Wanajeshi wa Uholanzi waondoka Afghanistan leo
Wanajeshi wa Uholanzi waliokuwa wakitumika katika kikosi cha kimataifa cha kulinda amani nchini Afghanistan, ISAF, wanaondoka leo nchini humo baada ya miaka minne, kufuatia mzozo wa kisiasa nchini Uholanzi. Kuondoka kwa wanajeshi hao ni hatua ya kwanza ya kuanza kuondoka vikosi vya kimataifa vinavyopigana vita nchini Afghanistan, ambayo viko katika mwaka wake wa tisa, na kunafanyika baada ya upinzani wa wanamgambo wa Taliban kuzidi kufikia kiwango kibaya zaidi. Kunafanyika pia wakati Marekani ikiwa imeshuhudia mwetzi mbaya zaidi kwa kupoteza idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wake. Afisa wa ubalozi wa Uholanzi mjini Kabul amesema sherehe ndogo ya kukabidhi madaraka na kuwaaga wanajeshi hao, imefanyika katika kambi ya kijeshi iliyoko katikati mwa mkoa wa Uruzgan ambako wanajeshi 1,950 wa Uholanzi wamekuwa wakitumika katika shughuli za kulinda amani. Kikosi cha ISAF ambacho kilikuwa kimeitaka Uholanzi kurefusha muda wa wanajeshi kuednelea kuwepo Afghanistan kwa mwaka mmoja, kimeupongeza mchango uliotolewa na wanajeshi wa Uholanzi na kuahidi kuendelea kupiga doria katika eneo walikokuwa wakitumika. Nafasi yao itachukuliwa na vikosi vya Marekani, Australia, Slovakia na Singapore.
Wakati huo huo, watu zaidi ya 400 wameandamana kuelekea ikulu ya rais mjini Kabul kulalamikia mauaji ya raia 52 waliouwawa kwenye shambulio la roketi la jeshi la Jumuiya ya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO kusini mwa Afghanistan. Jumuiya ya NATO imekanusha ripoti za kuuliwa raia kwenye shambulio hilo. Wajumbe wa jumuiya hiyo na wale wa serikali ya Afghanistan wanafanya uchunguzi wa pamoja kutafuta ukweli halisi wa shambulio hili lililofanywa katika wilya ya Sangin mkoani Helmand. Waandamanaji wa mjini Kabul wamesema wanaamini jumuiya ya NATO ina hatia katika mauaji hayo ya raia. Walibeba picha za watoto waliojeruhiwa au kuuwawa kwenye shambulio hilo na kupiga kelele kuilaani Marekani na jumuiya ya NATO. Waandamanaji hao hawakufanya fujo na walilindwa na maafisa wa polisi wa Afghanistan ambao walizifunga barabara kuwawezesha kufanya maandamano yao kwa amani.
0 comments