WANANCHI wa kijiji cha Pande B katika mkoani Tanga jana walimzuia kwenye mvua mbunge wa viti maalum mkoa wa Tanga, Amina Mohamed Mwidau (CUF), wakitaka kujua sababu ya uongozi wa halmashauri hiyo kuuza ardhi yao hekari zaidi ya 370.
Ardhi hiyo inadaiwa kuuzwa kwa mwekezaji wa kiwanda cha Tanga Cement bila kulipwa fidia zao kama walivyotegemea.
Mbali ya kufikisha maombi hayo kwa mbunge Mwidau bado wananchi hao walidai kuwa wamefikisha kilio chao kwa mkuu wa mkoa wa Tanga na Rais Jakaya Kikwete bila kujibiwa na kuomba Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa chini ya mwenyekiti wake mbunge wa jimbo la Vunjo, Augustino Mrema, na Waziri wa Ardhi na Makazi Prof. Anna Tibaijuka kutembelea jiji la Tanga kuona viongozi wanavyoendekeza ufisadi katika ardhi.
Wananchi hao walifikia uamuzi huo juzi wakati wa mkutano wa mbunge huyo kwa ajili ya kuvunja makundi ya kisiasa na kuhamasisha wananchi kuanzisha vikundi vya kiuchumi; mkutano uliofanyika katika mtaa wa Pande B.
Pamoja na mvua kubwa kuanza kunyesha mara baada ya mbunge huyo kumaliza kuwahutubia bado wananchi hao walimtaka mbunge huyo pamoja na msafara wake kuendelea kukaa nje kwenye mvua huku baadhi yao wakikaa katika madimbwi ya maji ya mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha, wakimtaka mbunge huyo kusikiliza kilio chao kuhusu kupokonywa ardhi yao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake kiongozi wa wananchi hao wanaodai kutapeliwa ardhi yao, Mohamed Issa, alisema kuwa utaratibu wa kuiuza ardhi hiyo hekari 371 kutoka kwa wananchi kwenda kwa Kiwanda cha Saruji Tanga haujazingatia sheria za umilikishaji ardhi zaidi ya halmashauri ya jiji la Tanga kutumia nguvu kupokonya eneo hilo kwa maslahi binafsi.
Mbali ya halmashauri hiyo kuhusishwa na ufisadi huo wa ardhi bado alisema kuwa viongozi wa serikali ya kijiji hicho akiwemo mwenyekiti na afisa mtendaji wamefanya utapeli wa kutisha katika zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza majina yao na ndugu zao ili kupatiwa fidia bila kuwa na ardhi katika eneo hilo.
Pia alisema kuwa wakati halmashauri ya jiji la Tanga likifika katika kijiji hicho kutaka wapishe eneo hilo kwa ajili ya mwekezaji, walifanya hivyo bila kuwapa fomu namba 69 kwa ajili ya kuthaminisha ardhi na mali zilizo katika eneo husika ambalo linapaswa kubadilishwa matumizi ya awali.
Alisema kuwa wananchi halali ambao wamo katika mgao wa fedha za fidia katika eneo hilo ni 30 ila viongozi wa kijiji kwa kushirikiana na halmashauri wamefoji majina hewa 36 ili kuingika katika mgao wa fedha hizo.
Pia wananchi hao walihoji sababu ya fedha za fidia kwa wananchi wote kufanana bila kujali ukubwa na mali zilizomo.
Kwa upande wake mbunge Mwidau aliwataka wananchi hao kuvuta subira na kuwa lazima atazungumza na kamati hiyo ya Mrema ili ifike katika mkoa wa Tanga hasa halmashauri ya jiji ili kusafisha rushwa na ufisadi uliopo katika idara ya ardhi.
Mkurugenzi wa jiji la Tanga John Gikene alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alikiri kuwepo kwa dosari katika zoezi hilo na kuwa wananchi hao wana chuki na kuwataka viongozi wao wa kijiji kuondoka madarakani.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na kuwa yuko likizo kwa ajili ya kustaafu kazi hiyo ila amepata kulishughulikia vya kutosha suala hilo na kuwa si kweli kama halmashauri ina maslahi binafsi katika suala hilo.
0 comments