Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Zitto amshangaa Pinda kutojua ubadhirifu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe amesema anasikitishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokuwa na taarifa za ubadhirifu mkubwa wa fedha za Mfuko wa Kuhuisha Uchumi.
Taarifa ya Zitto aliyotoa kwa vyombo vya habari jana, inasema hatua ya Pinda kuonyesha kwamba hana taarifa za upotevu wa Sh48 bilioni, inaonyesha kuwa Serikali haipo makini katika kusimamia fedha za umma.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, alitoa taarifa hiyo baada ya kutoridhishwa na majibu ya Waziri Mkuu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, kuhusu upotevu wa Sh48 bilioni za mfuko huo ambazo zimeonyeshwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba zimepotea na Pinda kusema hana taarifa hizo.

Taarifa ya CAG inaonyesha upotevu wa Sh48 bilioni kati ya Sh1.7 trilioni zilizotolewa na Serikali. Pia inadaiwa kuwa Serikali ilimnyima majina ya watu na kampuni zilizokopa fedha hizo ili kujua iwapo zilitolewa kwenye taratibu za kawaida.
Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, alimtaka Pinda kutoa taarifa kwa umma mara moja kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha hizo.

“Vilevile Serikali ihakikishe CAG anafanya ukaguzi maalumu kwenye fedha zote za Mfuko wa Kuhuisha Uchumi, ambazo ni takriban Sh1.7 trilioni. Kuna shaka kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili hii zilitumika vibaya, kufujwa na kuibwa. Shaka hii itaondoka iwapo CAG atafanya ukaguzi maalumu.”

Alisema akiwa Waziri kivuli wa Fedha na Uchumi, ataendelea kuhoji suala hilo hadi ukweli utakapobainika na waliofuja fedha hizo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.“Naomba umma wa Watanzania ujue kuwa fedha za mpango huu ni nyingi mno, haiwezekani kuachwa bila kufanyiwa ukaguzi ambao unatakiwa kuwekwa wazi kwa umma,” alisema.

Baada ya kutokea mtikisiko wa uchumi duniani, Serikali ilitenga Sh1.7 trilioni kwa ajili ya kampuni ambazo zilikuwa zimenunua mazao ili kuzinusuru na mtikisiko huo.

Miongoni mwa kampuni zilizopata fedha hizo ni zile zinazonunua pamba ambazo zilitakiwa kutoa fidia ya Sh80 kwa kilo ya pamba ambayo ilikuwa imenunuliwa.Hata hivyo, kwa mujibu wa Mbunge wa Bariadi Magharibi (UDP), John Cheyo hadi sasa wakulima hawajalipwa fidia hiyo.

0 comments

Post a Comment