SASA ni dhahiri kuwa Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, ana siri nzito kuhusiana na madai kwamba ameandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete, akikusudia kujiuzulu.
Katika hali iliyotafsiriwa kuwa waziri huyo anaepuka kutoa mwenyewe msimamo wa kujifunga moja kwa moja kuhusu kuwa na nia ya kujiuzulu au kutojiuzulu, jana Katibu wa Wizara yake, Herbert Mrango, ndiye aliyejitokeza kukanusha taarifa zilizoandikwa na baadhi ya magazeti zilizohusu kujiuzulu kwake.
Mrango akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, alisema habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti: “Magufuli Ajiuzulu” au “Magufuli Azushiwa Kujiuzulu” si za kweli, huku akikataa katakata kuulizwa swali lolote kuhusu undani wa taarifa hizo zinazomhusu mkuu wake.
“Mheshimiwa waziri anaendelea na kazi zake vizuri, alikuwepo ofisini jana na leo yupo; na anaendelea na programu zake za kazi kama kawaida.
“Tunawaomba muwahakikishie wananchi kwamba Waziri Magufuli hajajiuzulu, hajawahi kuwa na wazo la kujiuzulu na hana sababu ya kujiuzulu,” alisema Mrango.
Hata waandishi walipong’ang’ania kumuuliza maswali, Mrango aliwataka wamtafute siku nyingine za kukutana kwa ajili ya maswali bali siku hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kutoa taarifa fupi.
“Hiyo ndiyo taarifa fupi nimemaliza sihitaji maswali kwa kuwa sina majibu na kama mnataka kuuliza maswali naomba mnitafute siku nyingine tukutane kwa ajili ya hiyo, asanteni,” alisema Mrango na kunyanyuka huku akitoka nje ya ukumbi huo.
Taarifa zinadai kuwa katika majumuisho ya ziara ya Waziri Mkuu Pinda baada ya kauli hiyo mkoani Kagera , Magufuli alilazimika kueleza kuwa amefikia hatua ya kuamua kuchukua maamuzi magumu baada ya kubaini kuwa hataweza kutekeleza vema utawala wa sheria ambao umeonekana kupindishwa.
Chanzo kimoja kilicho karibu na waziri huyo kililidokeza gazeti hili kuwa alifikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kusikitishwa na kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ya kusitisha zoezi la bomoa bomoa lililokwishaanza katika baadhi ya maeneo nchini.
“Ni kweli baada ya kutolewa kauli ile kule mkoani Kagera katika kikao chetu cha majumuisho ya ziara hiyo Magufuli alisikitishwa na kauli ile ambapo aliweka bayana kuchukua maamuzi magumu hatua ambayo haikukubaliwa na viongozi waliokuwa katika ziara hiyo,” kilisema chanzo hicho.
Taarifa za kujiuzulu kwa Waziri Magufuli zimeonekana kuwashtua baadhi ya viongozi kutokana na baadhi ya watendaji kujaribu kupeleleza wananchi wamepokeaje juu ya kuzagaa kwa taarifa hizo.
Taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa ni kweli Magufuli alifikia uamuzi huo hata baada ya kushauriwa na viongozi mkoani humo na kuamua kuandika notisi ikiwa ni njia ya kutaka kumtikisa Waziri Pinda ambayo hajaikabidhi kwa wahusika.
0 comments