RAIS wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Mwashamu Thadeus Rwaichi amekemea kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wana CCM za kulihusisha kanisa hilo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Rwaichi alitoa kauli hiyo Gairo wakati wa mapokezi ya Mwashamu Gervas Nyaisonga ambaye anatarajiwa kusimikwa leo kuwa askofu mteule wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma.
Hafla ambayo itahudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Polycap Kardinali Pengo.
Akizungumzia tuhuma za kulihusisha kanisa hilo na CHADEMA, rais huyo wa TEC aliwataka watu warejee historia kwani awali Dk. Slaa alikuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na leo amehama na kujiunga na CHADEMA na kuagiza CCM ihojiwe imelipokeaje suala la Dk. Slaa kukihama chama hicho kama alivyoacha nyadhifa alizokuwa nazo ndani ya kanisa Katoliki ambapo alisema kama CCM wakijibu swali hilo itakuwa vizuri.
Rwaichi alitaka kujua CCM ina mchango gani katika suala hilo la Dk. Slaa kuhama chama na si kukurupuka na kulitupia Kanisa Katoliki kauli za ajabu zisizo na ukweli ndani yake.
Askofu Rwaichi alisema kuwa ndani ya Kanisa Katoliki kuna waumini ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa, kama ilivyo kwa Waislamu na wapagani na kwamba kila mtu ana uhuru wa kujiunga na chama chochote anachokipenda.
Alisema kuwa Kanisa Katoliki halina chama ila linafanya kazi kwa msimamo ulio wazi na unaojali maslahi ya watu wote.
“Naomba nilisisitize hilo la Kanisa Katoliki kufanya kazi kwa maslahi ya watu wote bila kubagua na nilishalisema hili kwenye vyombo vya habari,” alisisitiza Rwaichi.
Aliwataka viongozi kuzidodosa kauli hizo ambazo alisema ni kauli za baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na waandishi wa habari ambazo zinakanganya.
Alisema anashindwa kuelewa ni kwa sababu gani Kanisa Katoliki linahusishwa na CHADEMA au kwa kuwa sababu Dk. willbrod Slaa alikuwa Mkatoliki na akagombea urais?
“CCM siku hizi imekuwa ikipigiwa debe na kutetewa na madhehebu ya dini fulani je kwa kigezo hicho nayo ni chama cha madhehebu hayo yanayokibeba na kukipigia debe?” alihoji askofu huyo.
Alisema watu wote wakiwemo waandishi wa habari wamepewa kipaji cha akili na maarifa ya kuchambua mambo kwa kina hivyo wasimeze kiholela kauli za kurubuni.
Aidha aliwataka kutumia akili hizo walizopewa kuchambua mambo bila kukanganya lakini kwa kutoa na kuandika ukweli kwa watu bila kubagua misingi ya dini, kabila wala chama chochote cha siasa.
Akizungumzia suala lililojitokeza hivi sasa la viongozi wa dini kudaiwa kuingilia vyama vya siasa, alisema kuwa viongozi wa dini kuzungumzia siasa sio kuingilia bali wana wajibu wa kutoa kauli za kuwasaidia wananchi.
Alisema viongozi wa dini wakikaa kimya bila kusemea kauli zinazotolewa na wanasiasa ambazo nyingi ni za kupotosha watakuwa hawalitendei haki taifa.
Aidha alisema kuwa viongozi wa dini wana wajibu wa kutunza dini na maadili na si kukaa kimya wakati maadili yanaporomoka na huku watu wakitoa kauli zinazovuruga amani ya nchi.
0 comments