Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - ‘Ndiyo’ ya Pinda Ilivyotunisha misuli Upinzani bungeni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MAKOFI mazito mezani, ndicho pekee kilikuwa kiashiria na namna wabunge wa Kambi ya Upinzani bungeni, walivyofarijika, kwa jibu la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipomuunga mkono Mbunge wa Singida Mashariki, wakili machachari, Tundu Lissu (Chadema) hivi karibuni.

Kauli ya Pinda aliyoirudia mara tatu, iliwaacha midomo wazi baadhi ya Wabunge wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wengine wakijilazimisha kuamini kuwa jibu hilo alilitoa kuwatia moyo wapinzani.

Pinda aliunga mkono marekebisho ya kuingiza mapendekezo ya Lissu, kutaka wakuu wa mikoa na wilaya wasiwepo katika Kamati za Maadili za Wilaya za Mahakama, kwa kile alichosimamia kuwa wanateuliwa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, hivyo wakuu hao ni makada wa chama hicho.

Kamati hizo ni zile zinazosimamia maadili ya mahakimu, kama inavyopendekezwa katika kifungu cha 50 cha Muswada wa Sheria ya Utawala wa Mahakama wa mwaka 2011, uliowasilishwa bungeni na Serikali na kupitishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge mjini Dodoma hivi karibuni.

Lissu alitaka kifungu hicho, kirekebishwe kwa kuwaondoa wakuu hao ; na badala yake awepo mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Baada ya Spika, Anne Makinda, kuuliza wanaoafiki marekebisho ya Lissu, waseme ‘Ndiyo’ na wasioafiki waseme ‘hapana’, sauti zilisikika kuwiana. Ndipo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), alipoomba mwongozo wa Spika na kutaka kura za kuulizwa mbunge mmoja mmoja zipigwe.

Spika aliridhia pendekezo la Zitto ; na kura zilianza kupigwa, kwa kuanza kumuuliza Waziri Mkuu, ambaye ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Pinda alipoulizwa, alisema ‘ndiyo’, akionesha kuwa anakubaliana na mapendekezo ya Lissu, kuingizwa katika muswada huo.

Wabunge wa upande wa Upinzani, walishangilia kiasi cha kusababisha Spika, arudie swali kwa Pinda mara tatu, ambapo mara ya tatu Waziri Mkuu, huku akiwa amesimama alisema; “Nimesema Ndiyo” . Jibu hilo liliwaacha mawaziri na wabunge wa CCM, wakishangaa, kutokana na ukweli kwamba walitegemea jibu la ‘siyo’.

Kura hizo za ‘ndiyo’ au ‘hapana’, zilipigwa wakati Bunge lilipokaa kama Kamati, kupitia kifungu kimoja baada ya kingine cha muswada huo wa sheria ya uendeshaji wa Mahakama wa mwaka 2011, unaosubiri sasa rais ausaini, ili uwe Sheria.

Pinda aliposema ‘ndiyo’, Zitto alisimama na kumpongeza. Lakini, ghalfa alisimama Spika Makinda ; na kueleza kuwa hakusikia jibu la Pinda, hivyo alimuuliza tena. Waziri Mkuu alirudia kusema ‘ndiyo’. Jibu hilo liliamsha hisia kwa wabunge wa upinzani, ambao hukaa upande wa kushoto kwa Spika.

Hali hiyo ilisababisha upande wa kulia waliko wabunge wa CCM, ambao ni wengi zaidi, kuduwaa kwa dakika chache.

Nje ya Bunge, Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema jibu la Waziri Mkuu, linadhihirisha kuwa mapendekezo ya Upinzani, yanakubalika na yana msingi, lakini kutokana na uchache wao, yanakosa nguvu ya kusababisha yapite.

Baada ya ‘ndiyo’ ya Pinda, baadhi ya wabunge wa CCM, walisema ‘ndiyo’ lakini walipoulizwa mara ya pili, walisema ‘siyo’, akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu, Angelah Kairuki, anayewakilisha kundi la Wafanyakazi.

Hata hivyo, pamoja na nia njema ya Waziri Mkuu kumuunga mkono Lissu, matokeo ya kura yaliwagaragaza wapinzani, ambapo Spika alipotangaza, alisema waliosema ‘ndiyo’ wakiwa upande wa Lissu akiwemo Pinda ni 69 ;na siyo ni 152, hivyo ushindi kupatikana kwa waliosema ‘siyo’.

Hata hivyo, kura hizo za mmoja mmoja kuulizwa, zilipigwa na wabunge 122 pekee, kati ya wabunge 350 waliopaswa kuwepo bungeni. Spika alionesha kukerwa na idadi ya wabunge 128, kutokuwepo bungeni wakati huo.

