KANISA Katoliki katika Jimbo la Mpanda mkoani Katavi, limeagiza kurudishwa kwa msaada uliotolewa na Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM), Moshi Kakoso kwa ajili ya kusaidia vigango vya Parokia ya Karema.
Agizo hilo linatokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kanisa kukerwa na hatua ya uongozi wa CCM wilayani Mpanda, kulikashifu.
Habari zilisema agizo hilo lilitolewa juzi na Makamu Askofu wa Jimbo hilo, Padri Patrick Kasomo, ambaye pia ni Paroko wa Karema, kufuatia maneno ya kejeli na kashfa yanayodaiwa kuwa yalitolewa na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mpanda.
Padri Kasomo alidai kuwa Katibu huyo wa CCM alitoa kashfa hizo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, ulioitishwa na mbunge huyo kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua.
Hata hivyo alipoulizwa kuhusu madai hayo, Katibu huyo Jacob Nkomola, alisema hakusema maneno hayo dhidi ya kiongozi huyo wa kanisa na kwamba kilichopo ni mgogoro baina ya wananchi na kanisa baada ya Padri Kasomo kupora sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji, yakiwemo maeneo ya wazi.
Alidai kuwa maeneo hayo ni pamoja la uwanja wa kuchezea mpira, ambao alipitisha trekta na kuubadilisha kwa ajili ya shughuli za kilimo.
"Nilichozungumza kwenye mkutano wa hadhara ni kwamba kiongozi wa dini anayevaa msalaba na kanzu anatakiwa kuwa mkweli, sasa huyu padri anaingiza ushabiki wa kisiasa, yeye tangu wakati wa uchaguzi alikuwa akipigia kampeni Chadema na anafanya hivi huku akipora maeneo ya wazi ili kumkwamisha diwani wa CCM aliyeshinda katika Kata ya Karema," alidai katibu huyo katika mazungumzo ya njia ya simu.
Msaada uliokataliwa ni wa Sh300,000 zilizotolewa kwa nyakati tofauti katika vigango vya Kaparamsenga, Ikola, na Karema.
Kila kigango kilipewa kilipata Sh 100,000 ikiwa ni msaada kutoka kwa mwanasiasa huyo.
Padri Kasomo alidai kuwa katika mkutano huo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mpanda, alimkashifu yeye na imani ya kanisa.
Alisema kuwa mtendaji huyo wa CCM aliwasalimia wananchi kwa salamu inayotumiwa na Kanisa hilo Katoliki inayosema ‘Kristu’ na kujibiwa tumaini letu lakini mtendaji huyo alisema tumaini liwe kwenu tu si kwa padri wenu Kasomo,fisadi ambaye hastahili kuwa kiongozi wa kiroho .
Padri huyo alidai kuwa kejeli na kashfa hizo zilizotolewa mbele ya waumini wake.
Alidai katibu huyo aliwataka waumini wa kanisa kuandamana kwenda parokiani kumvua kanzu ya upadri
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Dk Rajab Rutengwe alipohojiwa kwa njia ya simu alikiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa Makamu wa Askofu Kasomo.
0 comments