Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kikwete acharuka, amtaka Ngeleja awe makini

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
RAIS Jakaya Kikwete amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kuwa makini na utatuzi wa suala hilo ili kuiepusha nchi kuingia katika kashfa kama iliyosababishwa na Mkataba wa Richmond.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ameagiza kuwekwa pembeni kwa ushabiki wa kisiasa katika utekelezaji wa miradi ya uzalishaji umeme ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya kuzalisha zaidi ya megawati 1,130 za umeme ifikapo mwaka 2013.

Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na maofisa wa Idara na Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini katika ziara yake ya kikazi ya siku moja kwa wizara hiyo jana.

“Katika suala hili la uzalishaji wa umeme wa dharura, naomba tujifunze kutokana na historia. Nakumbuka suala la Richmond lilitokana na suala kama hili la uzalishaji wa umeme wa dharura.
“Nililisema hili pale katika kikao cha Baraza la Mawaziri, shughuli hizi zote za uzalishaji wa umeme wa dharura zianzie na kuishia palepale Tanesco. Bodi ya Tanesco isimamie mchakato mzima bila kuingiliwa na wizara, naomba tusirudi tena kule,” alisema Rais Kikwete.
Kabla, Waziri Ngeleja alisema Wizara yake inachukua mikakati mbalimbali ya muda mrefu, muda wa kati na mikakati ya dharura katika kukabiliana na matatizo ya umeme nchini.
Kuhusu mikakati ya dharura inayochukuliwa sasa ni kuagizwa kwa majenereta ya kufua umeme yanayotumia mafuta mazito yenye uwezo wa kuzalisha megawati 260 ambapo jana ilikuwa mwisho wa kupokea nyaraka za zabuni kwa ajili ya uagizwaji wake.
“Mheshimiwa Rais, ni imani yetu kwamba katika wiki ya pili au ya tatu ya Mwezi Aprili, mwaka huu, majenereta haya yatakuwa yamewasili na lengo letu ni kuona kuwa umeme unaanza kuzalishwa ifikapo mwezi wa saba,” alisema Ngeleja.
Waziri alisema pamoja na mpango huo wa dharura ni matumaini ya Wizara hiyo kuona kuwa kunakuwa na uzalishaji wa megawati 1,130 za umeme zitakazoingizwa kwenye gridi ya taifa ifikapo mwaka 2013 kutokana na kukamilika na kuanza kazi kwa miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ule wa Kiwira (Mbeya) utakaozalisha megawati 200, Mnazi Bay (Mtwara) megawati 300, Kinyerezi (Dar es Salaam) utakaozalisha megawati 240 na Mwanza megawati 60.
Waziri Ngeleja alitaja mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika miradi ya umeme inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) yenye miradi 41 sasa, miradi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), miradi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na miradi ya uzalishaji umeme kupitia majenereta na mitambo inayosimamiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumzia miradi hiyo, Rais Kikwete alisema itaweza kukamilika kama ilivyopangwa kama watendaji ndani ya wizara hiyo watapeleka nguvu na fikra zao katika utekelezaji wa miradi na si maneno yasiyokuwa na nia ya dhati na ya kisiasa.
“Lengo langu ni kuona tunaondokana kabisa na umeme wa maji.Tukiweza kupata umeme wa Mtwara na Kiwira tu utaweza kabisa kutufanya tuachane na umeme wa Mtera na Kidatu. Umeme wa maji uwe umeme wa ziada na si tegemeo kama ilivyo sasa.
“Mradi wa Kiwira haukuweza kukamilika kutokana na siasa kuingia ndani yake, lakini sasa mradi umerejeshwa serikalini na kuna hatua zinaendelea kuchukuliwa ili mradi uanze uzalishaji upya, hili likitekelezwa tutakuwa mbali,” alisema.
Rais pia alieleza kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na mikakati inayochukuliwa na Taneso chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi William Mhando na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) chini ya Mkurugenzi Mkuu, Haruna Masebu katika kuongeza miradi ya uzalishaji wa umeme na usambazaji.
Alisema ili kufikia lengo la Wizara ya Nishati na Madini la kuona umeme unawafikia asilimia 30 ya Watanzania nchi nzima kutoka asilimia 14 za sasa ifikapo mwaka 2015, jitihada za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa na vyombo husika hasa REA, Ewura na Tanesco ili kuhakikisha miradi yote iliyoainishwa inatekelezwa.
Kampuni ya Richmond ilipewa zabuni na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, ili kuzalisha umeme wa dharura baada ya nchi kukumbwa na nakisi kubwa ya umeme mwaka 2006 kutokana na kukauka kwa maji katika Bwawa la Mtera, kazi ambayo kampuni hiyo ilishindwa kuifanya.
Hatua hiyo ilisababisha Bunge kuunda Kamati Teule ili kuchunguza mazingira ya mkataba huo baina ya serikali na Richmond chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, iliyobaini kuwa kampuni hiyo ilikuwa hewa na haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kama ilivyodai kwa serikali.
Kutokana na kitendo hicho Kamati hiyo ilipendekeza kujiuzulu kwa viongozi wa serikali waliohusika na mkataba huo wa Richmond kwa kuiingiza nchi katika hasara, hatua iliyomfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, kujiuzulu Februari 2008 na kumlazimisha Rais Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri.
Tags:

0 comments

Post a Comment