Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - CHADEMA: Sumaye hakutajwa orodha ya mafisadi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kimetoa ufafanuzi juu ya orodha mpya ya ufisadi na mafisadi nchini, iliyosomwa juzi Mjini Tabora na Katibu Mkuu wa
chama hicho, ikiwa ni mwendelezo wa ile iliyotolewa mwaka 2007, Mwembeyanga, Dar es Salaam.

CHADEMA kimelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya taarifa ya baadhi ya vyombo vya habari jana kumnukuu Dkt. Slaa akisema kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Fredrick Sumaye ni mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi nchini, kwa mujibu katika orodha hiyo mpya.

Akizungumza jana Dar es Salaam na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Bw. Kigaila Benson, alisema kuwa wamelazimika kufafanua jambo hilo kwani hawataki kumtuhumu mtu bila kuwa na ushahidi wa tuhuma hizo, kwani kufanya
hivyo haingekuwa sahihi.

"Hili suala tumeamua kulifanyia ufafanuzi kwa sababu hatutaki wala hatuwezi kumtuhumu mtu au watu bila kuwa na ushahidi, kama mnavyojua sisi tunapoamua kusema fulani na fulani ni fisadi huwa tunaweka ushahidi bayana, kwa maana kuutaja ufisadi
waliofanya, si maneno matupu.

"Sasa imeandikwa kuwa katibu mkuu wetu Dkt. Slaa amemtaja Sumaye kuwa ni mmoja wa walioko katika orodha mpya ya mafisadi, hii si kweli, katika orodha hiyo hatukumtaja...hatusemi kuwa Sumaye ni fisadi au si fisadi, tunachosema ni kuwa sisi hatujamtaja katika orodha yetu.

"Kama kuna mtu anao ushahidi juu ya ufisadi wake anaweza kumtaja, hata sisi siku tukipata ushahidi juu ya Sumaye tutamtaja ...asubuhi nimeongea na Dkt. Slaa na Marando
(Mabere) wanasema Sumaye hakutajwa katika orodha, mazingira ambayo Dkt. Slaa alimzungumza Sumaye hayakunukuliwa sahihi," alisema Bw. Benson.

Aliongeza kuwa Dkt. Slaa alitaja jina la Bw. Sumaye alipokuwa akisema kuwa mafisadi na ufisadi ambao ameutaja mara kwa mara haujali dini, uhusiano, kabila, rangi wala umri wa mtu, hivyo akatolea mfano jinsi alivyowahi kumshambulia waziri mkuu huyo
mstaafu ambaye anatoka naye eneo moja huko Arusha, wakati akiwa madarakani kwa kushindwa kudhibiti ufisadi serikalini.

Bw. Benson pia alizungumzia kauli iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri ya Taifa (NEC) ya CCM, Bw. Nape Nnauye kuwa kuna vyama vya upinzani vimetumwa na mafisadi kumchafua Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, huku pia akidai kuwa kuna
wanasiasa wa upinzani wametumwa Tabora kufanya kazi hiyo hiyo.

"Unajua kitu kimoja ambacho mtu mwenye akili hawezi kuwaelewa CCM, hususan wanapoamua kutuhumu, wanaimba sana ngonjera. Unapoamua kusema kuwa kuna mafisadi wanatumia vyama vya upinzani kumchafua rais, ili ueleweke na kuaminika unawataja hao mafisadi
au huyo fisadi na vyama au chama kinachotumika.

"Ndiyo maana sisi tunapenda kuwaonesha njia sahihi ili wajikosoe vizuri, tukitaja mafisadi tunaonesha na ufisadi wao, hatubahatishi, sasa wao wanaimba tu ooh tunawapatia mafisadi siku tisini wajiuzulu lakini hawana ubavu wa kuwasema kwa
majina hao mafisadi ni akina nani na ufisadi wao uko wapi na wanachukua hatua gani za kisheria juu ya ufisadi wao.

"Tena sasa wanataka kuleta utamaduni mbaya sana ambao utatengeneza mwanya kwa watu walioko madarakani kufanya ufisadi maana wanajua wataambiwa wajiuzulu tu, hakutakuwa na hatua za kisheria juu ya yao, tulitegemea kwa chama chenye serikali kama CCM, kuiagiza serikali kuchukua hatua si kulalamika au kuimba ngonjera kama wanavyofanya sasa."

Bw. Benson alisema kuwa si sahihi watu wanaotuhumiwa ufisadi katika chama kinachounda serikali, huku wakiwa na dhamana ya uongozi sehemu zote mbili, kuachia nafasi zao ndani ya chama husika pekee, badala ya kuchunguzwa, kisha kufikishwa
mahakamani kwa ajili ya hatua za kisheria.

"Alitakiwa ataje jina la huyo fisadi au mafisadi na hivyo vyama vya upinzani. Pia fisadi ni mwizi, amefilisi taifa, raslimali za nchi sasa unaposema ajiuzulu nini kinafuata sasa, mwizi anakamatwa, mwizi hasemwi tu, sisi hatuna serikali sasa, lakini
tumewataja, hawa wana serikali mbona hawachukui hatua."

Juzi katika mkutano wake wa ujenzi wa chama hicho mkoani Tabora, Dkt. Slaa akiwa na pamoja makada wengine wa chama hicho, wakiwemo wanasheria Profesa Abdalla Safari na Mabere Marando pamoja na baadhi ya wakurugenzi na maofisa wa chama hicho walitaja
orodha ya watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Dkt. Slaa ambaye aliwahi kutoa orodha aliyoita ya aibu ya watuhumiwa 11 wa ufisadi mkubwa unaolifilisi taifa, mwaka 2007, juzi aliongeza majina mengine matatu, ambapo alimtaja Dkt. John Magufuli kuhusiana na uuzaji wa nyumba za serikali, Bw. Phillip Mangula na Dkt. John Malecela kuhusiana na Fedha za EPA, huku
akimtaja Rais Kikwete kwa kushindwa kuwachukulia hatua mafisadi na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, katika uuzaji wa nyumba za serikali bila kufuata utaratibu. 

0 comments

Post a Comment