Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - CCM yatamba haiogopi mafisadi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter



KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema uamuzi wa chama hicho kuwapa miezi mitatu wajumbe wa NEC wanaotuhumiwa kwa ufisadi, haina maana ya kuwaogopa.

Bali amesema ni utaratibu uliowekwa akiufananisha na wavuvi wa pweza wanapomtengeneza kwa ajili ya kuliwa supu kirahisi.

“Msiwe na wasiwasi ni kama kumvua pweza baharini, akifika nchi kavu unamtandika mikwaju kisha mnampika baada ya kulainika na ndivyo tafsiri ya muda waliopewa,” alisema Nape Aprili 17 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembe Kisonge, mjini hapa.

Nape alikilinganisha na kitendo cha kujivua gamba kwa CCM na kuwasha Mwenge unaomulika kwenye chuki, pasipo na matumaini, pasipokuwa na nidhamu na kupaweka sawa na kwamba Mwenge huo hautazimika.

Sekretarieti mpya ya CCM iliyopokewa kwa kishindo visiwani hapa ilitangaza operesheni fagio la chuma ndani ya chama, kwamba inaanzia ngazi ya tawi kuwataka viongozi wenye tuhuma kujivua gamba wenyewe.

Wakihutubia kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara, viongozi hao walisema CCM imeamua kuwasha Mwenge nchi nzima na kuleta matumaini mapya kwa Watanzania.

Nape alisema baada ya kuanza kwa operesheni ‘jivua gamba’ baadhi ya watu waliotoswa ndani ya chama hicho wameanza kutumia baadhi ya vyama vya upinzani, vyombo vya habari na hata wasanii.

“Tunazo taarifa kwamba baadhi ya watu waliotoswa katika chama chetu wameanza kutumia magazeti. Tunawaambia hawatashinda vita hivyo, CCM ni chama kikubwa na makini,” alisema Nape huku akishangiliwa na wana CCM wa hapa.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati, aliwataka wanachama wanaojiona wamechafuka ama kwa tuhuma za ufisadi kuanzia ngazi ya matawi, majimbo, wilaya, mikoa na kwenye NEC wajiondoe kwenye nyadhifa zao.

“Tunapenda kuwahakikishia wananchi kuwa safishasafisha ya CCM itaendelea hadi kwenye matawi...tunataka chama chenye nidhamu,” aliahidi Chiligati.

Chiligati alisema anawashangaa wanaobeza uamuzi wa NEC kujiuzulu kuwa wajaribu katika vyama vyao, kama havikusambaratika, kwani ni uamuzi mgumu ambao CCM iliuchukua na imevuka salama.

“Kuachia ngazi ni jambo gumu sana na si la kubeza hata kidogo, tumelazimika kujiuzulu kukinusuru chama, ingelikuwa vile vyama vingine mngevisikia vimesambaratika … wajaribu
waone,” alisema Chiligati.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, mbali ya kuelezea historia ya kujivua gamba kwa chama hicho, alielezea mpango mkakati wa CCM katika kujenga chama kipya chenye matumaini kwa Watanzania.

0 comments

Post a Comment