Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Wazanzibari wazidi kuchokonoa Muungano

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KUNDI la wazee wanaodai kuwakilisha mikoa mitano ya Zanzibar, limemwandikia Rais Jakaya Kikwete, barua ya malalamiko kuhusu Muungano na kumtaka atimize ahadi zake za kuondoa kero za chombo hicho, kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi wa taifa.

Barua hiyo ya Aprili 21 mwaka huu, imekuja wakati Watanzania leo wanasherehekea miaka 47 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Maadhimisho hayo yatafanyikia katika uwanja wa Aman, mjini Zanzibar.Katika barua hiyo, kundi hilo limeelezea kusikitishwa juu ya kile kilichoelezwa kuwa ni mwendo wa konokono wa Rais Kikwete ,katika kushughulikia ahadi zake za kuzimaliza kero za Muungano.

“Kwa masikitiko makubwa hatuna budi kufikisha kilio chetu kwako wewe rais wetu ambaye upo katika kipindi chako cha pili na cha lala-salama kikatiba, katika kuliongoza taifa hili bila ya mafanikio juu ya ahadi zako ulizotoa kuhusu kuzimaliza kero za Muungano baina ya watu wa Zanzibarna wa Ttanganyika,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo imeongeza kuwa wakati Rais Kikwete alipokwenda visiwani kuomba kura kwa mara ya kwanza mwaka 2005, alipewa ushirikiano pale alipowaahidi Wanzanzibari kwamba, angezipatia ufumbuzi kero zote za Muungano.

Wazee hao, walitaja mambo ambayo Rais Kikwete aliahidi kuyatekeleza alipokuwa akilihutubia Bunge Desemba 30 mwaka  2005 kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa pande zote mbili za  Muungano, zinafaidika na kuridhishwa na Muungano.

Hali kadhalika kukuza demokrasia itakayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.

“Licha rais na serekali yako kushindwa kuyatekeleza mambo makuu matatu uliyoyapa kipaumbele katika awamu yako ya kwanza, lakini pia hukujisikia aibu kuwaeleza Watanzania kupitia  Bunge jipya la kumi  kwamba mambo yale uliyoyaahidi katika Bunge lililopita  bado yataendelea kuwa ndiyo majukumu yako ya msingi katika kipindi chako hiki cha pili,"imesema barua hiyo.

Wamegusia pia viaumbele 13 alivyovitoa Rais Kikwete, alipokuwa akilihutubia Bunge mwishoni mwa mwaka jana, ambavyo ni pamoja na kuwa na nchi yenye umoja, amani, na usalama na muungano ulioimarika.

Walisema hata hivyo vipaumbele hivyo, vinakwamishwa na rasimu ya katiba mpya iliyoandaliwa bila hata kufuata kanuni na sheria za muungano.

“Je, ndio kutaka kuimarisha umoja, amani na usalama wa kweli?  Huu ndio utawala bora, utawala wa sheria wa demokrasia yenye kujali haki za binadamu Au huu ndio mkakati maalum wa kuhakikisha kuwa muungano wetu unaendelea kudumu na kuimarika," ilihoji sehemu ya barua hiyo.

Wazee hao wameunga mkono hatua ya Wazanzibari kuukataa muswada wa marejeo ya katiba na kutoa pongezi kwa wananchi hao.

“Rais, tunakuomba kwa heshima zote wewe na serekali yetu ya muungano; tafadhalini sana sana msikie kilio cha wazanzibari. Tunajua asili na tabia yako wewe si mtu wa pupa, jazba na hamaki. Tabia yako imepambwa na busara, hekima, usikivu na utaratibu, sifa ambazo ni sawa na lulu na ndizo zinazokutofautisha sana  wewe na baadhi ya viongozi waliotangulia,” ilisisitiza barua.

Walisisitiza  Wazanzibari wanataka mabadiliko makubwa ndani ya Muungano, kwa sababu makubaliano ya muungano huu yamekiukwa na hivyo kuweka kasoro kubwa katika uhalali wake.

“Sisi tunaamini kwamba huu ni wakati muafaka na mnasaba wa kuujadili muungano upya. Na baadaye watu wa Zanzibar na watu wa Tanganyika,wapewe fursa ya pekee ya kuulizwa kuhusu Muungano upi wanaoutaka. Majibu yatakayotoka katika pande zote mbili ndiyo yapewe kwa tume ili yafanyiwe kazi inayostahiki." alisema.

Wamekumbushia pia mpango uliokuwepo wakati wa serekali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, ambapo aliyekuwa Waziri mkuu wake, John Malecela alishakamilisha na kulieleza Bunge juu ya nia ya kuwapo kwa muswaada wa kuanzishwa kwa serekali yaTanganyika, lakini baadaye Mwalimu Nyerere alitumia uwezo wa chama na kulilazimisha Bunge lisiujadili.

0 comments

Post a Comment