KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amemtaka Rais Jakaya Kikwete awataje watuhumiwa wa ufisadi na kisha kuwavua nyadhifa zao zote na kisha kuwafikisha mahakamani katika muda wa siku 90 kama kweli anataka kukivua gamba chama hicho.
Kauli hiyo ya Chadema kwa Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya CCM kuchukua hatua katika kile ilichokiita kujivua magamba kwa kuwataka watuhumiwa wote wanaotajwa kuhusika katika kashfa kadhaa za ufisadi, kujiondoa wenyewe katika nafasi zao ndani ya chama hicho katika kipindi cha miezi mitatu vinginevyo watawajibishwa.
Jana, akiwa kwenye Uwanja wa Kaliua, Urambo Magharibi, Dk Slaa alisema kama kweli Rais Kikwete amedhamiria kukivua gamba chama chake, anapaswa kuuthibitishia umma kwa kufanya hivyo vinginevyo itakuwa ni ‘usanii.’
Kwa mujibu wa Dk Slaa, endapo watuhumiwa hao watatajwa na kuchukuliwa hatua ikiwamo kuvuliwa nafasi zao na uanachama na kupoteza ubunge au kufukuzwa serikalini, dhana hiyo ya kujivua gamba itakuwa na mantiki.
Dk Slaa alisema, Watanzania wanataka kuona fedha zao zilizoibwa na mafisadi zinarejeshwa na watuhumiwa kufikishwa mahakamani, hivyo haitoshi kusema neno kujivua gamba.
Mwanachama mwingine maarufu wa Chadema, Frederick Mpendazoe ambaye aligombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho, Jimbo la Segerea katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alisema endapo CCM kitashughulikia watuhumiwa hao wa ufisadi ndani ya siku 90 ni dhahiri kutafanyika uchaguzi kutokana na kile alichodai kwamba ni kuwa na wabunge wengi waliingia madarakani kwa njia ya rushwa.
Alidai kwamba CCM imepoteza mwelekeo kutokana na kuhodhiwa na watu wenye malengo ya kibiashara ambao huchochea ufisadi unaokigharimu sasa.
Mpendazoe ambaye aliwahi kuwa kada wa chama hicho tawala alisema miaka ya nyuma wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, CCM kilikuwa madhubuti kutokana na kuwa na viongozi waliokuwa tayari kupambana na rushwa na ukosefu wa maadili ya uongozi, hali ambayo ni tofauti kwa sasa.
Mpendazoe ambaye alijiondoa CCM kutokana na kile alichodai kuwa ni fitina za mafisadi alisema uongozi ndani ya chama hicho tawala kwa sasa ni uwekezaji akisema asiye na fedha ni vigumu kupata uongozi.
Alisema kutokana hali hiyo, hata ile misingi ya waasisi iliyojengwa katika miaka ya 1960 na 1970 imebomolewa na mafisadi kushika hatamu za uongozi wa chama hicho tawala.
Mpendazoe alisema Serikali iliyopo ni ya kidemokrasia lakini imekuwa ikiyapa kisogo matatizo ya wananchi wa tabaka la chini na kukumbatia wafanyabiashara ambao wana nguvu ndani ya chama hicho.
Kuhusu muswada wa Sheria ya Marejeo ya Katiba, alisema hadi sasa serikali imeuondoa muswada huo bila kuweka mambo wazi na kuonya kama ukirejea kama ulivyo na tume ikiundwa na rais chama hicho kitaandamana.
0 comments