Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - URAIS 2015 CCM: Waliowekeza NEC walizwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


*Kamati yaundwa kubuni utaratibu mpya wagombea urais
*Yaelezwa wa sasa umejaa rushwa, chanzo cha mgawanyiko



KATIKA mkakati wake wa kujisafisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza utaratibu wa kuvunja nguvu ya mtandao wa
wanaotarajia kugombea urais 2015 waliokuwa wamewekeza kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa kuandaa utaratibu mpya wa kupitisha majina ya wagombea.

Hatua hiyo inatokana na CCM kuunda Kamati Maalumu ya watu sita itakayoangalia mfumo mpya wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho, tofauti na ule wa sasa ambao wamebainisema haufai kwa kuwa unakumbatia rushwa na kusababisha mgawanyiko.

Kwa muda mrefu baadhi ya wanaCCM wenye nia ya kuwania urais wamekuwa wakiandaa safu za uongozi wa chama hicho kuanzia ngazi za chini hadi wajumbe wa NEC ili kujihakikishia uteuzi kwa kuwa walikuwa na sauti kubwa chini ya utaratibu wa zamani.

Akizungumza na Majira jana, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Bw. John Chiligati alisema utaratibu huo ni sehemu ya chama hicho kujivua gamba na kuleta mabadiliko.

"Tumeunda Kamati maalumu kuangalia mfumo mpya wa kumpata mgombea urais, mfumo sasa unashawishi vitendo vya rushwa na mgawanyiko," alisema Bw. Chiligati bila kutaka kuingia kwa undani.

Hatua hiyo ya CCM inawamaliza baadhi ya watu wanaoaminika kutaka urais kwa udi na uvumba kupitia chama hicho, ambao tayari walishatumia mabilioni ya pesa kuweka msingi ndani ya NEC ya sasa kuhakikisha wanafanikiwa kupitishwa 2015.

Kama hatua hiyo haitoshi, Bw. Chligati aliambia Majira kuwa CCM imeamua kuwachagua wajumbe wapya wa NEC kupitia maeneo wanakotoka na si kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa chama hicho mjini Dodoma kama ilivyozoeleka.

"Ule mfumo wa wajumbe wa NEC kuchaguliwa na Mkutano Mkuu Kizota nayo tumeona inasababisha kuwepo kwa picha ya chama chetu kuwa cha watu wenye uwezo wa kufanya kampeni.

Wakati mwinginge inajenga mazingira ya rushwa kule kwa wajumbe, tumeamua mwakani wajumbe wote wa NEC watachaguliwa huko huko kwenye maeneo yao, haya yote ni mabadiliko sawa na kuwaondoa mafisadi," alisema.

Uchunguzi wa Majira ulibaini kuwa Kamati iliyoundwa kimya kimya na chama hicho kupendekeza mabadiliko yanayoendelea sasa ndio iliyokabidhiwa kazi ya kutafuta mfumo mpya kupata wagombea urais.

Kamati hiyo inaelezwa kuwa na msimamo chanya kwa taifa na kwamba ni pigo kubwa kwa mafisadi kwa kuwa haitoi nafasi kwao kupumua kama walivyozoea.

Alisema watu wanaodhani kuwa chama hicho kilifikia hatua ya kuwaondoa wajumbe watatu tu walioagizwa kujiondoa, kutambua kuwa huo ni mwanzo tu na kwamba fagio la mafisadi ndani ya chama hicho itakwenda hadi matiwini.

Alitoboa siri ya kujizulu kwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho wiki iliyopita mjini Dodoma kuwa kulitokana na kuchoshwa na vitendo vya ufisadi walioshuhudia huku wahusika wakiendelea kuwepo.

"Kamati Kuu ilifikia hatua ya kujiuzulu baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo, katika nchi zetu za Kiafrika desturi ya kujiuzulu hasa unapokuwa kwenye nafasi kubwa siyo rahisi. Lakini kwa kuwa wao ndio wakubwa na mambo yaliharibika wakiwamo walimua kutoa mfano.

Unapoona watu wakubwa kama Kamati Kuu walifikia hatua hiyo ilikuwa ni kuonesha mfano na njia kwa watuhumiwa wote kujiondoa wenyewe, wale ambao hawataki wasubiri siku 90 wataondolewa kwa lazima," alisema Chiligati na kuongeza:

"Tayari tuna Orodha kamili ya mikoa, wilaya hadi matawini, fagio la kuwaondoa inaendelea hadi ngazi ya chini kabisa," alisema Bw. Chiligati bila kutaka kutaja majina yao.

Alisema CCM imekuwa na uvumilivu kwa kuwataka watu wajirekebishe huku ikisimamia imani yake ya kusema ukweli daima na kusisitiza kuwa hatua iliyofikiwa sasa inathibitisha hilo.

Akizungumzia ziara yao ya kutambulishwa katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibara alisema mapokezi waliyopata yamewatia moyo na kuwapa picha mpya ambayo hawakutarajia.

"Kutokana na jinsi tulivyopokelewa na wanachama na wananchi kwa ujumla ni wazi kuwa hatua iliyochukuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kule Dodoma ni nzuri na imewatia moyo Watanzania wote," alisema.

Naye Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, alisema kilichofanywa kwa kuwaagiza wajumbe watatu wajiondoa wenyewe NEC kabla ya kupitiwa na fagio la kusafisha chama ni sawa na mtu mzima kuoga.

"Mtu mzima anapooga anaanzia kichwani, huwezi kuanzia kwenye miguu, ila mwisho ni lazima uoge mwili mzima na kumalizia kwa kusugua vizuri miguu yako ndio unakamilisha kuoga kwako," alisema Bw. Nnauye akimaanisha CCM kusafisha mafisadi ngazi zote.

Hata hivyo alioneshwa kushtushwa na baadhi ya vyama vya upinzani kuingilia kati kazi ya chama hicho kudai kujivua gamba na kusisitiza kuwa kazi hiyo waachiwe wenyewe.

0 comments

Post a Comment