| Some parts of Snow Crest Hotel's fence being demolished today for allegedly encroaching road reserve. Demolition of the entire parking lot was at an advanced stage. (Photo by MARC NKWAME). |
Mussa Juma,Arusha. HOTELI ya kisasa ya kitalii ya Snow Crest, ambayo ilizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki mjini Arusha, imebomolewa kwa madai kuwa ilijengwa katika eneo la akiba ya barabara kuu ya Moshi-Arusha. Mara baada ya kuizindua hoteli hiyo, Rais Kikwete aliisifia kuwa imejengwa vizuri licha ya kuwa katika eneo dogo, lakini saa 36 baadaye uzio wake wote, bustani na eneo la kuegesha magari vilibomolewa na kusababisha mawasiliano yote ya simu hotelini humo kukatika. Kitendo cha kubomoa sehemu hizo muhimu za hoteli hiyo muda mfupi baada ya kuzinduliwa na kiongozi huyo wa nchi, kimepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi ambao wengi wamesema kinamdhalilisha rais na idara ya usalama wa taifa. Akizungumza na waandishi wa habari jana, mkurugenzi wa hoteli hiyo, Wilfred Tarimo alisema maafisa wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Arusha pamoja na askari sita walienda hotelini hapo jana alfajiri saa 11:30 na kuanza kubomoa sehemu hizo. "Kitendo hiki kimetusababishia hasara kubwa sana kwa kuwa tulikuwa na wageni 40 kutoka nje ya nchi ambao wameshangazwa na hali hii na wameondoka bila hata kupata kifungua kinywa na simu zote za hoteli zimekatwa," alilalamika Tarimo. Mkurugenzi huyo alisema hakuna tahadhari yoyote ambayo ilichukuliwa na maofisa hao wa Tanroads na polisi na hivyo nusura hoteli hiyo iteketee kwa moto kutokana na kukatwa nyaya mbalimbali. Tarimo alisema mwezi Novemba walipokea notisi ya kuondoa uzio wa hoteli na baadaye walifanya mazungumzo na meneja wa Tanroads mkoani Arusha, Deosdedith Kikoko ambaye aliwaruhusu kuendelea na ujenzi na ukarabati wa eneo hilo. "Tuna barua ya kuruhusu ujenzi wa bustani mbele ya hoteli na pia kuwa na uzio usio wa kudumu, lakini tunashangaa wamevunja kila kitu hata eneo la maegesho ya magari," alisema Tarimo. Mkurugenzi huyo alisema tangu kuanza kubomolewa sehemu ya hoteli hiyo, wamekuwa wakipokea simu za wateja kukatisha kupanga katika hoteli hiyo huku wateja waliopo wameomba kuhama. "Hadi sasa kuna hasara ya zaidi ya Sh10 milioni kwa kuharibu bustani tu, bado kuna kuvunjwa uzio; kuvunjwa taa mbali mbali; kuondolewa eneo la maegesho ya magari na kukatwa mawasiliano ya simu," alisema Tarimo. Diwani wa Kata ya Baraa ilipo hoteli hiyo, Lota Laizer alisema wamesikitishwa na kitendo cha Tanroads kubomoa hoteli hiyo bila ya taarifa rasmi na bila kumheshimu Rais Kikwete ambaye aliifungua. "Huku ni kumdhalilisha rais; iweje wabomoe sasa. Hoteli hii ina miezi tisa sasa na walikuwepo wakati inajengwa sasa wameona rais kaifungua ndio wanabomoa hili ni jambo la ajabu," alisema Laizer. Hata hivyo, Kakoko alisema wamebomoa hoteli hiyo baada ya kujengwa katika eneo la hifadhi ya barabara. "Mimi sina cha kusema ni kweli tumebomoa na hakuna sheria tuliyokiuka kwani tuliwahi kuwapa notisi,"alisema Kakoko, ambaye aliahidi kukutana na waandishi jana mchana, lakini hakuweza kutokana na kuitwa ofisini kwa mkuu wa mkoa, Isidori Shirima. Rais Kikwete aliwahi kukataa kukabidhi pikipiki zilizotolewa na mfanyabiashara mmoja wa Arusha kwa ajili ya shughuli za CCM kutokana na mtoaji huyo kuhusishwa na tuhuma za ufisadi. |
0 comments