawa suala hilo halikuwa ajenda ya kikao cha kamati yake, walilijadili baada ya kuwasilishwa na Diwani wa Kata hiyo, Ulole Juma Athuman.

licha ya kusema kwamba kitendo cha kuifunga barabara hakikuwa sahihi, alimtaka diwani huyo kuwa na subira huku akimsihi kutoitisha mkutano wa wananchi kama alivyoahidi.

“Najua anataka kutumia ile ‘people’s power’ (nguvu ya umma) lakini nimemtaka awe na subira kwanza wakati suala hilo linashughulikiwa,” alisema Tarimba.hata hivyo, Diwani huyo alisema kuwa dhamira yake iko palepale huku akitangaza kuitisha mkutano wa wakazi wa eneo Jumapili jirani na eneo la tukio.

Alisema amechukua hatua hiyo kwa kuwa kinachoonekana ni kutupiana mpira baina ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Manispaa ya Kinondoni, huku wananchi wanaoendelea kupata adha wakidai majibu kutoka kwake. “Walinituma kulalamikia hali ya kufungwa kwa barabara hiyo, nimeleta malalamiko kunakohusika. Hatua za maana zisipochukuliwa, nalirudisha jambo hili kwao waamue,” alisema Ulole.

Diwani alisema haoni sababu ya kuendelea kusubiri wakati sheria na taratibu zipo wazi:
“Hivi kama ningekuwa mimi ndiye nimeziba barabara, hadi sasa wangekuwa wanajadili kweli jambo hilo?” Alihoji na kuongeza kuwa anarudisha majibu kwa mabosi wake ambao ni wananchi siku hiyo ya Jumapili.

Alisema kwamba wananchi wanaitafsiri hatua ya kufungwa kwa barabara hiyo kama ni kuporwa kipande cha ardhi ya barabara na kugeuza kuwa ni sehemu ya kiwanja cha kiongozi huyo jambo ambalo linawapa adha kubwa wakazi wa eneo hilo na lile la jirani.

“Safari ya dakika tano kutoka Kijitonyama kwenda Sinza leo unaifanya kwa dakika zaidi ya 45, kisa! Barabara imefungwa na mtu mmoja kwa matakwa yake. Hiyo haiwezekani,” alisema.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusufu Mwenda alisema kuwa suala hilo limeshatoka kwake na lipo mikononi mwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema juzi kuwa baada ya ofisi yake ilichunguza sababu za kiusalama ambazo zimetajwa kuchangia kufungwa kwa barabara hiyo, ilibaini kuwa hazipo.

“Nilijaribu kuwasiliana na ngazi za juu kidogo pengine kulikuwa na maagizo yoyote ya kiusalama, lakini hakuna kitu kama hicho hivyo suala hilo wanalo wenyewe manispaa,” alisema Rugimbana.Spika alifunga barabara hiyo inayopita jirani na nyumba anayojenga katika kiwanja namba 630 Kitalu 47, mnamo Mei 13, mwaka huu kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni za kiusalama.

0 comments

Post a Comment