Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Kanisa lakemea Katiba mpya kugeuzwa Ilani

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KANISA Katoliki limevitahadharisha vyama vya siasa kutofanya suala la mchakato wa Katiba mpya kama Ilani ya vyama vyao, bali watambue kuwa suala hilo ni mali ya kila Mtanzania.

Aidha, limesema ikiwa vyama vya upinzani vinataka Katiba mpya ili kuking’oa Chama Tawala (CCM) madarakani na kama Chama Tawala kitaitaka Katiba ili kiendelee kutawala, itakuwa si suala la amani tena, bali hatari tupu kwa usalama wa nchi.

Hayo yamesemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Euzebius Nzigirwa katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Pasaka iliyofanyika
Kitaifa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.

Askofu Nzigirwa alisema, “nchi yetu hivi sasa ipo katika wakati wa historia, tupo katika mchakato wa kupata Katiba mpya, lakini kwa namna dalili zinavyoonekana, kuna baadhi ya wanasiasa wanataka kuandaa Katiba kama Ilani ya vyama vyao vya siasa, Katiba si mali ya chama chochote cha siasa… …ikiwa wapinzani watataka Katiba mpya ili waking’oe Chama Tawala madarakani na kama Chama Tawala kitaandika Katiba ili kukisaidia kibaki madarakani, itakuwa ni hatari kubwa, wanasiasa wasitupeleke huko.”

Alisema ikichukuliwa kama mali ya vyama vya siasa, itahatarisha amani ya nchi na utakuwa muziki mbaya ambao Bwana na Mwokozi Yesu Kristo ambaye Wakristo kote duniani waliadhimisha jana ufufuko wake, hapendi ubinafsi na aliukemea kwa nguvu zote.

Alisema katika kipindi kifupi, kumetokea mijadala kadha wa kadha katika jamii nchini
inayodhihirisha kuwa baadhi ya vyama vinachukulia suala la Katiba kama la kwao, hivyo akataka lifanyike kwa nia njema, uadilifu na maslahi ya Taifa kinyume cha hapo, historia haitamvumilia atakayetaka liwe suala binafsi.

“Suala la Katiba linahusu uhuru wangu wa kutoka sehemu moja hadi nyingine, kuabudu na kila kitu, Katiba ni uhai wa Mtanzania, ni vizuri wananchi wote wahusishwe na kusiwe na ‘mti wa katikati’ kama waliowekewa Adam na Eva katika bustani ya Eden wakala matunda, wakafa,” alisisitiza Askofu Nzigirwa.

Hata hivyo, alisema Katiba ya sasa si mbaya kiasi hicho kinachosemwa na baadhi ya watu, bali ina mambo mengi mazuri yanayofaa kuchukuliwa na kuwekwa katika Katiba mpya ili yaendelee kuwepo na kutaka katika kila jambo Mungu awekwe mbele.

Awali, akihubiri kuhusu sikukuu ya Pasaka, Nzingirwa alisema hivi sasa katika dunia kumekuwa na shida kubwa ya watu kutokupenda kupatana wanapokoseana hivyo kusababisha ndoa nyingi kuvunjika, familia kusambaratika na kuwataka Wakristo wanaposherehekea Pasaka, wakumbuke kuwa na amani na kila mtu.

“Ni Pasaka gani hiyo unayoisherehekea wewe unayekula kiapo cha kutopatana na ndugu yako
kiasi hata cha kugoma asikuzike, unasubiri kupatana mbinguni, mbingu gani hiyo?

Pasaka gani hiyo? Pasaka ni sikukuu ya kurejesha amani katika familia, jamii na nchini kwetu,” Nzigirwa aliwaasa waumini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia akizungumza mara baada ya Ibada hiyo ya Misa nje ya Kanisa, alimshukuru Askofu kwa mahubiri mazuri na kuongeza kuwa suala la Katiba kweli halipaswi kuwa la chama fulani cha siasa, bali liwashirikishe Watanzania wote.

“Tumepokea maonyo na mahubiri ya Baba Askofu, sisi kama wanasiasa ni changamoto kwetu, ni changamoto pia kwa Chama Tawala, usawa na haki izingatiwe, Katiba isichukuliwe kama suala la vyama vya siasa maana asilimia 25 pekee ya Watanzania ndio wapo katika vyama vya siasa, lakini asilimia 75 hawapo, hivyo hili ni suala la Kitaifa zaidi,” alisema Mbatia.

Katika hatua nyingine, Jumapili ijayo, Mei Mosi Kanisa Katoliki kwa mara ya kwanza litamtangaza Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II aliyefariki dunia miaka sita iliyopita kuwa
Mwenye Heri.

Mwenye Heri ni hatua ya kwanza ya kutangazwa mtu aliyekufa katika Kanisa ambaye anatarajiwa kutangazwa Mtakatifu.

Hata hivyo kutoka hatua hiyo mpaka kutangazwa Mtakatifu, hakuna muda maalumu uliowekwa na Kanisa.

Mkoani Arusha, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephati Lobulu amewataka Wakristo mkoani Arusha, kuwapuuza na kuwadharau wale wote wanaobeza dini ya wenzao kwani kwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kuepuka uvunjwaji wa amani nchini.

Askofu Lobulu akihubiri katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia, alisema wakati wa kujibishana juu ya udini hauna nafasi kwa sasa.

Aliwaomba Wakristo wawe wavumilivu na kashfa za mara kwa mara zinazotolewa juu ya Kristo kwani kwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kuokoa mambo mengi ya muhimu.

0 comments

Post a Comment