Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Profesa Mkandala kujieleza kwa kushindwa kutaja mali zake

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Profesa  Rwekaza  Mukandala  (katikati)

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala jana alishindwa kufika mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa  Umma, lililokaa kusikiliza mashauri ya viongozi walioshindwa kutangaza mali zao.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu,Damian Lubuva, alisema kwa mujibu wa ratiba, Profesa Mukandala alitakiwa kufika mbele ya baraza hilo jana.Jaji Lubuva alisema juzi Profesa Mukandala alimpigia simu kumweleza kwamba asingeweza kufika mbele ya baraza hilo kama ilivyopangwa kwenye ratiba kwa kuwa ana shughuli maalum.

"Kutokana na hali hiyo, sasa tumempangia siku ya Jumatatu ijayo ili atafika mbele ya baraza," alisema Jaji Lubuva.
Profesa Mukandala na viongozi wengine wanadaiwa kushindwa kuwasilisha fomu katika Sekretarieti ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, zinazoonyesha mali wanazozimiki kwa mujibu wa sheria.

Waliofika jana mbele ya baraza hilo ni Diwani wa Kata ya Mondo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, John Ndama na Rose Komba ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda.Wengine ni Thecisius Malulefu ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo wa Mbulu na Adam Materu, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo katika Wilaya ya Mpanda.

Katika utetezi wao, madiwani wote wawili walikiri kupokea fomu, kuzijaza na kuzirejesha katika sekretarieti kupitia kwa wakurugenzi wa halmashauri zao."Nilipewa fomu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu, nikajaza na kumrejeshea kama taratibu zetu zinavyosema lakini nimeshangaa kwamba hazikufika," alisema.

Diwani wa Viti Maalumu katika Halmashauri ya  Wilaya ya Mpanda, Komba alisema huo ni utaratibu wao kupitishia fomu kwa mkurugenzi mtendaji."Sasa kama hazikufika fomu kwenu nani alaumiwe wakati niliziwasilisha kwa mkurugenzi mtendaji," alihoji Komba.

Kufuatia kauli hiyo wanasheria waliomba uthibitisho unaoonyesha kwamba waliwasilisha fomu hizo, lakini hawakuthibitisha.Hadi gazeti hili linaondoka katika viwanja vya Karimjee saa 7.00 mchana, viongozi wengine walikuwa wakiendelea kuhojiwa na baraza hilo.

0 comments

Post a Comment