Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Vikosi vya Gaddafi vyashambulia Benghazi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Obama aionya Libya kujiandaa na hatua za kijeshi

Vikosi vya kiongozi wa Libya Mohamar Gaddafi vimeendelea kushambulia kwa mizinga viunga vya mji wa Benghazi ambao ni ngome kuu ya waasi licha ya tangazo la serikali hapo jana kwamba inasitisha mapigano mara moja.
Takriban mashambulizi mawili ya anga yamefanyika dhidi ya kiunga katika eneo la kusini na mashambulizi ya mizinga yamekuwa yakiendelea huku ndege moja ya kivita ikisemekana kuwa imeanguka na kuripuka.
Waasi ambao wamekuwa wakijaribu kumpinduwa  Gaddafi kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa wanasema vikosi vyake vimekuwa vikiendelea kushambulia miji na hivyo kuendelea kukiuka usitishwaji wa mapigano tokea kutangazwa kwake.
Serikali kwa upande wake imesema vikosi vyake vimekuwa vikishambuliwa magharibi mwa Benghazi na vilijibu mapigo ili kujihami.Libya hapo jana ilitangaza kusitisha mara moja operesheni zake zote za kijeshi dhidi ya waasi baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio lenye kuweka marufuku ya kuruka ndege kwenye anga ya Libya.

Rais Barack Obama ameonya juu ya matumizi ya nguvu za kijeshi, iwapo kiongozi wa Libya Kanali Muhammar Gaddafi hatosimamisha mashambulizi yake dhidi ya waasi.

Rais Obama amesema hakuna mjadala juu ya yale yaliyomo katika azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo ni kuwalinda raia.Ufaransa na Uingereza pamoja na nchi nyengine za kiarabu zinatarajiwa kuongoza juhudi za mashambulizi ya anga dhidi ya Libya
Wakati huo huo viongozi wa mataifa kadhaa duniani wanakutana hii leo huko mjini Paris Ufaransa, kabla ya kufanyika kwa mkutano utakaoamua jinsi ya kutekeleza azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la vikwazo vya anga dhidi ya Libya.
Mkutano huo unawajumuisha viongozi kutoka Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ya Kiarabu.Viongozi wa mataifa duniani wamesema kuwa ni muhimu kuwalinda wananchi wa kawaida nchini Libya ambao wamenaswa katika mapigano kati ya majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Kanali Mohamar Gaddafi na waasi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton anaudhuria mkutano huo pamoja na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ijapokuwa nchi yake ilisusia kupiga kura juu ya azimio hilo huko New York.
Kansela Merkel alisema hatua hiyo ya Ujerumani kujiondoa katika kupiga kura kusichanganywe na kutoegemea kwa nchi hiyo upande wowote.

Tags:

0 comments

Post a Comment