Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye |
SIKU moja baada ya Chadema kutangaza orodha mpya ya watu, kinachodai kuwa ni mafisadi ndani ya CCM, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa chama hicho tawala, Nape Nnauye amesema orodha hiyo ni sawa na mchezo wa kuigiza.
CCM katika vikao vyake vya Nec na Kamati Kuu vilivyofanyika Dodoma wiki iliyopita, kilifanya mageuzi makubwa ya uongozi na maazimio kadhaa yenye lengo la kuwaondoa wote wenye tuhuma nzito za ufisadi na ukosefu wa maadili katika kile inachokiita kujivua gamba. Lakini juzi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alirusha kombora jingine akiongeza orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho.
Akizungumza kabla na baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika jana mjini Zanzibar, Nape alisema; “Huo ni sawa na mchezo wa kuigiza. Hatua hiyo haina lolote katika mchakato wa kung'oa mafisadi ndani ya chama chetu tena nawaambia wanachofanya ni sawa na kuwasha moto juu ya petroli.”
“Bahati nzuri tumeshajua mipango yao yote ya kujaribu kuendesha kampeni ya kuchafua watu wasafi ndani ya chama akiwamo Rais na familia yake.”“Tunajua wamepanga kutumia baadhi ya vyama
vya siasa vya upinzani, viongozi wa dini, baadhi ya vyombo vya habari na waandishi. Kwa hiyo hata hiyo orodha mpya tunajua ni sehemu ya mchezo huo.”
Nape alisema mkakati huo wa kuwachafua makada wa CCM na Rais Kikwete hautafanikiwa akisema kila kitu kiko wazi.“Ni mchezo wa kuchafua watu tu lakini nawaambia mkakati huo hautaweza kukigharimu chama wala kukifanya kiachane na mchakato wa kuwashughulikia mafisadi ndani ya CCM ,” alisisitiza Nape.
Mkutano wa hadhara
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Kisonge, Mjumbe huyo wa Nec ya CCM alisema, uamuzi uliochukuliwa na chama hicho wa kujivua gamba ni mgumu na ulihitaji ujasiri mkubwa.
Alisema uamuzi huo ni sawa na mwenge ambao umewashwa Dodoma na kwamba utazunguka nchi nzima na kumulika maeneo yote ili kurejesha imani ya wananchi na wanaCCM ambao kwa muda mrefu wamekata tamaa na chama chao ambacho kinazuliwa mambo mengi machafu ikiwamo madai kuwa ni chama cha mafisadi na chama cha matajiri jambo ambalo halina ukweli.
Aliwataka wanachama wa CCM Zanzibar, kurejesha matumaini kwa chama chao huku akisisitiza kwamba uamuzi wake wa kujisafisha, unawalenga wote wenye kukidhoofisha hivyo kuwataka wale wote wenye shutuma wajitose wenyewe kabla hawajatoswa kwani wakichelewa watatoswa kwa lazima ili boti iendelee na safari yake.
“Tunawaambia kabla boti yetu haijaondoka wale wote wanaotuhumiwa ndani ya chama chetu tunataka watoke. Kama hawataki basi tutawatosa kabisa ili sisi tuendelee na safari,” alisema Nape.
Akifafanua sababu za kutoa miezi mitatu, kwa wale wote wanaotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa mbalimbali za ufisadi zilizokitia doa chama hicho, Nape alisema lengo la uamuzi huo ni kuwapa nafasi ya kujitathmini wenyewe.
Alitoa mfano wa hatua hiyo kwamba ni ; “Sawa na pweza unapotaka kumla lazima umpige na michanga hivyo miezi hiyo mitatu ni kujisafisha kabla ya kuliwa.”
Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Januari Makamba, amesema chama hicho hivi sasa kitaendeshwa kisiasa kwa lengo la kujiimarisha vyema kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema hivi sasa chama hicho kimepata wataalamu na wenye kufanya mipango kisomi zaidi kuliko kilivyokuwa mwanzo, hivyo hakuna sababu ya vijana kuvunjika moyo hasa kwa kuzingatia kuwa ndiyo waliopewa majukumu ya kukiendesha.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai alisema moja ya majukumu yake ni kukiunganisha na kukiimarisha chama hicho. Aliwataka wanachama wanaokwenda kwake kupeleka maneno yenye kukijenga na siyo fitina na majungu.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa alisema mabadiliko hayo yana lengo la kukirejesha chama katika mstari lakini akiwataka wananchi kuridhika na uamuzi huo mgumu ambao alisema hakuna chama kingine ambacho kinaweza kuiga mfano huo.
0 comments