Awali, kabla ya wabunge kupiga kura ya pamoja, kwa kusema ‘ndiyo’ au ‘hapana’ na kisha ile ya mmoja mmoja, kulikuwa na mvutano wa vifungu vya sheria, vinavyohusika na muswada huo, baina ya Lissu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.

Mvutano huo ulitokana na mapendekezo ya Lissu ya kutaka kurekebisha vifungu kadhaa, kwenye muswada huo ili sheria inayotungwa iwe na manufaa, kikiwemo kipengele cha Ibara ya 9, kinachoonesha hakuna sababu ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, kuwa na taaluma ya sheria.

Lissu alipendekeza kuwa Ofisa huyo atakayeteuliwa na Rais, sheria itakapoanza kazi, kuwa na taaluma ya sheria ili aweze kuelewa kinagaubaga matakwa ya uendeshaji wa Mahakama. Kipengele hicho kinamtaka awe na taaluma ya Fedha na Uongozi (Utawala). Katika hayo yote, Kombani na Werema walimlalamikia Lissu, kuwa ni mpotoshaji. Hali hiyo iliongeza majibizano.

Lakini, suala hilo liliwekwa sawa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge, ambaye alipofafanua, Lissu alikubaliana naye na mapitio ya kifungu kwa kifungu cha muswada yakaendelea.

Waliosimama na kupinga mapendekezo ya Lissu kwa nyakati tofauti ni pamoja na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Akitoa taarifa kwa Spika, Manyanya alitumia fursa hiyo kusema kuwa Lissu alikuwa akiingiza masuala ya Chadema bungeni, na kwamba Mbunge huyo alikuwa akipoteza muda.

Hoja ya Lissu kuhusu kamati za maadili za Mahakama, ilikuwa ni kuitenga na mikono ya wanasiasa ; na kuzifanya kamati kuwa kama kamati za maadili za madaktari na wahandisi, ambazo zinatokana na watu wa taaluma husika.

“Madaktari wana kamati zao, wahandisi na sisi wabunge hivyo hivyo, kamati hizi zinatokana na sisi wenyewe. Wahusika wanapokosea wanashughulikiwa kimaadili na kamati zenye uelewa wa mambo wanayofanya.

Vipi Mahakama washughulikiwe na wanasiasa? Hii si sawa” , aling’aka Lissu, huku akiwatahadharisha wabunge, kutambua kuwa wanapiga kura kwa mustakabali wa nchi ; na si Chadema, hivyo mamlaka ya kudhibiti nidhamu ya mahakimu, isiende nje ya utumishi wa Mahakama.

Lissu alipendekeza badala ya wakuu wa mikoa na wilaya, kuwepo na mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanzania Bara (TLS) na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) chini ya Msajili wa Mahakama Kuu.

Kwa upande wake, alipopewa nafasi na Spika kuchangia mapendekezo ya Lissu, kuhusu kutengwa kwa kiwango maalumu cha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Mahakama chini ya Kifungu cha 57 cha Muswada, Sitta alisema kuweka kiwango maalumu katika kila bajeti kwa ajili ya Mfuko huo ni jema, lakini wakati wake ni Bunge la Bajeti litakaloanza Juni ; na si hilo la Miswada la Aprili.

Sitta anasema “Lissu ana hoja nzuri sana, lakini asipingane na Katiba ;na wakati mwingine asikilize hoja za wanasheria wazoefu kama mimi, mimi si mtu wa kukurupuka. Suala analosema kikatiba si la kujadili katika Bunge hili, bali la Bajeti, Ibara ya 99 ya Katiba hairuhusu hilo analolitaka”.

Baada ya majibu hayo ya Sitta na majibu ya Lissu, akimtuhumu kuwa amekosea, hivyo ingekuwa bora anyamaze, Lukuvi alifunga mzizi wa fitina, kwa kusema kuwa mapendekezo ya Lissu kuhusu bajeti ya Mahakama ni sahihi.

Ila, Lukuvi alisema fedha kwa ajili ya Mfuko wa Mahakama, zitatengwa kulingana na uwezo wa bajeti ya nchi, kwa kuwa hata wizara na Bunge hawapati fedha kwa mujibu wa mahitaji yao.

Baada ya Bunge kukaa kama Kamati, lilirejea kama Bunge na Spika baada ya kuwahoji wabunge, Muswada uliungwa mkono kuwa Sheria, ambapo baada ya Rais kusaini kutaanzishwa Mfuko wa Mahakama.

0 comments

Post a Comment