Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Vigogo wanaoichafua CCM kulimwa barua

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Katibu Mkuu mpya wa CCM Mh. Wilson Mukama
HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemuagiza Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama, kuwaandikia barua viongozi wanaotakiwa kujiuzulu kuwafahamisha kwamba, kama hawatafanya hivyo kikao kijacho cha NEC kitawafuta uongozi.

Watuhumiwa hao wa rushwa na ufisadi wakiwemo wajumbe wa NEC taifa, wamepewa muda wapime uzito wa tuhuma zinazowakabili, wajiuzulu.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, amesema NEC imeamua kubadili muonekano wa viongozi wake hivyo watuhumiwa wa rushwa, wabinafsi, waliojilimbikizia mali, na wanaojitafutia umaarufu watawajibishwa ipasavyo.

“Tulisema tuwape muda, wao wenyewe, watafakari, wajipime, wajiuzulu… lakini wasipofanya hivyo, chama kitatoa maamuzi ya kuwawajibisha chenyewe” amesema Msekwa mjini Dodoma wakati wa mkutano wa kuwatambulisha wajumbe wa sekretarieti akiwemo Katibu Mkuu, Wilson Mukama.

Kwa mujibu wa Msekwa, ufisadi umeathiri taswira ya CCM, na kwamba chama hicho kilifanya kosa la kuwakubali wafanyabiashara wasio waaminifu katika vikao vya CCM.

“Bado wananchi wengi wanaionyooshea kidole CCM kuwa inakumbatia wala rushwa” amesema Msekwa na kubainisha kwamba rushwa imekuwa ni mzigo mkubwa sana katika chama hicho.

“CCM imepoteza sifa yake ya awali ya kuwa ni chama kinachojali maslahi ya wanyonge na sasa inabebeshwa mzigo wa kuwa ni chama cha matajiri”amesema Msekwa.

Amesema, CCM imejivua gamba, kimekuwa chama kipya, na kwamba jogoo amewika hivyo waamke. Msekwa amesema, maamuzi ya NEC CCM ilikuwa ni utekelezaji wa kufanya mageuzi ndani ya chama hicho kwa kujivua gamba mithili ya nyoka.

Kwa mujibu wa Msekwa, NEC ilifanya maamuzi katika maeneo manne ikiwa ni pamoja kna kufanya mageuzi ya kuiwezesha CCM kupambana na ukoloni mamboleo unaoathiri siasa za nchi yetu.

Amesema, CCM imefana mageuzi ya kubadilisha muonekano hasi wa chama hicho kwa wananchi, kujipanga upya ili kujiimarisha kishinde uchaguzi, na mageuzi ya kukiwezesha kupambana na maovu ukiwemo ufisadi na rushwa.

Kwa mujibu wa Msekwa, CCM imeamua kusahihisha makosa ya nyuma kwa kubadili masuala mengi ikiwa ni pamoja na kutoteua wagombea wasiokubalika, na pia kitafanya mageuzi ili kuongeza wigo wa kuwa karibu na makundi ya watu.

CCM pia imeamua kubadili utaratibu wa kumpata mgombea wake wa urais ili kuzuia matumizi makubwa ya fedha zinazonunua kura za wajumbe wa vikao vya uchujaji na vya uteuzi wa mwisho katika mchakato huo.

“Makundi ya vinara wanaowania urais yamewagawa wanachama wetu na kuathiri umoja na mshikamano ndani ya chama kwa kiwango kikubwa sana” amesema Msekwa.

“Tatizo hili ni kubwa na lina athari kubwa kwa chama chetu” amesema Msekwa na kubainisha kwamba, CCM pia imesitisha utaratibu wa kutoa kadi za uanachama za papo hapo.

“Tumefanya mageuzi ya kubadilisha utaratibu wa kuingiza wanachama wapya kwa kufanya uamuzi kwamba, chama katika ngazi ya matawi kitenge siku moja maalumu katika mwezi ambapo wanachama wapya watapokea kadi zao kwa sherehe rasmi” amesema.

Kwa mujibu wa Msekwa, CCM pia imebadili salamu yake, mtu akisema ‘ Kidumu Chama Cha Mapinduzi’ unaitikia ‘ Idumu CCM mpya’. CCM pia imebadili utaratibu wa utoaji kadi za uanachama wakati wa kura za maoni.

“Tumefanya mageuzi ya kuweka muda wa mwisho wa utoaji wa kadi za wanachama kwa ajili ya upigaji kura za maoni uwe tarehe 31 Desemba ya mwaka unaotangulia mwaka wa uchaguzi mkuu husika” amesema Msekwa na kuongeza kuwa, CCM pia imebadili utaratibu wa uchaguzi wa chama na jumuiya zake

“Kuanzia sasa tutakuwa tunafanya uchaguzi wa chama na jumuiya zake katika mwaka mmoja” amesema na kubainisha kwamba, uamuzi huo utaiwezesha CCM kupata muda wa kutosha wa kufanya kazi za chama ndani ya chama na kwa umma.

Amesema, CCM pia imebadili utaratibu wa uteuzi wa wagombea wa CCM wa ubunge na udiwani, na kuanzia sasa watachujwa ili kupata wagombea wasiozidi watatu ambao watapigiwa kura za maoni.

Msekwa amesema, CCM pia itaangalia uwezekano wa kuanzisha viwango vya ada vinavyotofautiana kulingana na kipato cha wanachama, kampuni za chama hicho ambazo hazifanyi kazi vizuri zitafutwa, na pia chama kitaangalia uwezekano wa kuuza baadhi ya mali zake ili kiwekeze kwenye miradi yenye tija.

0 comments

Post a Comment