Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Askofu: Bunge sasa ni kama shule ya msingi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
ASKOFU Mkuu wa Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa amewashukia wabunge kwa tabia yao ya kuzomeana wakati vikao vya Bunge hilo vikiendelea, akisema hali hiyo inawashushia heshima ya uwakilishi wa wananchi waliyonayo.

Pia Askofu huyo ameweka bayana kuwa anachukizwa na kitendo cha mgawo wa umeme na kuitaka Serikali kuacha kuegemea zaidi katika uzalishaji umeme wa maji kwa kuwa ukosefu wa umeme pamoja na kuchangia kurudisha maendeleo, pia ni chanzo cha ukosefu wa amani nchini.

Akizungumza katika Ibada ya Misa ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Albano Dayosisi ya Dar es Salaam, amesema kwa sasa vyombo vingi vya Dola vimekuwa vikitenda mambo kinyume cha taratibu zinazotakiwa, jambo ambalo pamoja na kuvishushia hadhi, pia linachangia kuleta machafuko ya amani.

“Sote tumeshuhudia juzi namna Bunge lilivyopoteza thamani na heshima yake na kuwa kama shule ya msingi, wabunge wanazomeana kama watoto wadogo, natamani Mwalimu Nyerere angekuwa hai….lazima angetembeza mikwaju ndani ya Bunge hili,” alisema Askofu Mokiwa na kuongeza kuwa anampenda Nyerere kwa sifa na uongozi wake.

Kauli ya Askofu Mokiwa imekuja wakati hivi karibuni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kilimtaka Spika wa Bunge kutumia wadhifa wake na Kanuni za Bunge kama rungu ili kulinda heshima bungeni kutokana na tathmini ya Mkutano wa Tatu wa Bunge ambayo imebaini pamoja na mambo mengine, matumizi ya lugha chafu ya wabunge wakati wa vikao vya Bunge.

Aidha, Askofu Mokiwa alisema pamoja na Bunge, pia suala la kukatika mara kwa mara kwa umeme huku sababu zikitolewa kuwa ni ukosefu wa mvua wakati gharama za matumizi ya umeme huo zikipanda kila kukicha, linachukiza na ni kero kubwa kwa Watanzania.

“Jamani mimi ni mdau mkubwa ninayekerwa na tabia hii ya umeme kukatwa bila taarifa halafu ukiuliza eti mvua hazijanyesha, ni upuuzi kuendelea kutegemea maji kama chanzo cha kuzalisha umeme wakati Tanzania ina malighafi nyingi za kuzalishia umeme huo,” alisema.

Askofu Mokiwa pia alikemea tatizo la sasa la udini linalochangiwa na viongozi wenyewe wa dini pamoja na baadhi ya wanasiasa wanaong’ata na kupuliza katika kila dini, hali ambayo aliwataka Watanzania wajihadhari na viongozi wa aina hiyo na kutowasikiliza kwa kuwa mgawanyiko wa dini katika taifa ni hatari.

“Sasa hivi wana dini tunataka kuota pembe, ni kweli tunazo nguvu kubwa katika jamii hatuhitaji polisi wala Katiba, lakini tumeweka mbele ajenda ya kupondana kwa kutumia vyombo vya habari hali inayoleta mgawanyiko kwa Watanzania, pia wapo wanasiasa wanaharibu makanisani na misikitini,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema suala la ufisadi nalo kwa sasa limekuwa tishio kwa amani ya Tanzania kwa kuwa mtu yeyote mwenye mafanikio anapachikwa jina la ufisadi huku akitolea mfano wa viongozi ambao pamoja na mazuri waliofanya, lakini wanaitwa mafisadi kuwa ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Waziri wa Ujenzi John Magufuli, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz.

Alisema iwapo viongozi hao na wengine waliotajwa ni mafisadi Tanzania ni nchi inayoendeshwa kisheria wachukuliwe hatua, lakini kitendo cha kuwataja hadharini bila ushahidi au hatua zozote ni dalili kuwa sasa nchi inaenda pabaya.

Alisema kutokana na mambo mengi yanayoizonga Tanzania na kuhatarisha amani, Mungu amewaona Watanzania na kuwaletea kikombe cha Samunge kinachotolewa na Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwaisapile na kuwataka waumini wa kanisa hilo kwenda Loliondo na kupata tiba hiyo kwa kuwa inaponesha kwa uwezo wa Mungu.

“Sisi kule kwetu Muheza tunachemshiwa ndula na kunywa na tunapona magonjwa mbalimbali sembuse

kikombe cha Samunge ambacho tena kinaombewa kwa jina la Mungu, nendeni mkanywe mpone kwa kuwa Mungu ametuona, huduma za kiafya kwa sasa ni mbovu na zikiendelea hivyo kikombe hiki kitafika hadi wodini,” alisema.

Aliwatoa hofu wote wasioamini tiba hiyo ya kikombe cha Babu na kutoa mfano wa Askofu Mstaafu Gerald Mpango kuwa alikwenda Samunge akisumbuliwa na ugonjwa wa tezi katika
shingo na sasa amepona kwa uwezo wa Mungu.

Wakati akipongeza mabadiliko ya uongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema mambo mengine yanayovuruga amani nchini ni ushindani wa viongozi, kutopenda kutawaliwa au kuongozwa kwa baadhi ya watu, kujiamini au kutojiamini kupita kiasi, kupotea kwa kuheshimiana na matumizi mabaya ya demokrasia.

Alisema wakati Yesu Kristo alipofufuka aliwaambia wanafunzi wake amani iwe kwao, jambo ambalo Watanzania wanatakiwa walipe kipaumbele kwa chachu ya amani na kuipenda nchi yao na kukataa kuwa mashabiki wa machafuko yanayotokea Libya, Misri, Syria, Tunisia, Sudan na Somalia.

0 comments

Post a Comment